Ifahamu miji 5 duniani yenye gharama ya chini zaidi ya kuishi




Gharama za kuishi ni muhimu unapochagua ama kutafuta mahali pa kuishi, itakusaidia kuishi raha mustarehe kwa sababu utaamua kuchagua mahali penye gharama nafuu ya vitu kama malazi, huduma za afya, gharama za usafari na vyakula.

Kuna baadhi ya miji, ama nchi gharama zake za kuishi ni kubwa mno kulingana na vipato vya watu wengi.

Kwa mfano majiji kama New York na San Francisco nchini Marekani gharama zake za kuishi ni za juu ukilinganisha na majiji mengi ya nchi hiyo, Afrika, Asia na baadhi ya majiji ya nchi za Ulaya.

Kwa upande mwingine yapo majiji ambayo gharama zake ni za kutupwa, ni rahisi na unaweza kuishi kwa mbwembwe kwa gharama nafuu na ukapata huduma zile zile ama zinazofanana na hizo kwa ubora tofauti ila kwa gharama ya kawaida.

Watu wengi hasa kutoka mataifa ya Ulaya na Marekani na wachache Asia, wanafunga safari kwenda kuishi ama kutembelea majiji ambayo gharama zake ni nafuu. Na hapa BBC inakuletea angalau majiji 5 ambayo maisha yake ni rahisi kutokana na gharama zake za maisha kuwa za chini kabisa duniani. Majiji ambayo pia unaweza kutumia pesa yako ya kustaafu vyema, ukifurahia utamaduni wake, historia, burudani na vitu vingine vya kuvutia.

5: La Paz, Bolivia


Bolivia ni moja ya nchi zenye gharama nafuu sana za kuishi katika eneo la Amerika ya Kusini, na kufanya kuwa sehemu nzuri ya kuishi na kutembelea.
Jiji la La Paz hasa lenye huduma zote muhimu na kubwa linavutia wengi kwa gharama zake nafuu.

Unaweza kupangisha nyumba ya ghorofa yenye kila kitu ndani katika jiji La Paz kwa kiasi kidogo cha kati ya dola 500 mpaka 600 kwa mwezi.

"Nilikutana na wanawake wawili waliostaafu, mmoja ana miliki nyumba kabisa na mwingine amepangisha nyumba ya vyumba viwili na kila kitu kwa dola $125 kwa mwezi. Wote bajeti zao kwa mwezi haizidi dola $500 mpaka $600," anaripoti Jason Holland, mhariri wa IL Roving Latin America.

Vyakula na vinywaji ni nafuu zaidi La Paz na unaweza kuvikuta vitu hivyo mtaani kirahisi tu na vya asili, na unaweza kutembelea kwenye maeneo ya vivutio kama ziwa Titicaca na majengo ya Uyuni Salt.

Ukiwa nchini Bolivia usafiri wa ndege kutoka popote pale ikiwemo La Paz gharama zake ni chini ya dola $50. Na wengi hutumia ndege kwa sababu ni nafuuu, lakini ukitaka kutumia basi ndiyo nafuu zaidi.

4: Sofia, Bulgaria



Bulgaria ni moja ya nchi zinazoonekana kama si kitu Ulaya kati ya nchi nzuri kwenda kuishi ama kuzitembelea, wengi wanazitazama nchi kama Uingereza, Ufaransa, Uholanzi na zingine wanasahau kwamba gharama nafuuu za maisha zinaifanya Bulgaria kuwa juu kati ya nchi nyingi Ulaya.
Jiji la Sofia, ndilo hasa lenye huduma zote muhimu, lakini utazipata kwa bei ya Afrika ama Amerika Kusini. Vitu ni rahisi na maisha ni rahisi.

Unaweza kuishi kwa chini ya dola 20 kwa siku na ukapata kila kitu, lakni si rahisi kwa fedha hiyo kuishi katia jiji la London na kuridhika. Usafiri wa ndege kutoka Sofia kwenda miji mingine ni rahisi.

