Dar es Salaam. Mwanamuziki wa siku nyingi, Waziri Ally amefariki dunia jana usiku huku familia ikitaja chanzo cha kifo chake kuwa ni malaria na alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo kwa muda mrefu.
Waziri licha ya kufanya kazi katika bendi mbalimbali ikiwemo Msondo Ngoma, alipata umaarufu zaidi akiwa na bendi yake ya Kilimanjaro maarufu kwa jina la Wana Njenje, ambayo ndio alikuwa anaitumikia mpaka umauti ulipomkuta.
Akizungumza leo Jumamosi, Julai 24,2021 msemaji wa familia, Aboubakary Liongo amesema Waziri alianza kujisikia vibaya siku ya Alhamisi baada ya kurejea Dar es Salaam akiwa ametoka safarini Tanga kwenye shughuli zake za muziki.
"Aliporudi safarini alikuwa anajisikia vibaya mzee wetu, hivyo akaenda hospitali ya Marie Stoppers maeneo ya Mwenge kwenda kujiangalia na akakutwa na malaria wakamtundukia drip na kumpa mapumziko saa kadhaa kabla ya kumruhusu kurudi nyumbani.
"Jana tena saa tatu usiku hali ikabadilika ikabidi ndugu wampeleke hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu zaidi, lakini wakati akiwa njiani ndio akafariki," amesema Liongo.
Pia msemaji huyo amesema kwa muda mrefu Waziri alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo lakini akawa akipata matibabu na kuendelea na shughuli zake.
Kuhusu ratiba za msiba, amwsema wataaga hospitali ya Mwananyama leo saa tano na kisha mwili kusafirifishwa kwenda Tanga na anatarajiwa kuzikwa kesho kijijini kwao Pongwe.
Post a Comment