MZEE MPILI "Hapa Dar Nimemaliza, Simba Mtanikuta Kigoma Natangulia"



SIMBA wanalia wakiwaambia wababe wao Yanga kwamba mumshukuru Mzee wenu Mpili vinginevyo mngekula nyingi lakini mwenyewe amejibu mapigo akiwaambia ‘Hapo mmepigwa na nyuklia moja tu mmesambaratika sasa subirini Kigoma mi natangulia’.

Yanga ilicheza kwa mbinu bora zaidi dhidi ya Simba juzi na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 la mapema dakika ya 11 tu kutoka kwa kiungo Zawadi Mauya na kuwacheleweshea Wekundu hao sherehe za ubingwa wa nne mfululizo.

Akizungumza jana na Mwanaspoti, Mzee Mpili ambaye ni shabiki wa Yanga kutoka Ikwiriri, Pwani alisema watani wao wana bahati kwani walikuwa wapigwe nyingi katika mchezo wa juzi.

Mzee Mpili ambaye alionekana kuwa mwenye furaha akiwa amevaa fulana yake safi akaenda mbali akisema safari ya kuipiga Simba ndio imeanza na sasa anatangulia mkoani Kigoma kuanza maandalizi ya mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) utakaochezwa Julai 25 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.

“Simba wana bahati sana jana (juzi) walikuwa wapigwe nyingi ila tukasema lile linatosha hawana timu ya kutufunga, sisi Yanga kama tuko sawa na tumeshikamana kama ambavyo hali ilivyo sasa ndani ya Yanga.

“Hii ni mwanzo tu mimi hapa nimemaliza sasa natangulia Kigoma watanikuta huko wakutane na kipigo kingine wakimaliza mechi zao watanikuta kule nawasubiri.


“Tuna mechi nao kama tatu hivi tumemalizana nao jana na sasa itafuata ile ya Kombe la Shirikisho (ASFC)kule Kigoma na baada ya hapo tutakutana nao tena katika mchezo wa Ngao ya Jamii, hizi zote nasema hivii Simba atapotea, sitaki kusema sana,” alitamba Mzee Mpili.

Kuhusu mabomu yake ya nyuklia alisema katika mchezo huo walitumia bomu moja tu ambalo ni mwanajeshi wake kiungo Zawadi Mauya na kwamba mechi zijazo ataongeza dozi.

“Nikisema nina watu basi mjue ni wachezaji wangu, mchezo huu nimetumia tu silaha moja ya Mauya (Zawadi) lakini huko mbele tutatumia silaha zaidi, tumepiga bomu moja tu Simba wote wamesambaratika na sasa tunaangalia mchezo ujao.”

Mwanachama huyo aliwapongeza wanachama wenzake na uongozi wa klabu hiyo akisema sasa wamekuwa kitu kimoja baada ya kugundua wapi wanakosea.

“Tulikuwa na shida kidogo katika uongozi wetu wa Msola (Mshindo) lakini sasa amejua wapi anakosea hakutaka kuitisha mikutano yetu tuzungumze, nawashukuru wanachama wenzangu Mzee (Jakaya) Kikwete, wadhamini wetu GSM na kijana wangu Manji (Yusuf) nilifurahi kumuona mkutanoni hivi karubuni sasa Yanga imekuwa ni moja.”

MASTAA WAOGA NOTI

Baada ya kumuua Mnyama mbele ya Rais Samia Suluhu, wachezaji wa Yanga kuna kufuru moja wamefanyiwa na matajiri wao wakianza na Bilionea wa GSM, Ghalib Mohamed. Habari iwafikie kwamba jamaa amefurahi na sasa ametoa Sh 500 Milioni kwa wachezaji wa timu hiyo kwa ushindi huo.

Ahadi hiyo ndio iliyowapa mzuka wachezaji katika mchezo huo wakionekana kuusaka ushindi mapema, weka mbali ile hasira ya wachezaji walipotaka kumjibu Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara aliyewaita nyota wa Yanga kuwa ni “wachezaji wa kuokotezwa”.

Taarifa kutoka kwa wachezaji wa timu hiyo ni kwamba hawakutaka kupishana na fedha hizo na kwamba walitambua viongozi wao wanataka ushindi nao wakafanya kweli.

Hesabu za harakaharaka ni kwamba kuna uhakika kila mchezaji haitapungua kiasi cha Sh 20 milioni katika ahadi hiyo ya vigogo wa klabu yao. Ahadi hiyo inaweza kuwashtua wengi kutokana kuwa ndio ahadi kubwa kwani hakuna klabu imewahi kutoa ahadi kubwa katika mchezo wa Ligi Kuu Bara zaidi ya hiyo.

Akizungumzia baada ya mchezo huo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Injinia Hersi Said ambaye pia ni msaidizi wa Ghalib alisema awali waliwahi kuwapa ahadi wachezaji wao ya Sh 300 milioni lakini kwa mchezo wa huo ni zaidi ya hapo.

“Wachezaji wetu wanajua tulichowaahidi na huwa hatutangazi na wanajua huwa tunakamilisha tunachoahidi, tuliwahi kuwapa ahadi ya Sh 300 milioni lakini safari hii watapata zaidi,” alisema Hersi ingawa Mwanaspoti lina uhakika ni Sh 500 milioni.



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post