Uganda. Hija Nulu Ssemakula anayeaminika kuwa na familia kubwa ya watoto 115, wake 20 na wajukuu 300, amefariki dunia Julai Mosi nchini Uganda.
Umauti ulimkuta akiwa na umri wa miaka 96 katika kituo cha afya cha Amazing Grace mjini Ntunagmo, baada ya kupata na ugonjwa wa shinikizo la damu.
Gumzo kuhusu mwanamume huyo, linatokana na jinsi alivyoweza kuhudumia familia hiyo kwa mahitaji ya kila siku, yakiwamo chakula, malazi na mavazi pamoja na huduma nyingine muhimu.
Ssemakula ni nani?
Katika mahojiano ya mwaka 2019 na gazeti la Daily Monitor, Ssemakula alisema ameoa wake 19, wanne kati yao walifariki dunia. Aliishi na wake saba katika nyumba moja, ikiwa ni pamoja na mke wake wa kwanza ambaye alimuoa mwaka 1952. Mke wake mdogo alikuwa na umri wa miaka 24 tu huku akiwa na mtoto wa miaka mitatu Pia alioa mke mwingine mwaka 2020 ambaye alijifungua wakati wa kifo cha Ssemakula .
Enzi za uhai wake akiwa katika umri mkubwa, Ssemakula aliweza kufanya shughuli zake mbalimbali kama kulima bustani, kuendesha gari, kusoma Quran, biashara, huku akipata muda pia wa kuwa na familia yake.
Maisha yake yalikuwaje?
Ssemakula anadhihirisha kuwa alikuwa mpenda maendeleo kama alivyothibitisha Waziri wa zamani wa kazi wa nchi hiyo, Mwisigwa Rukutana alipotumia Whatsapp kumkumbuka Ssemakula ambaye pia alikuwa jirani yake.
“Nuhu alikuwa shujaa na picha ya maendeleo na mabadiliko ya kijiji chetu kilichokuwa maskini, kisichokuwa na utaratibu na kurudi nyuma. Alianzisha kilimo cha kahawa na kilimo cha ndizi kibiashara. Alikuwa bora katika utunzaji wa ng’ombe wake wengi hadi pale alipoporwa na vikosi vya ukombozi mwaka 1979. Nina furaha nilimsaidia kupata fidia kutoka kwa serikali ya NRM wakati nilipokuwa DAG Naibu wa Mwanasheria Mkuu), Rukutana aliandika.
Hadi anafariki dunia Ssemakula alikuwa na wake 20 watoto 115, zaidi ya wajukuu 300 na vitukuu kadhaa.Tukio la Ssemakula linafanana na lile lililotokea Juni 14, 2021 ambapo baba wa familia yenye wake 39 na watoto 94 alipofariki dunia akiwa na miaka 76, katika jimbo la Mizoram kaskazini mashariki mwa India, huku akiacha wajukuu 33 na vitukuu kadhaa.Mwanaume huyo, Ziona Chana alifariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu, maradhi yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.
Wake wengi na changamoto za kiafya
Wataalamu wa afya wameeleza madhara ya kiafya na kisaikolojia, anayoweza kuyapata mwanamume mwenye wake wengi. Wameyataja madhara hayo kuwa ni kupata magonjwa ya kuambukiza yakiwamo ya zinaa, virusi vya Ukimwi, homa ya ini pamoja na saratani ya shingo ya kizazi.
Akizungumza na Mwananchi, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka Hospitali ya Salaamani iliyopo Temeke mkoani Dar es Salaam, Dk Abdul Mkeyenge, anasema kitaalamu kuoa wanawake wengi kunaweza kusababisha madhara ya moja kwa moja kwa mwanamume na mengine kwa wanawake.
Anasema ni vigumu mwanamume mwenye wanawake wengi kuweza kuwaridhisha wanawake wote, hivyo kati yao kuna wengine wanakaotoka nje ya ndoa na kuleta magonjwa.
“Kuna madhara ya maambukizi ya magonjwa ya zinaa, kaswende, pangusa na hata virusi vya Ukimwi. Endapo mmoja akiwa na ugonjwa huo ni rahisi mwanamume kuubeba na kwenda kuambukiza wengine,” anasema Dk Mkeyenge.
Pia anayataja magonjwa mengine kuwa ni homa ya ini na saratani ya shingo ya kizazi, kwani mwanamume anaweza kubeba virusi vya magonjwa hayo kutoka mwanamke mmoja kwenda kwa mwingine.
“Endapo mmoja kati ya wanawake hao akiwa na historia ya ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi, basi ni rahisi mwanamume kubeba kirusi cha ugonjwa huo na kupeleka kwa wanawake wengine. Pia homa ya ini inaambukizwa kwa njia ya majimaji, kwa hiyo mwanamume anaweza kuubeba na kuwaambukiza wengine.
“Na kisaikolojia pia inaweza kumuathiri mtu huyu, ujue kuwa na wanawake wengi sio kitu cha kawaida na kila mtu na tabia yake, kwa hiyo inaweza kuleta shida kwenye mambo ya saikolojia,” anasema Dk Mkeyenge.
Wake wengi inawezekana
Hata hivyo, kwa Dk Deogratius Mahenda kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), anasema hakuna tatizo kwa mwanamume kuwa na wake wengi, lakini tatizo linaweza kuwa ni uwezekano wa kupata magonjwa ya zinaa.
“Kiukweli mwanamume kuwa na wanawake wengi hakuna shida, na wala hawezi kupata tatizo lolote, isipokuwa madhara makubwa ni kwa yale magonjwa yanayohusiana na kujamiiana, labda na matatizo ya kisaikolojia,’’ anasema.
Anaongeza: “Ingawa zipo dini ambazo zinaruhusu kuoa wanawake wengi, suala la magonjwa kama akitokea mwanamke si mwaminifu na akaenda nje ya ndoa, akipata magonjwa ya zinaa, ni rahisi mwanamume kuyabeba na kwenda kuwasambazia wanawake wengine.’’
Hapa Tanzania na maeneo ya Afrika Mashariki, ndoa hizo zimeshamiri, sababu kuu ikiwa suala la dini na utamaduni wa maeneo hayo, huku katika maeneo mengine likibaki kuwa mjadala mkali hasa kwa wanawake.
Mfano mzuri ni mzee Meshuko Ole Mapi wa Monduli mkoani Arusha, aliyeripotiwa kuwa na wake nane, watoto zaidi ya 76 na wajukuu 300.
Ole Mapi maarufu kwa jina la Mzee Laibon alilazimika kuwa na shule yake na soko kwa ajili ya jamii yake hiyo, kiasi cha kusababisha kuwa kivutio kwa watalii wengi ambao hufika mkoani humo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa dini ya Kiislamu, pamoja na mafundisho yake kuruhusu mwanamume kuoa wengi, dini hiyo imeweka utaratibu wa idadi ya wanawake ambao ni wanne, idadi ambayo wataalamu wa afya wanasema haina madhara.
Post a Comment