Idadi ya waliokufa kutokana na ghasia zinazoendelea nchini Afrika Kusini imepanda na kufikia watu 212 kutoka vifo 117 vilivyoripotiwa siku iliyopita.
Waziri wa nchi katika ofisi ya rais, Khumbudzo Ntshavheni, ameuambia waandishi habari kuwa vifo vipya vimetokea katika jimbo la kusini mashariki la KwaZulu-Natal ambalo ndiyo kitovu cha machafuko yanayoshuhudiwa.
Hata hivyo kiongozi huyo amesema hali ya utulivu imeanza kurejea na hadi sasa zaidi ya watu 2,500 wamekamatwa kutokana na vurugu za karibu wiki nzima zilizohusisha uporaji wa mali na uchomaji wa moto majengo ya biashara.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema vurugu hizo ambazo zimelitikisa taifa hilo "zilipangwa" na ameapa kuwasaka wote walihusika.
"Ni wazi kwamba matukio yote haya ya vurgu na uporaji yalichochewa -- kulikuwa na watu waliopanga na kuyaratibu," amesema Ramphosa wakati alipolitembelea jimbo la KwaZulu-Natal, kitovu cha machafuko hayo mabaya zaidi kuikumba Afrika Kusini tangu kukomeshwa kwa enzi ya ubaguzi wa rangi.
Ramaphosa amesema uporaji na uchomaji moto uliotokea umeathiri pakubwa imani ya wawekezaji na kuathiri ukuaji uchumi wa Afrika Kusini. Amesema serikali yake inafanya kila liwezekanalo kutuliza hali hiyo.
"Tumewabaini kwa sehemu kubwa waliohusika na hatutaruhusu machafuko na ghasia kuzuka tu nchini mwetu" Ramaphosa amekaririwa na vyombo vya habari.
Wanajeshi waendelea na juhudi za kudhibiti vurugu
Vurugu hizo zilizuka siku moja baada ya rais wa zamani Jacob Zuma kuanza kutumikia kifungo cha miezi 15 gerezani alichohukumiwa kwa kosa la kupuuza wito wa mahakama.
Zuma, ambayo anatokea jimbo la KwaZulu-Natal ana uungwaji mkono mkubwa miongoni wa wanachama watiifu ndani ya chama tawala ANC wanaomtaja kama mtetezi wa watu masikini.
Katika matukio yaliyowashanga wengi nchini humo, waporaji wameyavamia maduka, majengo ya biashara na hata benki na kuondoka na mali huku maafisa wa polisi wakishindwa kufanya chochote.
Zaidi ya wanajeshi 25,000 wametawanywa kudhbiti ghasia hizo Rudzani Maphwanya alifanya ziara jini Alexandra kutizama wanajeshi wanavyotimiza wajibu wao wa ulinzi akisema hawataruhusu magenge ya vibaka na wahalifu kuendeleza hujuma bila kukabiliwa na mkono wa sheria.
Vurugu hizo zimesababisha hofu ya kutokea upungufu mkubwa wa bidhaa muhimu ikiwemo nishati ya mafuta, chakula na dawa kutokana na kuparaganyika kwa mfumo wa usambazaji mahitaji.
Kadhalika zimetishia kuongeza idadi ya maambukizi ya virusi vya corona katika taifa hilo amablo tayari linashuhudia idadi kubwa ya vifo katika wimbi la tatu la Covid-19.
Nafasi za Ajira Serikalini Bonyeza HAPANafasi za Scholarships Bonyeza HAPANafasi za Internships Bonyeza HAPA
Post a Comment