Dar es Salaam. Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka amesema chama hicho kitajikita kutekeleza malengo yake ya kuimarisha uchumi, badala ya kubishana na wasaka vyeo na madaraka.
Shaka ameyasema hayo jana Jumapili Julai 4, 2021 katika ofisi kuu ya CCM mjini Unguja akiwa katika msafara wa katibu mkuu wa CCM, Daniel Chongolo aliyeiongoza sekretarieti katika ziara ya kujitambulisha visiwani Zanzibar.
"Niwasihi wanasiasa nchini wajikite katika siasa za maendeleo kwa kutoa fikra na mawazo mbadala yanayoweza kuchangia kuboresha ustawi wa wananchi na kuharakisha maendeleo ya nchi yetu."
"Waachane na siasa za kitoto za kutoa mikwara ya maigizo kwa Rais Samia (Suluhu Hassan). Wanaompinga wafanye ukosoaji unaojenga na sio unaobomoa na kutishia kutugawa au kuvunja amani ya nchi," amesema Shaka.
Shaka amebainisha kuwa katika kipindi kifupi cha utendaji wa Rais Samia na Dk Hussein Mwinyi, wameakisi mambo yaliyokuwa yakitamaniwa na jamii yatokee na kufuatwa.
Amesema sauti za viongozi hao zimetoa mwanga, kuwapa matumaini mapya waliokata tamaa na tabasamu kutokana na uongozi bora wanaouonesha unaoheshimu taaluma, kusimamia weledi, utawala wa sheria na kutoa uamuzi wa haki.
Post a Comment