Kumekucha.. Kamati yaanika Makosa 6 Anayotuhumiwa Miss Tanzania




Dar es Salaam. Hatimaye kamati ya Miss Tanzania imeweka wazi makosa sita yaliyosababisha kutenguliwa kwa Miss Tanzania 2020/2021,Rose Manfere kwenda kuwakilisha nchi katika mashindano ya urembo ya dunia.

Miongoni mwa makosa hayo ni pamoja na kuunda menejimenti yake nje ya mkataba, kutofuata maelekezo ya kampuni ya The Look, ambao ni wasimamizi wa mashindano hayo na kufanya matangazo ya biashara.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi Julai, 17,2021na Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania,Azama Mwasango alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Mwasango amesema makosa ya mrembo huyo ni pamoja na kutofuata malekezo aliyokuwa akipewa na uongozi wa The Look ambayo ndio kampuni inayosimamia mashindano hayo.


Amesema pia amekuwa hakubaliana na mwongozo anaopewa wa jinsi ya kushirikiana na wadhamini wa shindano kwa mujibu wa mkataba.

“Kwa heshima yake na taji kuna vitu anapaswa afanye na aache, lakini kila anapopatiwa mwongozo sahihi wa kufuata anabisha”amesema na kuongeza.

"Mrembo huyu amekuwa akishiriki matamasha ya watu wengine bila kupata ruhusa ya The Look na wakati mwingine kuomba mialiko jambo ambalo linafedhehesha na kudharaulisha hadhi ya Miss Tanzania kwani kwa hadhi yake inapaswa aalikwe”amesema.


Amesema “Kufanya matangazo ya biashara pasipo kutaarifu kampuni ya The Look na kutozingatia muda kwenye shughuli za kazi, kama mkutano na waandishi wa habari kwa sababu zisizo za msingi kama kudai nguo kucheleweshwa na fundi, ni miongoni mwa makosa yaliyosababisha tumuengue"amesema Mwasango.

Mwasango amesema kama hayo hayatoshi kosa kubwa alilokuwa akilifanya ni kutumia jina la Miss Tanzania kwa maslahi yake binafsi.

“Ameunda menejimenti yake bila kuitaarifu kamati na menejiment hiyo inajitambulisha kwa wadau mbalimbali kuwa ni wahusika wakuu wa kamati ya Miss Tanzania na Miss World na kuiba utambulisho wa The Look.

"Menejiment hii imefanya hivyo kwa Wizara ya Habari,kitu ambacho ni kosa la jinai kama ilivyothibitishwa kwenye barua tuliyoiandikia Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) tukilalamika”amesema.

Maamuzi ya kumtengua Rose, yaliwekwa katika ukurasa wa kamati hiyo Julai 14 na kueleza kuwa Miss Tanzania namba mbili,Juliana Rugamisa ndio atakwenda badala yake.

Katika hatua nyingine,licha ya Basata kuielekeza kamati hiyo kupeleka jina la Rose,Miss World, wamesema tayari wameshalipeleka la Juliana na maandazi yanaendele ya kumuandaa kwenye safari hiyo.

Alipoulizwa haoni kama wanaenda kinyume na maagizo ya Serikali, Mwasango amesema “Sisi ndio tuna leseni na Misa World na sio Basata,kwani yenyewe ipo kwa ajili ya kutoa kibali”amesema.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post