Mamlaka zakanusha mwanamke kujifungua watoto 10 Afrika Kusini





Mamlaka nchini Afrika Kusini zimebainisha kuwa Gosiame Sithole hakujifungua watoto 10 kama ilivyoelezwa na wala hakuwa mjamzito.

Uongozi wa Mkoa wa Gauteng nchini humo umesema umefanya uchunguzi wa kina na kubaini kwamba hakuna hospitali ya umma au ya binafsi ilioweka rekodi za kujifungua kwake.

Kulingana na mwandishi wa BBC,  hatua hiyo inajiri baada ya mwanamke huyo kudaiwa kujifungua watoto na haikuthibitishwa.

Leo Alhamisi Juni 24, 2021 taarifa ya idara ya afya inaeleza kuwa Gosiame hakujifungua hivi karibuni  na wala hakuwa na ujauzito wowote bila kueleza sababu za mwanamke huyo kudanganya kuhusu ujauzito na kujifungua watoto hao na kwamba anapatiwa tiba ya kisaikolojia.

Mwandishi aliyechapisha habari hiyo,  Piet Rampedi huenda akachukuliwa hatua baada ya serikali kuagiza ofisi ya mwanasheria mkuu kumfungulia mashtaka.

Rampedi aliandika habari hiyo akieleza kuhusu kujifungua kwa mwanamke huyo.

Ujauzito huo ulivutia hisia tofauti katika mitandao ya kijamii kote duniani na watu wakaanza kutuma ufadhili kwa wazazi wa watoto hao.

Hata hivyo habari hiyo ilianza kutiliwa shaka baada ya Rampedi kushindwa kutaja hospitali ambayo watoto hao walizaliwa huku baadhi ya hospitali katika mkoa huo zikipinga madai kwamba mama huyo alikuwa amejifungua katika hospitali zao.

Shirika la habari la mitandaoni linalomiliki Pretoria News na ambalo ndilo la kwanza kuripoti habari hiyo lilisimama kidete na kuunga mkono taarifa yake.

Jumanne wiki hii taarifa iliyovuja ilieleza kuwa Rampedi aliomba msamaha katika chombo cha habari hicho kwamba hiyo ilikuwa habari nzuri na alihisi hakuna haja ya kuyafanyia uchunguzi madai ya Sithole.



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post