BENCHI la Ufundi la Yanga linaloongozwa na Kocha Mkuu Mtunisia, Nasreddine Nabi, limefichua kwamba lilikoshwa na aina ya wachezaji wao Yacouba Songne na Waziri Junior kwa kuwa walifanyia kazi kile walichowaelekeza.
Juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, Yanga ilipocheza dhidi ya Mwadui wakati wakiwa nyuma kwa mabao 2-1, Nabi alifanya mabadiliko kwa kuwaingiza wachezaji hao na kubadili ubao ambao mwisho ulisoma Yanga 3-2 Mwadui, huku kila mmoja akifunga bao moja.
Kocha wa makipa wa Yanga, Mkenya, Razack Siwa, ameliambia Spoti Xtra, kuwa mastraika hao waliyatendea kazi maelekezo ambayo waliwapa ya kumalizia nafasi nyingi za wazi ambazo walikuwa wanazipata na kushindwa kufunga.
“Tulikuwa nyuma kwa mabao 2-1, hivyo tukaingiza watu ambao watatusaidia ambao ni Yacouba na Waziri na tuliwaelekeza kutumia hizo nafasi ambazo tulikuwa tunakosa.
“Tuliwaingiza watu wa spidi kwa ajili ya kupata hizo nafasi na mabadiliko hayo yakafanya kazi kazi kwa kupata ushindi huu. Kocha amefurahishwa na viwango vyao.”
Tofauti na kufunga bao moja, Yacouba alihusika pia kwenye bao la tatu baada ya kumpa pasi Tuisila Kisinda ambaye alitoa asisti kwa mfungaji, Wazir Junior.
STORI: SAID ALLY, Dar
Post a Comment