BERNARD Morrison maarufu mzee wa kukera, jana hakuwakera Yanga, alikuwa muungwana sana na kufanya kitendo kama cha kujirudisha ndani ya Yanga muda mchache kabla ya mchezo kuanza.
Kiungo mshambuliaji huyo ambaye jana alianza kikosi cha kwanza, muda mfupi kabla ya mchezo kuanza, alienda kwenye Benchi la Ufundi la Yanga, kisha akakumbatiana na rafiki yake kipenzi, Said Juma Makapu.
Morrison ambaye aliitumikia Yanga kwa muda wa miezi sita kabla ya msimu huu kutimkia Simba, wakati akiwa Yanga kuanzia Januari 2020 hadi Juni 2020, rafiki yake mkubwa alikuwa Makapu anayecheza nafasi ya kiungo na beki.
Mghana huyo, jana alitumia nafasi hiyo kwenda kwa rafiki yake kumsalimia na kuonesha bado anamkumbuka na urafiki wao haujafa licha ya sasa kuwa timu tofauti.
Mbali na hivyo, Morrison jana alikuwa akisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki hasa wa Simba waliotaka kushuhudia mavituzi yake.
Wakati vikosi vikitambulishwa kabla ya mchezo kuanza, lilipotajwa jina la Morrison, shangwe kubwa la mashabiki lilisikika tofauti na wengine walivyotajwa.
Post a Comment