Msemaji Mkuu wa Serikali Msigwa Aeleza Manufaa ya Tozo iliyolalamikiwa




Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msingwa amesema tozo ya miamala ya simu ambayo Rais Samia Suluhu ameagiza ifanyie mapitio baada ya kelele za wananchi, ililenga kuboresha huduma za kijamii hususani maeneo ya vijijini.
Msingwa amesema hayo leo Julai 20, 2021, wakati akifanya mahojiano na kipindi cha 360 kinachorushwa na Clouds TV, amesema zilianzishwa ikiwa ni juhudi za Serikali kupanua wigo wa kodi ili kupata fedha za kuhudumia wananchi.

"Ile tozo ambayo Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba anaiita 'Tozo za Mshikamano' dhamira yake ilikuwa ni kwamba tuna tatizo kubwa la barabara vijijini. Hili jambo ukikaa huku Dar es Salaam unaweza kuliona kama dogo lakini vijijini huko hakuna barabara,” amesema.

Ameendelea kusema Serikali ilikusudia kwenye tozo ya miamala na ile ya laini za simu kukusanya karibu Sh1.6 trilioni na zaidi ya Sh1.2 trilioni zilikuwa zinatakiwa zitoke kwenye miamala. Hizi tozo zilitakiwa ziende zikajenge barabara na vituo vya afya huko vijijini na maji.

Hata hivyo, Msingwa alisema moja ya sifa ya Serikali hii ni usikivu na suala la tozo ni la kisheria na Serikali kazi yake ni kutekeleza sheria lakini sasa kuna maoni ya wananchi ambayo ni mazuri na Rais amesikia ndiyo maana ametoa maelekezo kwa mawaziri husika kufanyia kazi malalamiko ya wananchi na kuyapatia majibu.



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post