KWENYE ulimwengu wa mapenzi kuna baadhi ya watu wamewahi kupagawa. Wengine wakakatisha uhai wao au wa wenza wao au wote. Wengine wakaichukia kabisa sanaa ya mapenzi baada ya kupitia kwenye mateso na huzuni iliyosababishwa na mapenzi kama kukataliwa na kufanyiwa unyama wa moyoni. Asikudanganye mtu, mapenzi yanatesa, hivyo ukiona mtu analia kwa ajili ya mapenzi, basi usimcheke!
Kwa waathirika wa maumivu ya mapenzi, huwa sawa na wafiwa waliopoteza wawapendao. Hupitia kipindi cha maombolezo sawa na wale waliokuwa kwenye msiba na wapo wanaohitimisha maombolezo hayo, lakini wengine huchukua muda mrefu kufikia hitimisho hilo.
Hakuna kipindi kigumu kwenye mapenzi kama kile unapoachwa au kuachana na mwenzako, kwani unaweza kuhisi kama dunia imefika mwisho. Hasa pale unapoumizwa na yule uliyempenda kwa moyo wako wote.
Kwa kawaida moyo unapopenda kwa dhati, huwa na kawaida ya kujisahau. Hufikirii kwamba huyo uliyempenda anaweza kukufanyia kitu kibaya. Unampa moyo wako wote. Unapopenda sana, ndivyo utakavyoumia sana itakapotokea amekubadilikia.
Ndiyo maana siku zote unapopenda, ni muhimu kubakisha sehemu kidogo katika moyo wake kwa matukio ya kuachwa, kuumizwa au kukutana na usiyotarajia.
Kwa mtu yeyote ambaye amewahi kupenda kwa dhati, na baadaye akaja kuumizwa, atakuwa shahidi kwamba hakuna kitu kinachoumiza moyo kama maumivu ya mapenzi. Kwani kuna baadhi ya watu huwa hawajali kuhusu mioyo ya wenzao, anakufanyia jambo kwa makusudi bila kujua madhara atakayokusababishia.
Wapo ambao kwa sababu ya kushindwa kuyahimili maumivu ya mapenzi, hujikuta wakiyakatisha maisha yao.
Wengine hujikuta wakipoteza kila kitu maishani kwa sababu ya mapenzi. Unakuta mwingine hata kama alikuwa na kazi nzuri, inapotokea amekumbwa na dhoruba ya mapenzi, hawezi tena kufanya kazi kwa ufanisi, muda wote machozi, muda wote anahuzunika, matokeo yake, anashindwa kuendelea na kazi.
Wengine hujikuta wakiingia kwenye ulevi wa kupindukia, ikiwa ni juhudi za kujaribu kutafuta sehemu ya kupunguza machungu. Matokeo yake, wanazalisha matatizo mengine makubwa zaidi na pengine mwisho wao unakuwa ni mauti.
Ni kweli mapenzi yanatesa, lakini inapotokea umeumizwa na mtu uliyempenda kwa moyo wako wote, haimaanishi kwamba huo ndiyo mwisho wa maisha yako. Unaweza kusimama tena, inawezekana kabisa.
Kitu ambacho watu wengi huwa hawakikubali kirahisi, ni ukweli kwamba mapenzi yanatesa. Wengine hujitahidi kuficha maumivu wakijidai kwamba ni jasiri na hawajaumia popote na kujidai wanaendelea na maisha yao, wakati moyoni wanateketea.
Matokeo yake, unalimbikiza tatizo ndani ya moyo wako ambalo litaendelea kukusumbua kwa muda mrefu mpaka utakapotambua namna ya kulishughulikia.
Pale inapotokea kwamba mwenzako unayempenda, ambaye mlikuwa na ndoto nyingi za pamoja, mliyejadili na kupanga mambo mengi pamoja, amekutendea unyama wa moyoni, ameuvunja moyo wako na kukusababishia maumivu makali moyoni, kwanza jipatie muda wa kuwa peke yako kwa muda.
Pale unapopata nafasi ya kuwa peke yako, zungumza na moyo wako, kama unadhani kulia kunaweza kupunguza uchungu moyoni mwako, lia sana hadi moyo wako utulie. Jiulize mara kadhaa kuhusu uzito wa kosa alilokufanyia, jiulize mwenyewe, je, baada ya yote hayo unahitaji kuendelea kuwa naye au huwezi tena kuendelea.
Wanachokosea wengi, wakishakumbwa na kimbunga cha mapenzi, badala ya kupata muda wa kutosha wa kuwa peke yao, wanaanza kuwasimulia marafiki au ndugu wakitaka washauriwe nini cha kufanya.
Endapo moyo wako unakwambia kwamba japokuwa amekukosea, bado unampenda kwa dhati na unamhitaji, fanya kile moyo unachoona kinafaa. Na endapo moyo wako unaona umefika mwisho kabisa na huwezi kuendelea, usikilize pia moyo wako.
Ni hayo kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mara nyingine bomba.
Post a Comment