WAKATI winga wa Simba, Luis Miquissone, akijiandaa kujiunga na mabingwa wa Afrika mara mbili mfululizo, Al Ahly ya Misri, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mzambia Clatous Chama, naye ameshusha kishindo kizito baada ya kueleza kuwa anasikilizia ofa nono kutua mezani.
Ubora aliouonesha Miquissone katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliomalizika kwa Al Ahly kuibuka mabingwa, hususan kwenye michezo miwili nyumbani na ugenini dhidi ya Wamisri hao, imeifanya miamba hiyo kutoa ofa nono ambayo inaelezwa imekuwa vigumu Simba kuikataa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya Misri, klabu hiyo imekubali kutoa dola za Marekani 900,000 zaidi ya Sh. bilioni mbili za Tanzania ofa ambayo imekubaliwa na Simba kumuuza Miquissone.
Hata hivyo, Simba bado haijatangaza rasmi uamuzi huo wa kumuuza Miquissone, lakini inaelezwa ni suala la muda tu kwa kuwa winga huyo tayari amewaaga marafiki zake wa karibu kuwa anajiunga na Al Ahly.
Lakini Chama akizungumzia taarifa za kuwapo uwezekano wa kuondoka kwa Miquissone, alisema hata yeye kama itakuja ofa nono mezani hatakaa na klabu yake hiyo kuiomba umuuze.
“Kama Miquissone akiondoka, mimi pia ikija ofa nzuri klabu ikakubali nitaondoka. Nimekaa Simba miaka mitatu, nimefanya mambo mazuri, mashabiki wajue kuwa haya ni mambo ya kawaida yanatokea. Nilishasema tangu awali kama muda ukifika na mimi nitaondoka endapo ofa itakuja na Simba ikikubali,” alisema Chama.
Chama ambaye amekuwa na mchango mkubwa kwa klabu hiyo tangu ajiunge nayo mwaka 2018, aliongeza: “Ukitazama miaka yangu mitatu hapa Tanzania, nadhani nimefanya vizuri kwa timu, ninauhakika mashabiki wanapaswa kuelewa, endapo kuna klabu kubwa itajitokeza tutakaa na kujadili tukikubaliana na Simba ikikubali nitaondoka.”
Kwa misimu yote mitatu ambayo ameichezea Simba, Chama ameiwezesha klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu, huku ikibeba Kombe la FA mara mbili mfululizo na kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili.
Tayari Simba ipo katika mipango ya kuboresha kikosi chake na imeshatangaza usajili wa wachezaji wawili, winga Mmalawi Peter Banda pamoja na mshambuliaji Yusuph Mhilu kutoka Kagera Sugar.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, alimwambia mwandishi wetu kuwa, bado wataendelea kutangaza usajili mpya kwa ajili ya kukiimarisha kikosi hicho kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ile ya ndani. “Kwa sasa kazi yetu ni moja tu, kutangaza usajili, mambo mengine tunayaweka kando kwanza,” alisema.
Post a Comment