Ubalozi Wa Tanzania Nchini Afrika Kusini Waelezea Hali Za Watanzania Waliopo Nchini Humo Baada Ya Kuwepo Kwa Maandamano Na Vurugu




 Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ubalozi wake wa Afrika Kusini inapenda kuwaondoa hofu Watanzania kuwa mpaka sasa hakuna Mtanzania yeyote aliyedhurika ama kukamatwa kwa kujihusisha na vurugu na maandamano yanayoendelea katika baadhi ya miji Nchini humo kushinikiza kuachiwa kwa Rais Mstaafu wa Afrika ya Kusini Mhe. Jacob Zuma.

Serikali kupitia Ubalozi wake uliopo Nchini humo unaendelea kufuatilia na kuwasiliana kwa karibu na Viongozi wa Jumuiya mbalimbali za Watanzania waishio Afrika Kusini, Mamlaka na vyombo vya Ulinzi na Usalama ili kufahamu endapo kuna Mtanzania yeyote aliyehusishwa ama kudhurika na tukio hilo.

“Kama Serikali ya Afrika Kusini inavyoelekeza, Ubalozi wa Tanzania Afrika Kusini unawasihi Watanzania waliopo hapa kuendelea kuwa watulivu na kutojihusisha na vurugu,pamoja na maandamano yanayoendelea Nchini hapa,” Amesema Balozi Meja Jenerali (Mst) Gaudence  Milanzi.

Balozi Milanzi ameongeza kuwa, kwa sasa Serikali ya Afrika Kusini imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha vurugu hizo zinadhibitiwa kwenye maeneo hayo ili zisisambae katika maeneo mengine na kwamba Jeshi la Ulinzi la Afrika Kusini limeelekezwa kuungana na Jeshi la Polisi katika kudhibiti vurugu hizo.

Maandamano na vurugu hizo zilianza juma lililopita kupinga adhabu iliyotolewa na mahakama ya juu Nchini humo kwa Rais Mstaafu wa Taifa hilo Mhe. Jacob Zuma ya kutumikia kifungo cha miezi 15 Gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kuidharau Mahakama (Contempt of Court). Hadi sasa taarifa zinaonesha kuwa Miji mingi Nchini Afrika Kusini iko shwari na haijaathiriwa na vurugu na maandamano hayo.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post