Mapito Ya Lulu Michael Yamebeba Funzo Kubwa, Itoshe Kusema Amemshinda Shetani



Siyo stori kwamba supastaa kiwango kabisa wa Bongo Movies, Elizabeth Michael au Lulu amejaaliwa mtoto wa kiume wikiendi iliyopita.


Julai 17, 2021, Lulu alimzalia mumewe, Francis Ciza au Majizo mtoto huyo mzuri ambaye wamempa jina la G waliloanza kulitumia kabla hata kupata uzao wao huo.


Lulu na Majizo walifunga ndoa Februari 16, mwaka huu; ndoa iliyokuwa ya siri na ilihudhuriwa na watu wachache wa karibu yao.


Gazeti la IJUMAA shuhuda wa mambo makubwa aliyopitia Lulu kwa kusema ni dhahiri kwamba Mungu yupo! Hata wale ambao bado wana shaka juu ya hilo, niaminini mimi. Mungu yupo na kupitia maisha yetu hapa duniani, tunaziona ishara za makuu yake sema wakati mwingine tunajisahaulisha tu kutokana na ugumu wa mioyo yetu.


Mapito ya Lulu yamebeba funzo kubwa linaloonesha ukubwa wa Mungu na namna ambavyo mwanadamu anatakiwa kujitayarisha na mitihani. Mungu akisema ni wakati wa kupata mtihani, mwanadamu huwezi kupinga.


Mipango ya Mungu siyo sawa na ya mwanadamu. Lulu akiwa angali binti mdogo, alianza kuzichanga karata zake kwenye uigizaji. Akakutana na waigizaji ambao wakati huo walikuwa na umri mkubwa kuliko yeye kama Dokta Cheni, Kanumba, Ray na wengine, wakaanza kumkuza kisanaa ndani ya Kaole Sanaa Group.



Bahati nzuri nyota yake ilikuwa njema licha ya umri wake kuwa mdogo, Watanzania wakamkubali. Walimpa thamani ya kuwa staa mwenye umri mdogo. Kama ilivyo kwa mwanadamu yeyote, ni vigumu mno kuhimili kishindo cha ujana kama hutamshika Mungu, Lulu naye akapitia mapito ya ujana.


Alikuwa mtu wa viwanja. Alikuwa binti wa matukio. Kunywa, kulewa, kucheza kihasara kwake haikuwa ishu. Vyombo vya habari hususan Global Publishers viliripoti matukio yake mengi.


Kwenye maisha hayo ya ujana, Lulu alijikuta ameanzisha uhusiano wa kimapenzi na mwigizaji Steven Kanumba (kwa sasa marehemu).


Kanumba ambaye alikuwa mkubwa kiumri kulingana na Lulu, wakati huo, ilikuwa si rahisi sana kuamini kwamba Lulu anaweza kutembea na Kanumba. Kanumba alikuwa mkubwa kwa umri na hata kiumbo.


Wakitembea walikuwa kama mtu na mdogo wake, hivyo ilikuwa si rahisi kuamini kwamba wawili hao wanaweza kuwa na uhusiano wa kimapenzi. Lakini yote kwa yote, Lulu alihimili vishindo. Alitembea na Kanumba akiwa angali hajatimiza umri wa miaka 18.


Waliishi kwenye uhusiano wa siri kwa muda mrefu hadi pale kifo cha Kanumba kilipolidhihirisha penzi lao. Baada ya Kanumba kufariki dunia ndipo kila mtu akajua kwamba Lulu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kanumba. Tena kifo hicho kikampa mtihani mkubwa Lulu akiwa binti mdogo.


Lulu akahusishwa na kifo cha Kanumba. Akayaonja mateso yasiyoendana na umri wake. Alishtakiwa kwa mauaji, baadaye ikawa mauaji ya bila kukusudia. Safari za mahakamani zikawa ndiyo maisha yake.


Anatokea gerezani kuelekea mahakamani. Kwa mara ya kwanza anayaonja maisha ya kupigwa picha mahakamani kama mtuhumiwa wa mauaji. Hili si jambo dogo. Kwa kumtazama mwenzako akiwa anaelekea kizimbani, unaweza kuona ni jambo dogo, lakini kiuhalisia ni jambo zito mno.


Wazazi wa Lulu kipindi hicho walikuwa kwenye majonzi. Kwa vyovyote vile, walikuwa hata wakitamani warudishe siku nyuma na Lulu pengine awe hajajiingiza kwenye uhusiano na Kanumba. Lakini wapi, uhalisia ni kwamba Kanumba alishakufa na Jamhuri ikaendelea na kesi yake.


Lulu alipokata rufaa katika kesi hiyo na kubadilishiwa mashtaka ya kuua bila kukusudia, alipata dhamana. Akarudi uraiani kwa miaka kadhaa. Furaha ikaanza kurejea, akaanza kuyafurahia maisha ya uraiani.

Lakini furaha yake haikudumu kwani kesi iliendelea, akiwa ameshaanza na kuigiza tamthiliya, ghafla akahukumiwa kifungo cha miaka miwili jela. Ndugu zake nao wakarudi kwenye huzuni kubwa. Akatupwa gerezani.


Mungu si Athumani, baada ya safari ndefu yenye milima na mabonde, Lulu akatoka kwa msamaha wa Rais Hayati Magufuli. Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa mateso marefu. Akarudi uraiani. Bahati nzuri alishakutana na mchumba wa ndoto yake, Majizo.


Majizo alikuwa mvumilivu katika kipindi chote cha majonzi ya Lulu. Alipotoka kwa msamaha wa Rais, akamvisha pete kisha mapema mwaka huu akafunga naye pingu za maisha na sasa Mungu amewajaalia mtoto mzuri wa kiume.


Kimsingi maisha ya binti huyu yanatufundisha mengi, kwamba alipangalo Mungu binadamu hawezi kulipangua. Kwenye maisha kuna furaha na majonzi hivyo ni vizuri kama mwanadamu kujiandaa na yote. Maandiko matakatifu yanasema; “Duniani kuna taabu, jipeni moyo!” Itoshe kusema kuwa, Lulu amemshinda shetani na kazi zake zote, kifuatacho ni kumlea mwanawe katika njia impasayo, naye hataiacha hadi uzee wake!

Stori na Sifael Paul

O


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post