Ni Kweli Hakuna Mwanaume wa Peke Yako?


 TUNA kila sababu ya kuendelea kumshukuru Mungu. Ni Jumatatu nyingine tunakutana kwenye eneo letu hili maridhawa kabisa la kuzungumza yahusuyo maisha ya uhusiano. Kama uko kwenye uhusiano mzuri kwa sasa, endelea kushikilia mahali ulipo.

 

Kama upo kwenye changamoto yoyote ile, usihofu. Ndivyo maisha yalivyo. Huwezi kuwa kwenye furaha siku zote. Zipo nyakati ngumu, zipo pia nyakati za kufurahia maisha. Ukiwa kwenye furaha, si rahisi sana kujua kama kuna mwenzako yupo kwenye maumivu.


Pakua App MPYA ya 'EDUSPORTSTZ NEWS-(Lite Version)' Uweze kufurahia Habari zote za Mapenzi; Udaku, Ajira na Michezo kila siku Ipo Google Playstore, Kwa Ku BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD Kwenye Simu yako Utasoma habari zote hata kama hauna MB

 

Tujifunze kuzitambua nyakati hizi. Tujue kwamba maisha ndivyo yalivyo. Tusilie sana hadi tukakufuru. Kikubwa ni kuamini tu, ipo siku utafurahi, haijalishi upo kwenye magumu kiasi gani.

 

Baada ya utangulizi huo mfupi, turudi kwenye mada ya leo kama inavyojieleza hapo juu. Ukizungumza na wanawake wengi wa sasa, watakuambia hii kauli ambayo imekuwa kama mazoea. Wanawake wanakujengea hoja kulingana na shuhuda mbalimbali.

 

Kila mmoja atasimulia yake. Mtu atakuambia; “Mwanaume wangu nilimpa kila kitu. lakini bado alinisaliti! “Mwanaume wangu hana maana. Badala ya kutembea na mimi, mume wangu katembea na hausigeli. Wanaume hawana maana kabisa!”

 

Ndugu zangu, hili suala siku zote lina sura mbili. Kuna upande wa wanawake wenyewe, lakini pia upande wa wanaume husika. Tukianza na wanawake, ninyi wenyewe mnatakiwa kulikataa jambo hili katika akili zenu na kutokulipigia kabisa chapuo na kulifanya kama vile kampeni yenu.

 

Mwanamke unachotakiwa kufanya, ni kutimiza majukumu yako kwa mwenza wako ambaye tayari umejiridhisha na kuona kwamba si mtu wa kurukaruka. Si mtu mwenye tabia za hovyohovyo. Basi ukishampata, wewe timiza wajibu wako kwake.

 

Mwanaume anayejitambua atakuwa wako wa peke yako kama na wewe utajitoa kutimiza majukumu yako. Kweli utamsaidia. Wewe ndiye msaidizi, kwa nini sasa uache kumsaidia? Mfanye mwanaume wako awe rafiki, umjue anapenda nini na nini hapendi.

 

Ujue kipi kinamfurahisha kutoka kwako kwa jinsi ya tofauti na yake. Ukishakijua, basi wewe mfurahishe kwelikweli. Hatakuwa na muda wa kwenda nje kama anaipata furaha nzuri kutoka kwa mtu wake. Atakuheshimu.

 

Kikubwa pia wewe amini kwamba, hana makandokando. Kama anayo, anaweza kuyaacha kutokana na jinsi ambavyo wewe unamjali, unamthamini na kumheshimu. Lakini kwa upande wa wanaume, pia mnatakiwa kujitambua.

 

Mwanaume ujitambue wewe ni nani na nafasi yako katika familia. Kuwa mtu ambaye unajiheshimu, ambaye unatambua kwamba unapaswa kuwa na mtu mmoja maishani, ambaye mtashea furaha na shida zenu.

 

Tamaa za kijinga wakati mwingine, ni vyema kusema na moyo wako. Kwani inashindikana vipi kuwa na mtu mmoja na maisha yakaendelea? Acheni ubabaifu. Kwani ni kitu gani cha tofauti ambacho unakipata huko nje ambacho mke wako hana?

 

Ukifuatilia kwa makini hili, utagundua kwamba hakuna zaidi ya tamaa. Wanaume mnatakiwa kubadilika. Dunia ya sasa, endapo utakuwa bize na kazi na linapokuja suala la faragha, basi mkeo yupo utamkuta nyumbani jioni.

 

Jiheshimu ili pia na wewe uheshimike. Ukionesha heshima kwa mkeo, hata yeye pia atajisikia faraja na kukupa upendo unaostahili. Wanaume muache matamanio ya kijinga, ukiona kuna mahali labda pengine mke wako hatimizi wajibu wake, mueleze ili ajirekebishe.

 

Hakuna aliyezaliwa anajua kila kitu. Mnapokutana wawili, kila mmoja anamfundisha mwenzake. Mwisho wa siku mtakuwa na furaha nyote na maisha yenu hayatakuwa na makandokando. Usijione mjanja kufanya kwa siri kwani ipo siku yanaweza kujulikana na ikawa fedheha kwako.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post