UONGOZI unaomsimamia kipa Tape Eliezer Ira, umewaambia Klabu ya Yanga kuwa unahitaji dola 70,000 (sawa na Sh 161,584,000) ili kumuachia mchezaji huyo ambaye anahitajika na timu hiyo kwa ajili ya kuongeza nguvu kuelekea msimu ujao.
Yanga kwa sasa ina makipa watatu ambao ni Faroukh Shikalo, Metacha Mnata na Ramadhani Kabwili, lakini kuna kila dalili za viongozi wa timu hiyo kumuacha kipa mmoja na kumuongeza mwingine. Kipa huyo raia wa Ivory Coast mwenye umri wa miaka 23, anaitumikia FC San-Pédro inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo.
Akizungumza na Spoti Xtra, meneja wa mchezaji huyo, Faustino Mukandila, aliweka wazi kuwa thamani ya kipa huyo ni dola 70,000, huku akibainisha kwamba, ni kweli Yanga imeonesha nia ya kutaka kumsajili kipa huyo ambapo kwa sasa wapo katika mazungumzo ambayo hayajakamilika.
“Thamani ya Eliezer ni dola 70,000, bila kiasi hicho ni ngumu timu yoyote kumpata kipa huyu. Kuhusu Yanga ni kweli wameonesha nia ya kumuhitaji na tupo katika mazungumzo nao ambayo bado hayajakamilika, hivyo tunasubiri kuona nini kitakokea.
“Kama utaona dili kati yetu na Yanga limekamilika, basi unatakiwa kufahamu kuwa watakuwa wamelipa fedha hizo. “Ukiachana na Yanga, kuna timu nyingi zinamuhitaji kipa huyu, lakini Yanga wameonekana kuwa wapo siriaz zaidi,” alisema meneja huyo
MARCO MZUMBE, Dar es Salaam
Post a Comment