DPP kuamua hatma hausiboi aliyeua familia Dar



 
DPP kuamua hatma hausiboi aliyeua familia Dar  
JESHi la Polisi Mkoa wa Kinondon limesema upelelezi kuhusu mauaji ya mama na watoto wake wawili wa kike umekamilika na faili limepelekwa Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP) kwa hatua zaidi.

Ilidaiwa kuwa Emilly Mutaboyerwa na binti zake Damita (13) na Daniela Mutaboyerwa (15), waliuawa Juni 9, mwaka huu na miili ilikutwa Juni 11 nyumbani kwao Mtaa wa Maryknol, Masaki wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Polisi walimkamata Shadrack Kapanga (34) akituhumiwa kufanya mauaji hayo akiwa ni mfanyakazi wa ndani katika familia hiyo.

Imefahamika kuwa Kapanga ni mtuhumiwa namba moja katika shauri hilo na pia polisi walimkamata aliyedaiwa kuwa alikuwa mpenzi wa Emily na hadi sasa wapo rumande.


 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Ramadhani Kingai alisema upelelezi umekamilika na jalada la kesi lipo kwa DPP.

“Jeshi la Polisi Kinondoni limeshakamilisha kazi ya uchunguzi wa sakata hili la mauaji na kwa upande wetu kama ilivyo kawaida tukishawasilisha faili kwa ofisi ya DPP tunangojea kama kunakuwa na maelekezo mengine,” alisema Kamanda Kingai.

Aliongeza, “Kama likiwa sawa kwa maana ya upelelezi umekamilika inabakia suala la kupelekwa mahakamani kwa watuhumiwa na kuanza kwa kesi, kwa sasa bado tunawashikilia watuhumiwa hawa na wapo wawili aliyekuwa mfanyakazi na aliyekuwa mpenzi wa mama wa watoto wale waliouawa.”


Kuhusu watu wangapi walihojiwa, Kamanda Kinai alisema suala hilo hawezi kulizungumzia, lakini akasema watu wawili walikamatwa ila wapo wengine waliohojiwa.

Kapanga alikutwa akiuza simu za marehemu, televisheni, kisimbuzi cha DSTV na rimoti na alidaiwa alikuwa katika jitihada za kutoroka.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post