TUNAISHI katika dunia ya mitandao. Mchezaji anayeitwa Clatous Chama aliamua kwenda mubashara kwa mashabiki wake katika mtandao wake wa kijamii unaoitwa Instagram. Akaanza kujibu maswali ya mashabiki wake pamoja na kuchangia mijadala mbalimbali inayohusu klabu yao.
Likatokea swali linalomhusu msemaji wa zamani wa klabu hiyo, Haji Manara. Chama akajibu kwa kuonyesha anamkubali msemaji huyo. Ghafla akaibuka tajiri wa klabu na kumuuliza Chama swali la kebehi. “Nani alikulipa pesa za kusaini mkataba mpya?”
Tajiri na msemaji hawaelewani. Tajiri alichukizwa na namna Chama alivyoonekana kumkubali msemaji wa zamani ambaye kwa sasa ni adui yake. Nafungua rasmi mjadala wa kawaida tu ambao wote inabidi tukae chini na kujadili.
Kwa nini klabu ilitaka Chama aongeze mkataba? Kwa sababu ni mchezaji staa ambaye alikuwa anawindwa kwa udi na uvumba na watani zao pamoja na klabu nyingine mbalimbali. Nani hataki kuwa na mchezaji kama Chama kwa sasa?
Chama hajali nani alitoa pesa au nani hakutoa pesa. Alichojali ni pesa kuwekwa mezani ili asaini mkataba mpya. Bahati nzuri kwake ni pesa haikujileta mezani kwa bahati mbaya. Ameifanyia kazi. Kitendo cha kutakiwa na timu nyingine ni kwa sababu alikuwa ameifanya kazi yake vyema klabuni.
Hata maadui ambao walikuwa wamemwinda ni kwa sababu alikuwa ameifanya kazi yake vizuri hapo klabuni. Haikuwa hisani Msimbazi walikuwa wanataka kumbakiza klabuni hapo kwa gharama yoyote ile. Wangemwacha asingekosa timu.
Huyu ni staa wa klabu yake, pia ni staa wa timu ya taifa ya Zambia ambao ni Mabingwa wa Afrika wa mwaka 2012. Huyu ni staa ambaye ana heshima yake. Huyu ni staa ambaye anasimama katikati ya mafanikio ya klabu yake katika michuano ya Afrika ambayo klabu yake imekuwa ikifanya vyema.
Tuna mafunzo mawili hapa. Funzo la kwanza kabisa ni wachezaji wengi wa zamani kwa sasa ni masikini kwa sababu walidhani wanazichezea klabu hizi kama hisani. Hapana. Walikuwa wanazichezea kama kazi.
Wengi waligeuzwa kuwa kama mashabiki. Hilo lilikuwa jambo la kwanza. Lakini hapo hapo kwa wale waliokuwa wanajitambua bado walikuwa wanapewa vitisho kama vya Chama. Unakuta kiongozi anampiga mchezaji mkwara ambao hauna msingi wowote ule.
Kwa mfano, mchezaji akitaka kusajili kwenda upande mwingine au kwenda nje ya nchi halafu akalazimisha, anakutana na matajiri kama tajiri wa Chama na kisha anaanza kumpiga mikwara mingi ili asiondoke. Wanamkumbusha vitu vingi walivyoviona kama vile wamemtendea hisani zamani wakati ilikuwa haki yake.
Nyakati kama hizo unakuta mmoja kati ya matajiri anamkumbusha mchezaji huku akisema “Kwa nini unataka kwenda kwa hao jamaa? Unakumbuka mimi nilitoa hela yangu mfukoni kwa ajili ya wewe kusaini ule mkataba wetu wa mwanzo?”. Unaweza kudhani tajiri aliyesimama mbele yako alifanya hivyo kama hisani kumbe mchezaji alikuwa anahudumu kwa maarifa klabuni.
Kuna wachezaji wengi ambao wanaingia katika mtego huu. Huwa wanakumbushwa kutofuata malisho mema mahala pengine kwa kutajiwa baadhi ya vitu ambavyo waliwahi kufanyiwa zamani katika klabu husika.
Ukichunguza, ni mambo waliyofanyiwa, hata kama yalikuwa nje ya mkataba, yalitokana na mambo makubwa waliyoyafanya uwanjani. Hayakuwa hisani. Tatizo viongozi wetu ugeuza mambo haya kuwa hisani.
Nawalaumu pia baadhi ya wachezaji wetu kukubali mtego huu. Kuna wakati wachezaji pia huwa wanahitaji hisani kutoka kwa klabu hizi pindi wanapostaafu kwa kutaja mambo mengi mazuri waliyowahi kuzifanyia klabu zao kama vile walikuwa hawalipwi wakati wanacheza.
Neno hisani inabidi liondoke katika midomo ya pande zote mbili. Viongozi na mashabiki wajue wachezaji hawachezi kwa hisani. Wachezaji pia wajue mpira ni kazi yao. Hawapo kwa ajili ya hisani.
Kama ningekuwa Chama nadhani ningemkumbusha tajiri nilipokea kiasi nilichopokea kwa sababu ya kazi yangu nzuri. Ningemkumbusha pia tajiri kuvunja mkataba kama alidhani nilikuwa sistahili kupokea nilichopokea.
Tukiachana na hilo, lakini kitu cha pili cha msingi katika sakata hili ni kutengeneza itifaki nzuri ambayo inamweka mchezaji na tajiri kuwa mbali. Tajiri wa klabu hapaswi kuwa karibu na mchezaji hata katika suala la mitandao ya jamii.
Tajiri wa klabu ni mtu mkubwa anayepaswa kujificha na kukaa nyuma ya pazia huku akiitazama klabu yake kwa jicho la mwewe. Hapaswi kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na mchezaji kupitia katika mitandao ya kijamii.
Kama kuna kitu tajiri kimemkwaza, basi anapaswa kumtuma mmoja kati ya watendaji wake aandae kikao na mchezaji husika au njia nyingine ni kumpigia simu mchezaji moja kwa moja kueleza kusikitishwa kwake.
Roman Abramovich alikuwa na urafiki wa karibu na baadhi ya mastaa wa Chelsea kama vile Frank Lampard na Didier Drogba. Nadhani alikuwa anakutana nao katika boti zake za kifahari kwa ajili ya maongezi ya hapa na pale.
Hata alipokuwa akifurahishwa nao alikuwa hana muda wa kuwapongeza katika mitandao ya kijamii achilia mbali kuwaponda kama walikuwa wamemkwaza mahala. Hata hapa nchini tuna matajiri wa namna hiyo katika klabu nyingine.
Tuna matajiri wa klabu nyingine tunaowafahamu kwa upole wao. Hatujui hisia zao za moja kwa moja na muda mwingi wamekuwa wakikaa nyuma ya pazia katika matukio makubwa ya klabu zao achilia mbali matukio ya kawaida kama ya mitandao ya kijamii.
Post a Comment