Askofu Gwajima: Sijalishwa sumu



Dar es Salaam. Askofu wa kanisa la Ufufuo na Uzima Josephat Gwajima, amekanusha madai kuwa amelishwa sumu kutokana na msimamo wake kuhusu chanjo.

Askofu huyo ameeleza kuwa hajalishwa sumu, hakuna wa kumfanyia hivyo.

Akizungumza leo Jumapili Agosti 8, 2021 wakati wa ibada kanisani kwake kuwa, “Wanataka kusingizia watu, labda kusingizia kwamba serikali imeninywesha sumu. Niwahakikishie kwamba hakuna serikali imemnywesha sumu Gwajima kwa kuwa serikali ndiyo inasema chanjo ni hairi. Hakuna wa kuninywesha sumu na hatotokea.

Askofu huyo ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kawe alizungumzia pia suala la chanjo huku akisema suala la afya ya mtu linapaswa kulindwa na mtu mwenyewe.

“Labda nitoe changamoto kwa wanaojiita watalaam waje walete andiko linaloonyesha kemikali zilizopo kwenye  chanjo.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa kuratibu utafiti wa taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) Dk Paul Kazyoba ameeleza kuwa chanjo hiyo ni salama na imeanza kutolewa baada ya tafiti nyingi kufanyika na kujiridisha usalama wake.

“Tafiti zimefanyika na tumejiridhisha kuwa ni salama na ina ufanisi wa kumzuia mtu asipate corona na hata ikitokea amepata isiwe ugonjwa mkali wa kumsababishia kulazwa au hata kifo.

Baada ya kujiridhisha mamlaka za serikali zikaona ni muda muafaka kwa chanjo hiyo kuja nchini hivyo usalama wake umethibitishwa bila kuacha shaka yoyote kwamba haileti madhara yoyote kwa watanzania kama ambavyo imekuwa kwa watu wa mataifa mengi duniani.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Profesa Abel Makubi ilieleza kuwa tangu kuanza kutolewa kwa chanjo hiyo idadi ya watu wanaotaka kuchanjwa imekuwa ikiongezeka siku hadi siku.

Alisema rekodi ya Agosti 7 ilionyesha zaidi ya watu 164,500 walikuwa wamejisajili kwa ajili ya kupatiwa chanjo hiyo katika juma la pili tangu ianze kutolewa kwa watu wa makundi ya kipaumbele.



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post