Anachopaswa kufanya mke pindi anapoona Mumewe Amepunguza Mapenzi


 Katika ndoa za siku hizi mashauri mengi yanayopelekwa kwenye mabaraza ya usuluhishi yanahusu malalamiko ya wanawake kwa waume zao. Mara nyingi wanalalamika kuwa waume wamepunguza upendo na hata mapenzi kwao.

Katika makala fulani nilieleza malalamiko ya mwanamke aliyesema “Ingawa inaonekana kama ndoto, ukweli ni kwamba ndoa yangu imo katika matatizo. Mume wangu ananijali na kunifikiria wala hatuna mizozo au ugomvi. Lakini uhusiano wetu umekuwa tofauti na unaonekana umekuwa wa mbali sana. Tumekuwa kama watu wawili tunaochangia chumba na wala sio mapenzi ya mume na mke.

Ingawa hali hii haifurahishi wala haipendezi inatokea sana katika ndoa za siku hizi. Wewe kama mke unapohisi kama penzi la mumeo linaanza kupoa, kwanza fanya uchunguzi ili kuthibitisha kama ni kweli na utambue sababu. Kama ninyi ni wanandoa wapya, huenda ndoa yenu imekosa mahaba huenda mumeo ambaye mwaka mmoja uliopita alikuwa akipendezwa na kuridhika na kila alichofanya, ghafla amebadilika. Anakucharukia hata kwa jambo dogo kama chumvi kupungua kwenye mchuzi. Asubuhi alikuwa hawezi kukurupuka akatoka siku hizi anaondoka bila kukupatia busu la kukuaga na hasemi tena “kwa heri mpenzi!

Matukio kama haya hushangaza, lakini pia yanaweza kuwa sio ya ajabu kama mtu anavyoweza kuyafikiria. Wajibu wa ndoa haushii tu katika mawasiliano, mahaba na maliwazo ya kukumbatiana, bali ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa mahitaji muhimu ya maisha ambayo ni chakula, mavazi na malazi. Hivyo, hata mume mwenye mapenzi sana kwa mkewe anaweza kuonekana kama amepunguza mapenzi kutokana na mihangaiko ya kupata mahitaji hayo. Anastahili kusamehewa iwapo zitatokea nyakati ambazo atajikuta akili zake zimetekwa na kazi yake.

Hata hivyo, kitendo cha kumuweka mkewe kando kimapenzi kiwe kikitokea kwa nadra sana na wala usiwe ndiyo mwenendo wa maisha yao ya ndoa. Mume asiwe akitumia muda wake mwingi ofisini kwake. Wala anapotoka kazini asiwe katika shughuli zisizomjumuisha mkewe. Anapokuwa nyumbani na mkewe aepuke tabia ya kuwa kimya au kukwepa nafasi ya kuwa wawili peke yao. Vitendo hivi huweza kusabisha ashiki ya tendo la ndoa kuwa chini sana.

Hata katika hali hii bado mwanamke anapaswa kujiuliza kama mumewe anafanya kusudi au ni kutokana na hamasa ya maendeleo. Kwani mwanaume ana homoni ambayo wakati mwingine humfanya awe na shauku na shinikizo kubwa la kutaka maisha bora zaidi kwa familia. Hususan, wanapopata watoto kutamani kuwa baba mzuri kwa wanawe. Shinikizo huwa kubwa sana hata mawazo ya mabembelezo na mahaba kwa wake zao yanayumba sana.

Hali ya utata sana kwa mwanamume hutokea anapokuwa katika umri wa katikati. Katika kipindi hiki mara nyingi huwa anajiuliza katika nafsi yake kama kuna maendeleo au mafanikio yoyote aliyoyafikia katika maisha yake. Katika kipindi hiki hata mume mwenye mapenzi sana kwa mkewe anaweza kuzungwa na wasiwasi, hofu na mashaka.

