Zaidi ya watu 50 wamekufa baada ya moto kuzuka katika wodi ya wagonjwa wa Corona katika hospitali nchini Iraq. Moto katika hospitali ya Al-Hussein kusini mwa mji wa Nasiriya ulidhibitiwa mwishoni mwa Jumatatu. Sababu ya moto haijulikani wazi, lakini ripoti za mwanzo zinaonyesha kuwa ulianza baada ya tenki ya oksijeni kulipuka.
Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al-Kadhemi aliamuru kukamatwa kwa mkuu wa hospitali. Jamaa za wagonjwa wamekuwa wakiandamana nje ya jengo hilo. Shirika la habari la Reuters liliripoti mapambano kati ya jamaa za waliofariki na polisi huku magari mawili ya polisi yakiteketezwa.
Wodi hiyo mpya ilikuwa na nafasi ya vitanda 70 na ilijengwa miezi mitatu tu iliyopita, maafisa wa matibabu waliliambia shirika la habari la Associated Press. Afisa wa afya wa mkoa alisema kuwa watu wasiopungua 63 walikuwa ndani wakati moto ulipoanza.
“Nilisikia mlipuko mkubwa ndani ya wodi za corona na kisha moto ulikuwa umelipuka haraka sana,” mlinzi wa hospitali aliliambia shirika la habari la Reuters. Operesheni ya utaftaji inaendelea.
Spika wa bunge la Iraq Mohamed al-Halbousi alituma ujumbe katika twitter akisema kwamba moto huo ni “dhibitisho dhahiri la kushindwa kulinda maisha ya waIraqi, na ni wakati wa kukomesha janga hili”.
Mnamo Aprili, tanki la oksijeni likilipuka na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 82 katika hospitali katika mji mkuu wa Baghdad. Waziri wa afya Hassan al-Tamimi alijiuzulu baada ya moto huo.
Janga la corona limeathiri sana huduma za afya nchini Iraq, zinazokabiliwa na miaka mingi ya vita, kupuuzwa na ufisadi. Iraq imesajili maambukizi milioni 1.4 na kuripoti zaidi ya vifo 17,000 kutokana na Corona , kulingana na data za Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.
Nchi hiyo imetoa angalau dozi moja ya chanjo dhidi ya Covid kwa zaidi ya watu milioni moja kati ya wake milioni 40, Shirika la Afya Ulimwenguni linasema.
Post a Comment