“Sasa Bwana, niruhusu mimi mtumishi wako niende kwa amani kama ulivyoniahidi, kwa sababu macho yangu yameuona wokovu ulioandaa mbele ya watu wote, nuru itakayowaangazia watu wa mataifa na kuleta utukufu kwa watu wako Israeli.”
Alisema Simeoni, aliyekuwa Mwenye Haki na Mcha Mungu, akimuomba Mungu achukue pumzi yake ya uhai, kwani alimuahidi kuwa hatakufa kabla ya kumuona Mwokozi wa Dunia, Yesu Kristo. Imendikwa, Luka 22:25-35.
Inaelezwa kuwa kwa mfanano usiokuwa na usawia wa moja kwa moja, Mhubiri maarufu nchini Nigeria, Temitope Balogun Joshua maarufu kama ‘TB Joshua’, alipata hisia za kupoteza pumzi ya uhai, akiwa anaonekana kwa wengi kuwa buheri wa afya. Akawaaga waumini wake kwa ujumbe ambao ulikuwa fumbo, hadi walipolifumbua muda mfupi baada ya kupata habari kuwa amefariki dunia.
“Kuna muda wa kila kitu, muda wa kufika hapa kanisani kwa ajili ya maombi, na muda wa kurejea ‘nyumbani’ baada ya kutoa huduma,” inaelezwa kuwa alisema TB Joshua wakati wa ibada, Juni 5, 2021. Hivi sasa waumini wake wanaamini kuwa aliposema ‘nyumbani’, hakumaanisha nyumbani kwake bali alimaanisha kurejea tulipotoka, yaani kwa Mwenyezi Mungu.
TB Joshua
TB Joshua, kwa maelezo yaliyopo, hakufa tu kimaajabu, lakini kuzaliwa kwake hakukuwa na ukawaida, na maisha yake yalijaa vitimbi, mateso, miujiza, utata mkubwa wa miujiza iliyotokea kanisani kwake…. Na sasa amepumzika.
Ni hivi…. Mama mmoja maskini sana alishika ujauzito ambao uliompa tabu sana. Aliishi na ujauzito huo kwa kipindi cha miezi 15 badala ya miezi 9.
Alimuomba Mwenyezi Mungu amnusuru na asichokijua ndani ya tumbo lake, asielewe ni mtoto wa aina gani aliyeng’ang’ania ndani ya tumbo lake!? Hatimaye, mama huyo alijifungua mtoto wa kiume, Juni 12, 1963 katika mji wa Akoko nchini Nigeria. Akampa mwanaye jina la Temitope Balogun. Baba yake aliitwa Francis. Hapo tukampata Balogun Francis. Je, jina TB Joshua lilitoka wapi? Endelea…!
Kwa mujibu wa tovuti hiyo, inaelezwa kuwa kuzaliwa kwa mtoto Bolugun kulitabiriwa miaka 100 iliyopita. Inaelezwa kuwa ilitabiriwa kuwa mtoto wa kiume atazaliwa katika familia maskini kwenye makazi duni ya Oosin, na kwamba Mwenyezi Mungu atamtumia.
Imeelezwa kuwa siku saba baada ya kuzaliwa kwake, mtu asiyejulikana alirusha bomu juu ya paa la nyumba yao alipokuwa mtoto huyo. Hata hivyo, kwa mkono wa Mungu bomu hilo halikufanikiwa kuuondoa uhai wa mtoto Bolugun Francis.
Mtoto huyo alisoma na kumaliza shule ya msingi mwaka 1977, lakini kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi sana alishindwa kukamilisha elimu yake ya Sekondari, akaacha katika mwaka wa mwisho.
Hapo ndipo utaamini kuwa sio lazima kila mtu apite njia uliyopita kufikia mafanikio. Madarasa ya elimu yapo mengi, ukishindwa ya shuleni, yapo madarasa ya mtaani.
Akiwa na umri mdogo, mtoto huyo akaingia mtaani kutafuta maisha. Alifanya kazi nyingi za kawaida ikiwa ni pamoja na kazi za kubeba taka za kuku na kusafisha mashamba. Alijaribu kujiunga na jeshi lakini Kabla ya kuingia kambini mafunzo yalisitishwa, ikabidi arejee tena mtaani.
Hata hivyo, wakati wote alikuwa anapenda kusoma Biblia na walimtania kwa jina la ‘mchungaji mdogo’ (small pastor).
Joshua anasema wakati anahangaika na maisha, alipata maono kuwa anapaswa kuanzisha huduma ya kichungaji itakayokuwa kubwa. Hakujiuliza mara mbili, anasema alianzisha ‘The Synagogue, Church of All Nations (SCOAN).
The The Synagogue, Church of All Nations (SCOAN)
Baada ya maono hayo, alipanda mlimani kusali. Akafunga kwa siku kadhaa, akarejea uraiani akiwa amekonda sana. Na kisha akaendeleza huduma yake akiwa na jina jipya ‘Nabii TB Joshua’.
Alisimulia maisha yake mafupi kupitia kipande cha video alichoonesha, ambacho awali alikuwa anarekodi hatua za maono yake. Huduma yake ilianza akiwa na waumini wanane tu. Mara kadhaa kanisa lake la tope lilisombwa na maji, lakini alijenga tena jingine. Hakukata tamaa. Lakini leo huduma yake ina zaidi ya waumini 15,000 wanaohudhuria ibada moja ya Jumapili.
