Mahakama ya Afrika Kusini kusikiliza rufaa ya Zuma




Mahakama ya Afrika Kusini kusikiliza rufaa ya Zuma
Mahakama ya juu zaidi nchini Afrika Kusini imekubali kusikiliza ombi la Rais wa zamani Jacob Zuma la kutaka kifungo cha miezi 15 jela kifutiliwe mbali.


Siku ya Jumanne Mahakama ya Kikatiba ilimpata na hatia ya kudharau agizo la mahakama la kutokeza kwenye uchunguzi wa ufisadi.



Bwana Zuma alipewa hadi usiku wa manane Jumapili kujisalimisha mwenyewe.



Haijulikani kama uamuzi wa mahakama wa kusikiliza rufaa dhidi ya uamuzi wake wenyewe yanaathiri tarehe ya mwisho iliyowekwa.



Mahakama ya Katiba ilisema kwamba ilipokea ombi la kukata rufaa la Bw Zuma Ijumaa na itazingatia kesi hiyo mnamo Julai 12.



Wakati huo huo, Taasisi ya Jacob Zuma, mfuko wa misaada wa rais wa zamani, ilisema rufaa dhidi ya amri ya kukamatwa itasikilizwa na mahakama kuu ya mkoa wa KwaZulu-Natal Jumanne.



Jacob Zuma 79 aliondolewa mamlakani mnamo 2018, baada ya miaka tisa madarakani, akikabiliwa na shutuma za ufisadi.



Wafanyabiashara walishutumiwa kwa kula njama na wanasiasa kushawishi mchakato wa kufanya uamuzi.



Lakini Bwana Zuma amerudia kusema kuwa yeye ndiye mwathiriwa wa njama za kisiasa. Amekataa pia kushirikiana na uchunguzi juu ya makosa wakati wa uongozi wake.



Rais huyo wa zamani alitoa ushahidi mara moja tu wakati wa uchunguzi wa kile kilichojulikana kama "kukamatwa kwa serikali" lakini akakataa kujitokeza tena baadaye.



Katika suala tofauti la kisheria, Bwana Zuma alikana shutuma zilizomkabili katika kesi yake ya ufisadi iliyohusisha makubaliano ya silaha ya thamani ya dola bilioni 5 kutoka miaka ya 1990.



Umati wa wafuasi wamekusanyika nje ya nyumba yake katika mkoa wa KwaZulu-Natal - wengi wakitarajia kuhakikisha kuwa hapelekwi gerezani.



Mvutano wa kisiasa umekuwa ukiongezeka nchini Afrika Kusini wiki hii, huku wanachama wa chama cha maveterani wa jeshi wakitishia kwamba nchi hiyo italegalega ikiwa Bwana Zuma atakamatwa.



Chama tawala cha Afrika Kusini cha ANC, ambacho Bwana Zuma alikuwa akiongoza, kimetaka utulivu. Lakini akiogopa mgongano mkutano wa kamati yake kuu ya kitaifa umeahirishwa wikiendi hii.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post