Sheikh Farid Atema Nyongo, Aelezea Maisha ya Gerezani "Serikali Itumie Busara Kutufidia"

 



Unguja. Aliyekuwa kiongozi wa Jumuiya ya Maimam ya Uamsho Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed, ameeleza mambo mbalimbali kuhusu maisha yake ya gerezani na changamoto alizozipitia tangu alipokamatwa mwaka 2014.


Mbali na changamoto hiyo, amezungumzia madhila ya hasara aliyoipata na mipango yake ya baadaye baada ya kuachiliwa huru kuanza na maisha mapya na familia yake.


Juni 15 mwaka huu, Sheikh Farid na mwenzake, Msellem Ali Msellem aliyekuwa kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki) waliachiwa huru baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwafuatia mashtaka yaliyokuwa yanawakabili huku wenzao wakiendelea kutoka kwa nyakati tofauti.


Sheikh Farid na wenzake 35 walikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na makosa ya ugaidi kinyume na kifungu cha 27(c) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002, wakidaiwa kutenda makosa hayo Januari 2013 na Juni 2014, Tanzania Bara na Zanzibar.


Watu wote waliokuwa wanashikiliwa na kina Sheikh Farid na Mselem kwa sasa wameachiliwa kutoka gerezani.

Awali, walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Septemba 3, 2014 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kwa hatua za awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa usikilizwaji kamili; wakikabiliwa na mashtaka 25.


Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu nyumbani kwa mama yake Bububu Unguja jana, Sheikh Farid alimshukuru Mungu kwa hatua hiyo licha ya kudai wameathirika kwa kiasi kikubwa.

 

Wakati akizungumza, Sheikh Farid alianza kuelezea kwa sauti ya upole akisema, “maisha ya gerezani kwa kweli ni maisha mazito, gereza halina maisha mapesi, hata hivyo zile haki zako na utu wako havithaminiwi, kwa kweli ni changamoto kubwa sana.”


Sheikh Farida alisema katika kipindi cha miaka minane hawezi kusahau kwa sababu kuna mambo yanafanyika lakini hayana maana na kibinadamu hayana utu ndani yake.


“Kupekuliwa binadamu ni jambo la kisheria, lakini linahitaji faragha, sisi tuliingia gerezani lakini utaratibu wake wa kusachiwa haukuwa rafiki hata kama kuna sheria inayotaka hivyo,” alieleza Sheikh Farid, mwenye wake wawili na watoto 17.


Sheikh Farid alisema wanaopewa majukumu hayo kuna wakati wanatumia sheria vibaya kutekeleza wanayoambiwa.


Hata hivyo, alidai kuwa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, pia mambo yao ya mahabusu yalianza kubadilika.


Alisema kipindi cha nyuma walikuwa wakifanyiwa ukaguzi baada ya kupigwa kipenga.

“Ukisikia kipenga hicho moyo unaanza kudunda kutokana na mazingira unayokwenda kukutana nayo kwenye ukaguzi, sio ya kawaida.”


Sheikh Farid alisimulia ndani ya mahabusu kuna sehemu kama ukumbi, licha ya kutengwa vyumba vinne na kila chumba wanalala watu si chini ya 60 huku wakilalia vigodoro vya inchi mbili na nusu kwa sita vinavyokutanishwa kwa pamoja.


Kitu anachokisifia gerezani

“Kwa kweli gerezani haushindi na njaa na chakula kinakuja kwa wakati, ikifika saa 6:00 mchana chakula kinakuwa tayari,” anasimulia.


Sheikh Farid alisema katika siku za mwanzo walitengwa yeye na Msellem, lakini hawakutengwa kama adhabu bali ilikuwa ni namna ya kuzuia vurugu kwa sababu wao ni viongozi.

Alisema wakiwa humo mahabusu walikutana na watu wengi hasa vijana, lakini waliwapa ushauri.


Kuhusu mali zake

Sheikh Farid alisema amepoteza biashara zake zote zenye thamani ya Sh40 milioni ambazo alimiliki, ikiwamo teksi, daladala, boti tatu na mashine za uvuvi moja kati ya hizo moja thamani ya Sh12 milioni. Huku mashine yake ikiwa na thamani ya Sh8 milioni na nyavu za Sh10 milioni.


Alisema boti nyingine ilikuwa ni ya uvuvi wa kawaida yenye thamani ya Sh6.5 milioni na nyingine Sh10 milioni iliyokuwa ina mashine pamoja na nyavu.

“Mali hizo zote sikuzikuta kwa sababu niliziacha katika mazingira nisiyoyatarajia na nyingine zilikuwa kwenye mikono ya watu. Kuna mali nyingine zilipotea hata sijui zimepoteaje,” alisema.