Mke ni lazima atambue kuwa mashauri ya mapenzi ya mume kuonekana yamepungua hayataweza kutatuliwa na wazazi, ndugu, marafiki au mabaraza ya usuluhishi ya ndoa. Utafiti umeonyesha kuwa asilimia 25-35 ya wanawake wanapoona dalili za kupungua kwa mapenzi kutoka kwa waume zao huamua kuondoka na ndoa kuvunjika. Lakini kwa mwanamke ambaye bado anampenda mumewe na anayetaka ndoa yao iendelee, njia sahihi zaidi ni kuchunguza na kuzitambua sababu zinazofanya ndoa yao ionekane kama haikidhi matarajio. Badala ya mwanamke kujiuliza swali moja tu. Kwa nini mume wangu hanipendi kama ilivyokuwa zamani?” Pia ajiulize swali hili jingine “Je, mimi ninapenda na nina hali itayonifanya nistahili kupendwa kama ilivyokuwa zamani.”

Swali hili sio rahisi kwa mwanamke kulijibu. Tutatoa maswali mengine yatakayomsaidia kuhakikisha ndoa yake haiyumbi.

•Je, vipaumbele na msimamo wake katika ndoa uko sahihi?

Mwanasaikolojia mmoja aliwahi kusema, Ndoa thabiti hujengwa kwa kutambua ni kitu gani kitangulizwe mwanzo. Ushirikiano kati ya mume na mke ni wa kwanza wala usitanguliwe na kitu kingine chochote.

•Je, kuna shughuli za kijamii ambazo wewe huwa anaweza kuzishiriki hata asipokuwa na mumeo?

Bwana mmoja aliye na mke asiyefanya kazi alilalamika kwa kusema “Mimi nashinda kazini kutwa nikifanya kazi hadi ninaporudi nyumbani huwa niko hoi natamani kupumzika tu. Lakini, mke wangu huwa amekaa nyumbani kutwa akitumaini nikirudi nitamchangamsha kwa kumtoa nje. Nikishindwa kwa kuwa nimechoka hufikiria kuwa simpendi au penzi langu limepungua” ili kuepuka tatizo hili ni vyema mwanamke abuni kitu cha kufanya asipooze bure. Anaweza kufanya shughuli kama vile kulima bustani, kufuga kuku, kusuka vikapu na nyinginezo. Aidha, anaweza kujiunga na vikundi kama Vicoba, Saccos na vya maendeleo ya kina mama vitakavyomfanya akutane na wenzake na kuchangamka. Jioni wanapokutana na mumewe nyumbani hakuna atakayekuwa amechoshwa na upweke.

•Je, unakabiliana na changamoto badala ya kuzikwepa au kuzipuuza?

Watu wawili wanapoamua kuishi pamoja tofauti ndogo ndogo ni lazima ziwe zikitokea. Iwapo mwanamke atakuwa na tabia ya kuzifunikafunika bila kuzidhihirisha na kuzitafutia sululu zinaweza kukomaa zikawa kama sumu. Wanasaikolojia husema mitafaruku na tofauti katika ndoa zineposhughulikiwa kwa maneno mazuri huimarisha mshikamano. Mtaalamu mmoja alimwambia mwanamke fulani kuwa ikiwa wewe na mumeo hamjawahi kutofautiana hadi mkapigiana kelele ni hatari sana. Inawezekana kuna hasira iliyofichika ambayo siku ikitoka hamtaweza kuisuluhisha.

• Je matarajio kwa mumeo yana busara

Kuna baadhi ya wanawake huwakomalia waume zao wawapatie vitu au kuwatendea mambo yaliyo nje ya uwezo wao hadi huwafanya wawe na maisha ya huzuni. Aidha wako ambao huwatumia waume zao katika shughuli za familia kiasi kikubwa hadi kuathiri kazi zao. Yote haya huweza kumkwaza mume hadi akachanganyikiwa na kumfanya aonekane kama mapenzi yake kwako yamepungua.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post