Bocco na Nado Wazawa Wakali wa Kucheka na Nyavu




WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara ikitarajiwa kufika tamati jana rekodi zinaonyesha kuwa wazawa watatu wamekuwa ni mwiba kwa upande wa kucheka na nyavu msimu wa 2020/21.

 

Ni John Bocco anayekipiga ndani ya Simba kwenye chati yupo namba moja akiwa ametupia mabao 15 na ana pasi mbili za mabao kibindoni. Timu yake imefunga jumla ya mabao 74.

 

Yupo mwingine kutoka Azam FC, Idd Seleman, ‘Nado’ ambaye yeye ametupia jumla ya mabao 10, katika mabao hayo amewatungua Simba nje ndani kila walipokutana kwa msimu huu ule mchezo wa kwanza, Uwanja wa Mkapa na ule wa pili Uwanja wa Azam Complex.

 

Azam FC ipo nafasi ya tatu ina pointi 65 ikiwa imefunga jumla ya mabao 52 baada ya kucheza jumla ya mechi 33.

 

Mzawa mwingine mkali wa kucheka na nyavu ni Danny Lyanga ambaye yupo zake JKT Tanzania akiwa ametupia mabao 10. Licha ya kuwa na mabao mengi timu yake ipo kwenye mstari mwekundu wa kushuka daraja na jana hatma yao ilitarajiwa kufahamika rasmi.

 

Ilikuwa nafasi ya 15 na pointi 36 na imefunga jumla ya mabao 32. Tayari mabingwa wameshapatikana ambao ni Simba wakiwa na pointi 80 nafasi ya kwanza ambapo jana walitarajiwa kukabidhiwa taji la ubingwa.

Mwandishi wetu, Dar es Salaam




0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post