Matokeo Ya Uchunguzi Wa Vifo Vya Samaki Eneo La Ufukwe Wa Aghakhan, Dar Es Salaam

 


Tarehe 21 Julai, 2021 kulikuwa na tukio la vifo vya samaki ambao walionekana wakiwa wamezagaa katika ufukwe uliopo kati ya Hospitali ya Aghakhan na Ocean Road, Dar es Salaam.

Pamoja na hatua zilizochukuliwa za kuzuia wananchi kuchukua samaki hao kama kitoweo na kuzuia uingizaji wa samaki hao katika Soko la Magogoni Feri,  sampuli za samaki hao zilichukuliwa kwa ajili ya chunguzi za kimaabara na kilogramu 156 zilizobaki kuteketezwa na Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Ili kubaini chanzo cha vifo vya samaki hao, uchunguzi ulifanyika katika maeneo makuu matatu:

i) Utambuzi wa aina za samaki waliokufa, ukubwa wao, aina ya vyakula ndani ya matumbo na muonekano wa hali ya  nje ya samaki vilifanyika kwenye maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI).

ii) Uchunguzi wa maji kuangalia vimelea vyenye sumu ulifanywa kwenye maabara ya Taifa ya Uvuvi, Dar es Salaam.

iii)  Uchunguzi wa viuatilifu, sumu zitokanazo na mimea na kemikali nyingine za viwandani ilifanywa katika Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

MATOKEO

i) Aina tisa za samaki zilitambuliwa ambazo ni kui, mkizi, janja, tambanji, chaa, kuku bahari, kolekole pandu, kaa, kambamiti na kambakochi. Aidha, samaki jamii ya kui ilichukua sehemu kubwa ya samaki hao kwa asilimia 36 ikifuatiwa na jamii ya mkizi iliyokuwa na asilimia 29. Kwa ujumla, samaki hawa hupatikana kwenye kina kifupi cha maji. Pia, wengi wa samaki hao walikuwa wachanga. Sehemu kubwa ya matumbo ya samaki hayakuwa na chakula, ingawaje aina tatu za samaki (kui, mkizi na tambanji) walikutwa na dagaa, kaa na uduvi katika matumbo yao. Samaki waliochunguzwa walikuwa na hali nzuri, ngozi ilikuwa haikutatuka na ikiwa na rangi angavu, macho yao yalionekana meusi na angavu, na mapezi yalikuwa angavu bila utelezi, walikuwa na nyama imara na hakukuwa na harufu mbaya. Hali hii inaondoa uwezekano kuwa vifo hivi vinaweza kuwa vimetokana na sumu au vilipuzi. Hata hivyo, samaki wengi walionekana kuwa na midomo wazi kuashiria kuwa walikosa hewa au walikufa wakitafuta hewa.

ii) Uchunguzi wa sampuli za maji yaliyochukuliwa katika eneo haukubaini vimeamaji vinavyohusishwa na sumu Mf. Kundi la Microcystis, dianoflagelates, pseudonitchia, na Gambierdiscus spp. Aidha, uchunguzi wa matumbo ya samaki haukubaini uwepo wa vimeamaji hivi hali inayoondoa uwezekano wa kuwa samaki hao walikufa kutokana na sumu itokanayo na vimeamaji hivyo.

iii)    Vilevile, uchunguzi wa kitaalamu kuhusu uwepo wa viuatilifu, sumu zitokanazo na mimea na kemikali nyingine za viwandani uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali umeonyesha kuwa hakukuwa na sumu katika samaki hao; hivyo kuhitimisha kuwa vifo vya samaki havikutokana na uwepo wa sumu ya aina yoyote ile kwenye maji eneo la tukio.

Kutokana na samaki wengi kuwa na midomo wazi na wengine kuwa na matamvua wazi, uwezekano ni mkubwa kuwa samaki hao walikufa kwa kukosa hewa ya oksijeni.


Imetolewa:                                                                  

Edward Kondela

Kny: Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post