Kufuatia matukio matatu ya moto katika Shule ya Sekondari Geita ndani ya siku saba na kusababisha wanafunzi watatu kujeruhiwa, maabara na darasa kuteketea kwa moto, mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule ameiagiza bodi ya shule hiyo kuwafukuza wanafunzi 11 waliobainika kuwa na makosa ya jinai.
Akizungumza leo Jumatano Julai 14, 2021 katika shule hiyo, Senyakule amesema uchunguzi uliofanywa na kamati iliyoundwa kuchunguza matukio ya moto imebaini mambo mbalimbali ikiwemo utovu wa nidhamu wa hali ya juu wa wanafunzi na matukio ya kijinai.
Amesema mbali na hao 11 wapo wengine 24 ambao bodi ya shule imetakiwa kuwapa adhabu ya kurudi nyumbani siku 30.
“Hawa wanafunzi 11 wamekutwa na makosa ya jinai walikuwa na visu, wana makosa ya kubaka na makosa mengine mengi ya kijinai wapo ambao walishajadiliwa na bodi na shule hawa washtakiwe kwa makosa ya jinai sio tu kufukuzwa shule, “ amesema Senyamule.
Amemtaka katibu tawala wa mkoa kumchukulia hatua za kinidhamu mkuu wa shule hiyo pamoja na walimu 13 walioshindwa kuwajibika kwa mambo muhimu na kutaka kuwabadilisha kituo cha kazi ndani ya siku saba.
Pia amezitaka kamati za usalama kwa kushirikiana na shule kuweka alama kwenye mabweni yote ya shule ili moto unapotokea usilete madhara na kutaka ulinzi shirikishi uimarishwe ili kuzuia matukio yasiyo ya lazima.
Katika hatua nyingine walinzi wa shule hiyo wamefukuzwa kazi kutokana na uchunguzi kubaini hawana mafunzo ya usalama na hawakupitia Jeshi la Akiba la Mgambo.
Post a Comment