Dar es Salaam. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amewaomba radhi wakazi wa wilaya hiyo aliowakosea katika kipindi cha utawala wake.
Kasesela ametoa kauli hiyo siku moja baada ya kutemwa kwenye nafasi hiyo kutokana na uteuzi wa wakuu wa Wilaya uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan jana, Jumamosi Juni 19, 2021.
Mwanasiasa huyo ameomba radhi wakazi hao kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram ambapo ameandika ifuatavyo; "Wana-Iringa imekuwa furaha kufanya kazi na nyie mmejenga mahusiano makubwa na udugu nitaendelea kuwakumbuka sana,
"Nawashukuru viongozi wangu niombe radhi kwa wale niliowakosea haikuwa kwa nia mbaya, upendo ndio msingi wa maisha"amesema
Katika uteuzi alioufanya Rais Samia, Mohamed Hassan Moyo ndiye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa akirithi mikoba iliyoachwa na Kasesela.
Kasesela ni miongoni mwa viongozi waliokuwa wanashutumiwa na wananchi kutumia vibaya madaraka ikiwemo kutoa maneno ya kejeli hasa kwa wapinzani.
Post a Comment