MWANAMUZIKI Bora wa Kike wa Tanzania, Faustina Charles Mfinanga au Nandy, ameingia matatani baada ya kufunguliwa kesi ya madai katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa madai ya kuingilia hakimiliki ya mwanamuziki Desire Manirapta almaarufu Daddy Face wa Marekani.
Daddy Face anadai Nandy amlipe kiasi cha shilingi milioni 260 pamoja na gharama za kesi na hasara alizopata baada ya kusababisha wimbo wake wa Naona Utamu kuondolewa kwenye Mtandao wa YouTube.
Msemaji wa Kampuni ya Uwakili ya Mbuya ya Dar es Salaam ambayo inamuwakilisha Daddy Face, Edrin Edwin ameliambia Gazeti la IJUMAA kwamba, kesi hiyo imewasilishwa katika mahakama hiyo kwa kutajwa.
Akifafanua zaidi, Wakili Edwin anasema kuwa, Nandy alishirikishwa na msanii huyo mwenye makazi yake jijini New York, Marekani katika wimbo wake huo wa Naona Utamu ambao aliingia mkataba na kulipwa chake hivyo hakuwa na chake tena kwenye wimbo huo
“Nandy alishirikishwa kwenye wimbo huo baada ya kuingia mkataba na kulipwa chake kiasi cha Dola za Marekani 2,000 (zaidi ya shilingi milioni 45 za Kitanzania) kwa ajili ya kushirikishwa tu huku haki zote zikiwa kwa Daddy Face,” anasema msemaji huyo.
Baada ya kuurekodi wimbo huo, ukaanza kurushwa kwenye YouTube hadi Aprili 16, mwaka huu ulipoondolewa baada ya Nandy kulalamika kuwa, wimbo huo ni wake.
“Nandy aliwaandikia YouTube kuwaambia kuwa huo wimbo ni wake nao wakaamua kuushusha na kumfanya msanii huyo wa Marekani asipate pesa tena kutokana na wimbo huo,” anasema Wakili Edwin.
Anaongeza kuwa, kutokana na kitendo hicho, mteja wake huyo amepata hasara kubwa kwani wimbo wake huo hauingizi tena pesa na wameamua kudai haki kwa kufungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania kudai fidia ya shilingi milioni 260 kutoka kwa Nandy.
Anasema kuwa, Nandy amekuwa akigoma kufika mahakamani, lakini sasa kesi hiyo itaendelea kutajwa hata kama hatakuwepo mahakamani.Nandy ameshiriki kwenye wimbo huo mpya wa Naona Utamu wa mwimbaji Daddy Face mwenye makazi yake nchini Marekani uliotoka rasmi Aprili 10, 2021 chini ya utayarishaji wa Producer Kimambo.
Daddy Face, baada ya kuachia Wimbo wa Marry You, Oktoba, mwaka jana ndipo akamshirikisha Nandy wimbo huo ukiwa ni wimbo wake wa kwanza kuuachia kwa mwaka 2021.
Nandy pia alifanya kazi na mwanamuziki maarufu Afrika, Koffi Olomide kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo wimbo huo unaendelea kufanya vizuri
Katika majibu yake kwa Gazeti la IJUMAA, Nandy anasema kuwa, hajui chochote juu ya ishu hiyo na wala menejimenti yake haijamlisha.
“Ndiyo kwanza nasikia kutoka kwako, menejimenti yangu haijanijulisha,” anasema Nandy ambaye anaendelea na matamasha yake ya Nandy Festival.
STORI: ELVAN STAMBULI, DAR
Post a Comment