SUPASTAA wa muziki wa RnB wa kiwango cha dunia kutoka nchini Marekani, Chris Brown kwa mara nyingine ameingia matatani kwa kumpiga mwanamke katika makazi yake huko Los Angeles (LA).
Kwa mujibu wa mitandao ya stori za mastaa huko unyamwezini, mkali huyo wa miondoko ya Rnb anachunguzwa baada ya mrembo huyo ambaye jina lake lilibanwa, kudai kuwa jamaa alimzaba kofi mpaka wigi lake likatoka, lakini hakupata majeraha.
Katika tukio hilo, inaelezwa kwamba, kulitokea mzozo kati ya Chris na mwanamke huyo kisha kusababisha kutandikwa kofi lililokwenda shule.
Maofisa wa Polisi waliitwa katika eneo la tukio, San Fernando Valley, Kusini mwa California; mwendo wa saa moja na nusu asubuhi.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Idara ya Polisi ya Los Angeles, ripoti ya kupigwa imeripotiwa na sasa inasubiri kuamuliwa na kiongozi wa mashtaka wa mji huo endapo staa huyo atafunguliwa mashtaka.
Itakumbukwa kwamba Breezy ambaye ni mshindi wa Tuzo ya The Grammy si mara ya kwanza kutuhumiwa kuwapiga wanawake.
Mwaka 2017, mpenzi wake wa zamani ambaye ni mwanamtindo na muigizaji Karrueche Tran alipewa masharti ya kukaa naye mbali baada ya kumpiga.
Pia mwaka 2009, Breezy alishtakiwa kumpiga mpenzi wake wa wakati huo, Rihanna na kupewa adhabu ya kutoa huduma ya jamii kwa miaka mitano.
Stori: Sifael Paul
Post a Comment