Nchi hii aina vivutio sana kama nchi zingine, lakini ukitaka kuishi kwa gharama ndogo Ulaya basi nenda Sofia, Bulgaria. Watu wake ni wakarimu na wanapenda wageni tofauti na watu wa mataifa mengi barani humo. Na wamekuwa wakitembeza watu bure tu kuona mandhari ya jiji hilo, vyakula na vitu vingine vya kitamaduni.

3: Bangkok, Thailand


Thailand ni moja ya nchi maarufu duniani yenye vivutio vizuri vya utalii duniani. Ni nchi inayopokea wageni wengi tu wanaotembelea vivutio mbalimbali, na jiji la Bangkok ambalo hufurika watu wengi, ni moja ya majiji yenye gharama nafuu ama za chini za kuishi duniani.
Lina sehemu nyingi za michezo mfano Mauy, ambalo ni maarufu kwa kushuhudia ndondi.

Pamoja na vitu vingi vya kuvutia unaweza kupata sahani moja ya chakula kizuri chenye kila kitu kwa maana ya mlo kamili kwa gharama isiyozidi dola $1.

Thailand ni nchi ya ngumi, wanapenda sana mchezo wa ngumi, na filamu. Tiketi kuangalia pambano la ngumi hugharimu dola isiyozidi 10 wakati Marekani ama Uingereza pambano moja linaweza kugharimu kati ya dola $100 mpaka $200. Yale mapambano madogo ukibahatika sana utatozwa dola $50.

2: Qoito, Ecuador

Jiji la Qoito ni moja ya majiji yanye mvuto Amerika Kusini, lakini ni rahisi kuishi kwa sababu ya gharama zake kuwa za chini.
Mtaani utapata kila kitu wa bei rahisi, huduma zote zinapatikana kwa unafuu.

Ukiwa hapo ni rahisi kwenda maeneo ya vivutio kama Amazon, Msitu wa mawingu, maeneo ya milima na miinuko, fukwe lakini hata visiwa vya Galapagos, kwa gaharama nafuu ajabu.

Usafiri wa umma ukiwa Quito ni rahisi sana, ambapo unaweza kutozwa chini ya dola 1 kwa safari ndefu ya jiji hilo.

1: Hanoi, Vietnam

Jiji hili linatajwa na mitandao ya World packers na International living kama jiji lenye gharama za chini kabisa za kuishi duniani. Linapatikana kusini Mashariki mwa bara la Asia. Ni makao makuu ya Vietnam, lenye historia kubwa, majengo ya usanifu wa kuvutia, vyakula vya asili vingi mtaani, utamdauni na burudani mbalimbali.
Ukitaka kuweka akiba yako vizuri lakini ukiendelea kupata huduma zote muhimu basi Hanoi ndo mahala sahihi.

Kuna utamaduni wa baadhi ya watu kuishi bure na wanafunzi kama wa vyuo kwa kupata malazi na chakula bure, na wao wanafunzi kusaidia shughuli ndogo ndogo za nyumbani ama za ofisini za mwenye nyumba.

Gharama za nyumba za Hanoi ni nafuu mara dufu ya zile za Magharibi, licha ya nyumba zake kuwa na viwango vya hadhi ya juu.

"Najiona mwenye bahati kuishi Vietnam," alisema Wendy Justice, mwakilishi wa IL Southeast Asia. "Mimi na mume wangu tulitumia pamoja dola $1,200 kwa mwezi hapa Hanoi, ambayo ukilinganisha na majiji makubwa ni nafuu sana.

''Miji mingine kama Dalat au Nha Trang, bajeti yetu ya kuishi kwa mwezi ni chini ya $1,000. Kwa watalii, gharama hii ni ndogo zaidi kwa mwezi ukilinganisha na majiji mengine duniani" Alisema.

 


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post