UMEKINAI UHUSIANO WAKO? PATA ELIMU HAPA!


UKIPATA bahati ya kuzungumza na watu wengi waliopo kwenye ndoa au uhusiano wa kimapenzi au waliopo kwenye uchumba, wengi watakwambia wamekinai uhusiano wao na kilichobaki ni uvumilivu na mazoea tu.
Mtu yupo na mwenza wake ilimradi tu kwa sababu yupo na hana namna nyingine. Hamjali mwenza wake, hana tena hisia naye, kilichobaki ni zile hadithi za kuwahadithia wenzake kwamba na mimi nina mke au mume. Mimi nipo kwenye uhusiano na fulani.
Tatizo hili linawatesa sana walioko kwenye ndoa. Kwa uzoefu nilionao, kupitia maoni ninayoyapata hapa kutoka kwa wasomaji mbalimbali, ninapata picha kwamba mambo sasa hivi yanakwenda ‘shaghalabagala’.
Mwanaume hana hamu na mkewe na mke naye hivyohivyo, hana hamu na mumewe. Hii ndiyo tunasema watu wamechokana, watu wamekinaiyana. Yale mapenzi waliyokuwa wanapeana wakati wanaanza uhusiano au miaka miwili-mitatu ya awali, si ya sasa.
Inafika mahali, mke anakwambia amechoka hivyo anaona ni bora kuanzisha uhusiano usio rasmi ilimradi tu kuipata furaha ya moyo. Anaamini kwamba akiwa na ‘kakijana kake’ huko pembeni, katamfanya afurahie maisha.
Yuko radhi kakijana hako akagharamie mahitaji yote muhimu ili tu kampe hitaji la moyo wake. Halafu sasa ukichunguza kwa undani, si kwamba mume wake hawezi kumtimizia mahitaji, anaweza! Basi tu mazoea yanawatafuna.
Mume naye anamchukulia poa mkewe, anatafuta ‘kabinti kake’ huko nje, basi anainjoi nako maisha. Nyumbani watakutana jioni, kila mmoja anafanya mambo yake kwa siri na anajiona mjanja kwamba mwenzake hajui.
Mwisho wa siku wote wanakuwa wanaishi tu ilimradi maisha yaende. Upendo ndani ya nyumba unakuwa haupo tena, hii ndugu zangu ni hatari sana kwa sababu kuishi na mke au mume kwa mazoea ya aina hii ni sawa na kuishi na mtoto wa shangazi au mjomba wako ndani ya nyumba.
Itafika mahali maana halisi ya ninyi kuwa wanandoa inakuwa haipo. Hivyo basi, ni vyema kupata elimu juu ya hili ili kama imekutokea au haijakutokea bado, ujue namna ya kujihadhari na tatizo hili ambalo linawatafuna wengi.
Tatizo hili husababishwa na mengi; yawezekana ikawa ni mabadiliko ya tabia, yawezekana ikawa pia ni hulka au utashi wa mtu. Yawezekana ikawa ni mapenzi ambayo tangu awali hakuwa nayo kwako. Staili hii ya uhusiano ni mbaya zaidi.
Kitendo cha mtu kuingia kwenye uhusiano na wewe halafu hakupendi kwa dhati, ni hatari zaidi. Matokeo yake yanagharimu maisha yenu yote. Kama ni mabadiliko ya tabia, ni suala la kujitathmini na kuona kwamba unafanya makosa, hivyo rudisha thamani kwa mke au mumeo.
Kama ni suala la tabia, basi badilika. Achana kabisa na tabia ambayo inahatarisha uhusiano wenu au afya zenu. Cha muhimu zaidi, kama ndiyo kwanza unaingia kwenye uhusiano, basi hakikisha unaingia na mtu ambaye kweli unampenda kutoka moyoni.
Usiingie kwenye uhusiano na mtu kwa tamaa ya fedha au mwili. Ishi na mtu ambaye kweli utampenda na hata ikitokea siku umeanguka bahati mbaya, basi haraka sana rudi kwenye mstari na umuheshimu mtu wako.
Ukiwa umefikia hatua ya kukinai, jiulize uliyenaye si mtu uliyempenda tangu zamani? Kama jibu ni ndiyo, jiulize ni kwa nini ukinai sasa? Tafakari na uchukue hatua haraka za kurejesha uhusiano wako uwe hai. Mheshimu mtu wako, mpe thamani ya juu kuliko yeyote yule. Mthamini, muishi pamoja mpaka pale kifo kitakapowatenganisha!


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post