Ingawa ana umaarufu mkubwa duniani kote, TB Joshua alikataa kufungua matawi ya huduma yake, alisema italeta mkanganyiko katika kupata aina ya viongozi wenye sifa zinazomuakisi yeye. Hivyo, kanisa lake lina tawi moja tu lililopo nchini Ghana, na makao makuu ni Lagos, Nigeria.
Kanisa la TB Joshua limekuwa moja kati ya vivutio vikubwa vya watalii wa kidini. Kwa mujibu wa Idara ya Uhamiaji ya Nigeria, watu 6 kati ya 10 wanaotoka nje ya nchi kutembelea nchi hiyo, safari yao ina uhusiano na kutembelea kanisa la TB Joshua. Gazeti la ‘This Day’ liliripoti kuwa takribani watu milioni 2, watalii wa ndani na nje hutembelea kanisa hilo kwa mwaka.
TB Joshua, alikuwa na mengi makubwa, alipendwa na wengi na alichukiwa na wengi. Alipendwa na kuwa mfano kwa watumishi wa Mungu wengi duniani, lakini alichukiwa na kulaaniwa na watumishi wa Mungu wengi pia ikiwa ni pamoja na wenzake wa Nigeria. Nani anafahamu yupi ni mtumishi halisi wa Mungu? Kasome Mathayo 7: 16-20. Wapo waliomuita ‘mtoto wa Mwenyezi Mungu’. Wengine walifikia hatua ya kumuita ‘mtoto wa ibilisi’. Inategemea unaamini nini.
Wengi walimpenda kwakuwa waliamini kupitia maombi yake Mwenyezi Mungu aliwaponya. Wengine hawakuamini hata kidogo, walidai anatumia nguvu za giza. Mambo ya imani yaachie waumini!
Mfano wa jambo lililoweza kutikisa na kuwagawa watu na Serikali, ni pale alipotangaza kuwa maji ya upako aliyoyatoa yalikuwa na uwezo wa kuponya ugonjwa wa Ebola.
Alitoa msaada wa chupa 4,000 za maji hayo pamoja na kiasi cha fedha $50,000 kwa wahanga wa Ebola nchini Sierra Leone. Sasa wakati huo, Seriklai ya Nigeria ilifika ofisini kwake na kumhoji huku ikimtaka kuacha kuwahamasisha wagonjwa wa Ebola kwenda kanisani kwake kuombewa. Lakini wakati huohuo, mwanasiasa maarufu wa Sierra Leone, Bi. Kargbo Fatmata alisema chupa za maji ya upako zilizowasili nchini humo ndizo zilizosaidia kupunguza kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola.
Kanisa lake limewahi kuonesha video kadhaa za TB Joshua akitabiri kuhusu mambo mengi makubwa, ambayo yalitokea. Mfano: kupotea kwa ndege ya Shirika la Malaysia – MH370.
Hata hivyo, yapo mengi ambayo ilidaiwa alitabiri na hayakwenda kama alivyotabiri.
Mwisho wa siku tukubali kuwa alikuwa msaada kwa wengi wenye matatizo. Aliwasaidia watu kwa fedha, vyakula, malazi na mengine mengi.
Alisaidia kuleta usuluhishi na upendo sehemu nyingi zilizokuwa na harufu ya moshi wa chuki au kutoelewana kwa kiasi kikubwa. Mfano,
TB Joshua alisaidia kusuluhisha mgogoro mzito kati ya familia ya aliyewahi kuwa Rais wa Liberia, Samuel Doe na aliyekuwa mbabe wa kivita Yormie Johnson. Mbabe huyo wa kivita alimpindu Samuel Doe, akamtesa na kumuua kikatili kwa kumkata vipande mwaka 1990.
Unaweza kuhisi chuki kiasi gani iliyopo kwenye mioyo na damu ya familia ya Rais Doe dhidi ya muuaji huyo.
Lakini katika miaka ya hivi karibuni, muuaji huyo alitubu na kurejea mikononi mwa Mungu. TB Joshua aliwakutanisha familia hiyo na bwana Johnson kwa lengo la kusuluhisha. Wakazungumza kwa kirefu na kusali. Mwisho, walijitokeza hadharani wote wakiwa na TB Joshua. Familia hiyo ikatangaza kuwa imemsamehe muuaji wa baba yao.
Katika siasa, tukumbuke TB Joshua aliitembelea Tanzania siku chache baada ya uchaguzi wa mwaka 2015, ambao ulikuwa na ushindani mkubwa. Alizungumza na waliokuwa wagombea wenye ushindani Mkubwa, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli (CCM) na Edward Lowassa (Chadema), pamoja na pande mbili za vyama vyao; mambo yakawa shwari zaidi.
Novemba 2019, aliitembelea Sudan Kusini na kupokelewa na Rais Salva Kiir Mayardit. Walifanya kikao na akaliombea Taifa hilo kuwa na amani na kusitisha mgogoro wa kivita. Februari 2020, Sudan Kusini iliunda Serikali ya Umoja wa kitaifa, iliyomshirikisha Rais Salva Kiir na aliyekuwa hasimu wake, Riek Machar.
Tukumbuke tu, kwa Tanzania tuna muunganiko kwa familia ya TB Joshua, hususan kwa kuwa binti yake Serah Joshua alifunga ndoa na kijana wa Kitanzania, Brian Moshi.
TB Joshua ameacha mjane na watoto watatu. Lakini amewaacha waumini wake wengi duniani.
Hivi sasa, TB Joshua ni mwendazake. Lala TB Joshua, umevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo umeumaliza na imani umeilinda.
Dunia itakukumbuka kwa mengi.
Post a Comment