Takribani watu saba wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa makundi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran wameuawa katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Jeshi la Marekani karibu na mpaka kati ya Iraq na Syria.
Shirika la kutetea haki za binaadamu nchini Syria limesema mashambulizi hayo yametokea usiku wa kuamkia Jumatatu na kuchochea wito wa kulipiza kisasi na hofu ya kuongezeka kwa mzozo kati ya Marekani na Iran.
Siku ya Jumapili, wizara ya ulinzi ya Marekani ilieleza kuwa Rais Joe Biden aliamuru kufanyika kwa mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo yanayotumiwa na wanamgambo hao kwenye mpaka huo.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani – Pentagon, John Kirby, alisema maeneo hayo yalikuwa yanatumiwa na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran kufanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya maafisa wa Marekani na maeneo yao nchini Iraq.
Maeneo mawili nchini Syria na moja nchini Iraq, ambayo yote yako karibu na mpaka kati ya nchi hizo mbili, yalilengwa. Aidha, Kirby amesema kuwa mashambulizi hayo yalikuwa ya kujilinda.
Shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza, lilisema kwamba mbali na wapiganaji waliouawa, wengine waliojeruhiwa wana mafungamano na vikosi maarufu vya uhamasishaji vya nchini Iraq, ambavyo vinajulikana pia kama Hashed al-Shaabi.
Kwa mujibu wa shirika hilo, mashambulizi hayo yalililenga jimbo la Deir al-Zour. Duru za kundi la wanamgambo wa Hashed al-Shaabi zimeliambia shirika la habari la Ujerumani, dpa, kwamba takriban wapiganaji wake wanne wameuawa.
Mashambulizi ya sasa ni ya pili ya kijeshi kufanywa chini ya utawala wa Rais Biden katika eneo hilo. Katika maagizo yake ya kwanza ya kulipiza kisasi akiwa Rais wa Marekani mwezi februari, Biden aliruhusu mashambulizi yafanyike dhidi ya makundi ya Wanamgambo yanayoungwa mkono na Iran mashariki mwa Syria katika kujibu mashambulizi ya roketi dhidi ya Marekani pamoja na miundombinu yake nchini Iraq.
Baadhi ya makundi ya wanamgambo yanayounda vikosi vya Hashed al-Shaabi yalipelekwa Syria miaka kadhaa iliyopita, kuviunga mkono vikosi vya utawala na kuendeleza maslahi ya Iran nchini humo.
Mashambulizi haya yamefanyika siku mbili baada ya Marekani na Ufaransa kuionya Iran kwamba muda unayoyoma wa kurejea kwenye makubaliano ya nyuklia, na kuelezea hofu kwamba shughuli za kurutubisha madini ya urani za Iran zinaweza zikaendelea, ikiwa mazungumzo yatasuasua.
By- BAKARI WAZIRI
Post a Comment