UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umempeleka Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi kutokana na kauli yake ya kuwaita wachezaji wao wakuokotwa.
Manara aliyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Juni 30, mwaka huu, kwenye Ukumbi wa Serena Hotel, Dar wakati Simba ikijiandaa na mchezo wa ligi dhidi ya Yanga.
Manara kwenye mkutano huo alisema: “Yaani Simba ina Chama, Bwalya, Bocco ukachukue watu wameokotwaokotwa halafu useme wanaweza kutufunga, hiyo haiwezekani.”
Chanzo kutoka Yanga, kimeliambia Championi Jumamosi, kuwa: “Baada ya Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara kuongea vibaya kwenye mkutano na waandishi wa habari, na kuwakandia wachezaji wa Yanga kuwa ni wa kuokotwa, viongozi wamechukia na kuipeleke kesi hiyo TFF na Bodi ya Ligi kwa ajili ya kuitolea hukumu.
“Mwanzo walitaka kuipeleka mahakamani kabisa wakaona waanzie huku ila na TFF wenyewe wanataka wampige faini kimya kimya,” alisema mtoa taarifa huyo.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alipotafutwa alisema kuwa: “Sipo ofisini kwa sasa, hivyo sifahamu juu ya malalamiko hayo ila nitakapoenda ndio nitajua.”
Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfikirwa alisema: "Ni kweli tumepeleka malalamiko yetu TFF juu ya kauli ya Manara.”
Post a Comment