Muuguzi, dereva gari la wagonjwa wafa ajalini

 


Same. Muuguzi wa zahanati ya Kisiwani na dereva wa gari la wagonjwa, wamefariki dunia baada ya gari hilo kupinduka na kupoteza mwelekeo wakati wakimuwahisha mgonjwa Hospitali ya Wilaya ya Same.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha leo Agosti 8, 2021 kutokea kwa ajali hiyo jana jioni  katika barabara ta Same kisiwani, eneo la Majevu, Kata ya Kisima,  wilayani Same.

Amewataja waliofariki dunia kuwa ni muuguzi wa zahanati hiyo, Joshua Methew (29) na dereva  Jumanne Makumbe (48).

Wengine ambao wamejeruhiwa ni Ester Laizer (35), Magdalena Kuvaa (45) na Paresetwi Peutu (50).

Kamanda Maigwa amesema chanzo cha ajali hiyo ni gari hilo kupasuka tairi la nyuma na kupoteza mwelekeo kisha kupinduka.

"Gari hili lilikuwa likitokea zahanati ya Kisiwani kuelekea Hospitali ya Wilaya ya Same likiwa limebeba mgonjwa. Lilipasuka tairi la nyuma na kupoteza mwelekeo na kutoka nje ya barabara na kupinduka," amesema Kamanda Maigwa.

Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Same na majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post