BARAZA la Wanawake la Chadema (Bawacha), limeiandikia barua Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, likiitaka uingilie kati tukio la kushikiliwa kwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe, kwa tuhuma za ugaidi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu, leo tarehe 29 Julai 2021, Katibu Mkuu wa Bawacha, Catherine Ruge, amesema barua hiyo wameipeleka jana katika ofisi za ubalozi huo, zilizoko mkoani Dar es Salaam.
Ruge amesema kuwa, barua hiyo ilipokelewa na Mkuu wa Masuala ya Siasa na Uchumi wa ubalozi huo, Douglas Morris, ambaye alisema watatoa tamko kuhusu tukio hilo wakati wowote kuanzia jana.
“Ni kweli tumeandika barua na imepokelewa na ubalozi jana, Morris alisema watatoa statement (tamko) muda wowote kuanzia jana,” amesema Ruge.
Katika barua hiyo ya Bawacha kwenda kwa ubalozi huo, baraza hilo linamuomba Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald Wright, atoe tamko la kuitaka Serikali imuache huru Mbowe bila masharti yoyote.
“Tunakuomba usimame kwa ajili ya misingi ya uhuru na haki za msingi za Watanzania, kama zilivyowekwa katika katiba na kanuni za msingi za haki za binadamu za kimataifa. Pia, tunakuomba utoe wito wa kutaka Mbowe aachwe huru haraka bila masharti yoyote, ambaye haki zake zimekiukwa,” imesema barua hiyo.
Mbali na hatua hiyo ya Bawacha kuwasilisha kilio hicho katika ubalozi huo, Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR), imetoa tamko kuhusu tukio la Mbowe na wenzake 11 kukamatwa jijini Mwanza.
Mbowe aliyeko rumande katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam na wenzake walikamatwa wakiwa katika Hoteli ya Kingodom Mwanza, usiku wa kuamkia tarehe 21 Julai 2021, wakijiandaa kushiriki kongamano la kudai katiba mpya, lililoandaliwa na Chadema.
Tamko hilo lililotolewa jana tarehe 28 Julai 2021 na Mwakilishi wa ACHPR nchini Tanzania, Solomon Ayele Dersso, limeiomba Serikali ya Tanzania iheshimu misingi ya kisheria, ili kutojenga hofu kwa wanasiasa wa vyama vya upinzani.
“Tume inaeleza wasiwasi wake kwamba, kutozingatiwa kwa haki katika michakato ya kisheria kama ilivyotamkwa katika mkataba wa Kiafrika ibara ya saba, inasababisha unyanyasaji wa haki ya kuwa huru dhidi ya kukamatwa kinyume cha sheria na kujenga mazingira ya hofu kwa vyama vya upinzani,” limesema tamko hilo.
Tume hiyo imeziomba Mamlaka za Tanzania, kutotumia vibaya sheria kwa ajili kuminya uhuru wa watu kujieleza.
“Tume inaisistiza kwamba, hatua zote zinapaswa kuwekwa ili kuzuia kuingiliwa kwa haki ya mchakato unaofaa wa sheria, uhuru wa kujieleza, haki ya uhuru wa kujumuisha na haki ya kukusanyika kwa amani, iliyohakikishiwa chini ya Ibara ya 7,9,10 na 11 ya mkataba wa haki za binadamnu ya Afrika,” limesema tamko hilo.
Tume hiyo imeziomba mamlaka zinazohusika na masuala ya kisheria na usalama Tanzania, kutekeleza kanuni za ACHPR na miongozo yake, kutenda haki katika masuala ya kisheria.
“Tunaomba mamlaka husika zitetee haki ya uhuru wa kujumuika na kukusanyika, ili kutoa nafasi sawa kwa raia na uhuru wa vyama vya upinzani nchini,” limesema tamko hilo.
Tangu Mbowe akamatwe na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza na kupelekwa katika Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kwa ajili ya kuhojiwa dhidi ya tuhuma za ugaidi zinazomkabili, makundi mbalimbali yameibuka kupinga hatua hiyo.
Hata hivyo, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa, aliyataka makundi hayo yaziache mamlaka husika zifanye kazi yake kwa mujibu wa sheria.
Mbowe alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Julai 2021 na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi na ugaidi.
Kwa mujibu wa mashtaka hayo, Mbowe anadaiwa kula njama na kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi. Inadaiwa kuwa, Mbowe alitenda makosa hayo kati ya Mei na Agosti 2020, kwenye Hoteli ya Aishi, Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kesi ya Mbowe, inatarajiwa kusikilizwa tena tarehe 5 Agosti 2021, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha nyaraka muhimu katika Mahakama Kuu, kwa ajili kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo.
Post a Comment