Watoto wawili wafa kwa moto nyumbani




Watoto wawili wa familia moja, Kijiji cha Njoro, wilayani Kiteto mkoani Manyara wameungua moto nyumbani kwao wakiwa wamelala baada ya kaka yao kuwafungia ndani akaenda kutazama video.
Watoto hao ni Bakari Mursali (8) na Abdi Mursali (6), ambao wakati tukio linatokea wazazi wao hawakupo nyumbani na aliyekabidhiwa jukumu la kuwalea ni kaka yao mwenye umri wa miaka 16, ambaye jina lake halikufahamika.

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mbaraka Alhaji Batenga amethibitisha kutokea ajali hiyo na kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kutaka kujua chanzo cha moto huo.

“Kamati yangu ya ulinzi na usalama tulifika Kijiji cha Njoro saa tano usiku na tukarudi saa 9 usiku tukijaribu kufuatilia sakata hili ambalo hata hivyo uchunguzi unaendelea,” alisema

Alisema watoto hao waliachwa na wazazi peke yao, wakiwa katika utafutaji wa maisha ambapo mama yao alikuwa shambani na baba alikuwa Simanjiro.

Mkuu huyo wa wilaya alitoa elimu ya kukabiliana na majanga ya moto akiwashauri wazazi kuwa makini kutowaacha watoto wakiwa hawana ulinzi, jambo ambalo alisema linaleta madhara kama hayo.

Diwani wa Kata ya Njoro, Ramadhani Mpolonge alisema wananchi wanashangazwa na tukio hilo kutokana na kwamba nyumba hiyo haipikwi chakula na hakuna chanzo cha moto, huku watoto hao siku hiyo walikula kwa jirani.

“Taarifa za uhakika hawa watoto usiku ule walikula kwa jirani, wakarudi nyumbani kwao na kuingia ndani, ndipo kaka yao akafunga kwa nje na kwenda kuangalia video kwa jirani na aliporudi akakuta moto unawaka ndani,” alisema.



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post