KUOLEWA ni heshima kwa mwanamke. Heshima hiyo inaenda mbali zaidi hadi kuwagusa wazazi wa binti ambaye ataolewa. Wazazi wanatembea kifua mbele pindi binti yao anapoolewa, tena wanafurahia zaidi binti huyo anapoolewa akiwa angali bado hajazaa.
Wanamshukuru Mungu kwa binti yao kujitunza. Wanamshukuru binti kwa kuwapa heshima katika familia yao na ndiyo maana siku ya sherehe ya kuagwa (send off) wazazi wanafurahi sana kuagana na binti yao kwa heshima.
Hali hiyo huwa inaleta shauku kubwa kwa warembo wengi kutamani kuingia kwenye ndoa. Wengi wanaguswa na rekodi za wanawake wenzao ambao wamejitunza na hatimaye kuwaletea heshima wazazi wao.
Kinyume chake, wengi wamejikuta wakijilaumu kwa kushindwa kuleta heshima katika familia zao. Binti umri unaenda, anatamani kuingia kwenye ndoa lakini hapati wa kumuoa. Au mwingine inatokea, anatamani kuolewa lakini anaishia kupigwa mimba na kuachwa.
Badala ya kuleta heshima, analeta aibu katika familia yake kutokana na mila na desturi zetu kumtaka binti azae pale tu atakapokuwa ameolewa. Azae pale atakapokuwa kwa mumewe na si vinginevyo. Inapotokea bahati mbaya basi ni mara moja na si kuzaa na kuzaa watoto kibao.
Pamoja na kuwa ndoa ni mpango wa Mungu lakini hivi umeshawahi kujiuliza wanaolewa wanakuwa na sifa gani? Kwa nini wanaume wanavutiwa nao? Wanakuwa na kitu gani cha ziada ambacho wanawake wengine hawana? Leo nitakuambia!
Jamani, sifa ya kwanza ambayo mwanamke anapaswa kuwa nayo ni ile hulka ya kuwa mke. Wanaume wengi huwa wanapenda kuishi na mwanamke ambaye ana ile sifa ya kuwa mke. Ninaposema sifa ya kuwa mke naamisha mwanamke ambaye atakuwa tayari kumlea mume na hata watoto.
Mwanamke ambaye atakuwa msaada kwa mwanaume wake pindi atakapokuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo za maisha pamoja na maradhi. Mwanamke ambaye atajua thamani ya mume, ambaye atajua nini maana ya heshima kwa mumewe.
Mwanamke ambaye atamudu misukosuko ya maisha ikiwemo kufilisika, kuachishwa kazi na mengine magumu yanayofanana na hayo. Mwanamke ataka-yevaa sifa ya kuwa mke kwa maana ya kumhudumia mumewe pindi atakaporudi amechoka kutoka kazini.
Wanaoolewa ni wale pia ambao wanajua kushuka pindi wanapoona kumetokea kutoelewana. Wanawake wale ambao wanajua kumtoa uchovu wa maisha mwanaume. Mwanamke ambaye hasababishi makelele ya mara kwa mara kwenye ngoma za masikio ya mwanaume.
Mwanamke ambaye hana gubu. Mwanamke atakayeelewa kwamba muunganiko wa ndoa una pande mbili hivyo kuwajali ndugu wa pande zote mbili, ndugu zake na ndugu wa upande wa mumewe. Mwanamke ambaye atakuwa na muonekano wa mke kwa maana ya mavazi na hata mazungumzo.
Wanaoolewa jamani wanakuwa na sifa ya uvumilivu. Wanakuwa na hofu ya Mungu. Mwanamke mwenye hofu ya Mungu, anamuomba yeye ampatie mwanaume mcha Mungu na kweli inatokea. Kuna siri kubwa sana katika kumuomba Mungu ambayo wengi wetu hatuijui lakini ni vyema kumtanguliza yeye katika kila jambo.
Ukiwa na sifa hizo, hata kama hautakuwa na muonekano wa kimisi au kuwa na shepu bomba kama wanavyosema vijana wa kisasa, utaolewa tu na hizo ndizo sifa za mwanamke anayetaka kuolewa!
Post a Comment