Shahidi Kesi ya Sabaya Aangua Kilio Mahakamani “Alitaka Kunipiga Bastola”





Shahidi wa sita wa Jamhuri katika kesi ya unyan’ganyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, Bakari Msangi ameangua kilio mahakamani wakati akielezea mahakama alipokuwa akitishiwa bastola na Sabaya huku akiwa amefungwa pingu miguuni na mikononi.

 

Msangi ambaye ni Diwani wa Sombetini kwa tiketi ya CCM, aliangua kilio hicho katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha akiendelea na ushahidi wake huku akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka.

 

Katika kesi hiyo ya jinai namba 105, 2021 inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo, Sabaya na wenzake wawili Sylvester Nyegu na Daniel Mbura wanakabiliwa na mashitaka matatu ya unyan’ganyi wa kutumia silaha.

 

Msangi ambaye alianza kutoa ushahidi wake jana alianza kulia mahakamani hapo wakati akiieleza mahakama namna alivyotekwa na kiongozi huyo na kundi lake ambapo alidai kufungwa pingu miguuni na mikononi akiwa ndani ya gari la Sabaya.

 

Ameeleza akiwa ndani ya gari hilo wakitoka katika duka la Mohamed Saad, Sabaya alitoa bastola yake na kumtishia nayo huku akimwambia anapenda kumwingilia katika mambo yake.

 

Shahidi huyo aliendelea kuieleza mahakama kuwa Sabaya aliendelea kumtukana na kumwambia dereva kuwa yeye (Sabaya) anayeweza kuongea nae katika nchi hii ni Rais Dk John Magufuli na siyo takataka nyingine huku akijipiga piga kifuani.

 

Aliieleza mahakama kuwa Sabaya alimtaka akamuonyeshe nyumba za Saad na ndugu yake na alipofika kwa Mohamed eneo la Dar Express, Sabaya aliwaeleza walinzi aliowakuta katika eneo hilo kuwa yeye ni DC wa Hai na ameelekezwa na Rais kufanya kazi fulani hivyo walinzi hao wakamuonyeshe anapoishi mtu huyo.

 

Shahidi huyo alidai mahakamani hapo kuwa baada ya dereva wa Sabaya na mmoja wa mabaunsa wake kumpa simu yake alimpigia mke wake na kumweleza kuwa ametekwa na Sabaya katika eneo la Tulia Lodge hivyo atafute jirani mmoja amsindikize katika eneo hilo.

 

Aliendelea kuieleza mahakama hiyo kumpigia simu mke wake aliambiwa afiche simu zake maungoni kwake na mke wake alipofika eneo hilo alipiga magoti mbele ya gari la Sabaya na kumuomba kiongozi huyo amwachie mume wake.

 

Alidai Sabaya alitoa bastola yake na kumwita mkewe na kumwelekezea bastola kichwani na kisha mdomoni huku akimwambia atamuua ambapo mmoja wa mabaunsa wa Sabaya walimwambia Msangi asiongee kitu kwani Sabaya alikuwa amelewa na risasi ilikuwa kwenye chamber hivyo anaweza kumuua mkewe.

 

Shahidi huyo alidai kuwa kabla ya kuelekea katika Lodge ya Tulia wakiwa ndani ya gari la Sabaya aliona simu ikiita(Whatsapp) iliyoandikwa DC Arusha Kenan ambapo ilipopokelewa alisikia Sabaya akisema location Mt. Meru.

 

Shahidi huyo alidai wakiwa katika eneo la hospitali ya Mt.Meru Sabaya alichukua fedha walizokuwa wametoka nazo dukani kwa Saad na kuweka bundle la kama Sh milioni moja kwenye soksi mguu wa kushoto na nyingine mguu wa kulia kisha akashuka kwenye gari.

 

Alidai baada ya kurejea kwenye gari alimsikia mshitakiwa huyo wa kwanza akisema aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenani Kihongosi ni maskini huku akisema angalia gari analoendesha (Altezza).

 

Alidai Sabaya alipokea simu nyingine na baada ya kuikata aliwaambia walinzi wake kuwa huyo aliyekuwa anazungumza naye ni OC CID wa Hai aliyemweleza kuwa watu aliokuwa amewakata mchana wametoa hela hivyo aifuate na ndipo walielekea Tulia Lodge, Sakina.




0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post