Mipango ya baadaye

Farid alisema kutokana na hali ilivyo ana mipango mbalimbali anayotarajiwa kuifanya ikiwamo kuanzisha kilimo cha nyanya, pilipili hoho, mapapai.


Hata hivyo, Farid alisema ni mapema kueleza kwa usahihi wa biashara atakazofanya, lakini atakaa pamoja na familia yake na ndugu zake kuangalia mchakato huo.

“Nilikuwa na biashara nyingi naziendesha, kwa sasa siwezi kusema moja kwa moja nitakachokifanya ila tutakaa na familia yangu na ndugu zangu. Nina wake zangu wawili na watoto 17 hivyo lazima tushirikishane,” aliongeza Sheikh Farid.


Alichofaidika nacho akiwa mahabusu

Wakati akielezea mipango yake ya baadaye, alisema akiwa mahabusu alikutana na watu mbalimbali waliomfundisha kilimo cha kitaalamu na chenye faida ya haraka ikiwamo cha pilipili hoho.


Sheikh Farid alisema wakati watu wakimfundisha alikuwa akiandika kwenye daftari lake, akisema suala hilo huenda likawa ni miongoni mwa miradi yake ya baadaye.


Alivyotoka gerezani kwenda nyumbani

Sheikh Farid alisema wakati anatoka gerezani kwenda Unguja hakuna ndugu yake wa karibu aliyekuwa akijua, walimuona akifika nyumbani kwasababu hawakuwa na taarifa yoyote

Baada ya kutoka gerezani, alisema walipewa mtu na utaratibu maalumu wa kusindikizwa hadi Unguja na hawakatakiwa kutoa taarifa kwa mtu yeyote hadi watakapofika.

“Tulisafirishwa kwa ndege na Serikali hadi Uwanja wa Aman Abeid Karume Zanzibar, tulipofika tulikuta magari mawili yakitusubiri kila moja litupeleke tunapoishi. Mimi nilisema nipelekwe kwa mama yangu mzazi nikaletwa hapa (Bububu) nilifika saa3.00 usiku,” aliongeza.


Mazingira ya kuachiwa

Alisema siku ya kuachiwa waliitwa katika jengo la utawala la Gereza la Ukonga na kuambiwa wasubiri utaratibu, ilipofika saa 10.00 alasiri waliamriwa kuingia ndani ya chumba maalumu kwa ajili ya kesi yao kusikilizwa kwa njia ya mtandao.

Baada ya kuanza kusikiliza mawakili wa upande wa mashtaka walimueleza jaji kwamba Serikali haina nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao.


“Haikuchukua muda mrefu kesi yetu kusikilizwa kutolewa uamuzi. Jaji aliingia na wakili wa Serikali akasema mheshimiwa tupo mbele yako tuna kesi, tukaitwa majina yetu sisi wawili kisha akasema Jamhuri imeona haina sababu ya kuendelaa na kesi hii, kwa hiyo tumeamua kufuta kesi hii, jaji akasema mmeachiwa huru,” alieleza Sheikh Farid.


Alisema baada ya kutoka chumba cha Mahakama walirudi mahabusu kuchukua nguo zao na baadhi ya vitu vya msingi kama miwani, lakini walielezwa kuwa hawawezi kuachwa hapa lazima wapelekwe Zanzibar.


Furaha aliyoipata alipoachiwa

Sheikh Farid alisema katika muda wote huo alikuwa kwenye furaha kwa sababu kesi ilivyokuwa hawakuwa na matumaini maana ilikuwa imesukwa kiuongo na kama ingeendelea ilikuwa inaonekana wazi watashinda.


Chanzo cha sakata lao

Sheikh Farid alisema mshikemshike huo waliopata ulitokana na mchakato wa mabadiliko ya katiba, akisema sheria iliyotoa fursa kwa taasisi na jumuiya za dini na za kawaida kutoa elimu jinsi gani ya kutoa elimu na mafao baina ya nchi hizi mbili, Zanzibar na Tanganyika zilizoungana.


Kuhusu kufungua madai

Alisema kama busara ilivyotendeka wakaachiwa basi wanaamini Serikali itatumia busara hiyo kuwaangalia walivyopata athari.

“Tumedhulumika kwa muda mrefu, kwa hiyo kunahitajika busara ya Serikali, tunachoomba zaidi ni amani ya nchi na hekima vitawale kwenye hayo, tunaamini vitafanyika, kwa hiyo tukae mezani tuyamalize haya,” alisema Sheikh Farid.

“Kwa hiyo kuna umuhimu mkubwa wa kukutana na Serikali tuzungumze haki zingine zipatikane,” alisema.


Tayari masheikh 36 wameachiliwa huru na kurudi nyumbani Unguja hadi jana jioni.


Mwananchi



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post