Nani anaikumbuka ladha ya mpenzi wake ambaye walishaachana mwaka mmoja uliopita? Tuache mwaka, ikiwa ulikuwa na mtu kisha ukakutana naye kimapenzi wiki iliyopita na baada ya hapo hamjakutana tena, ni ladha ipi unaikumbuka?
Kuna faida gani ya kusema au kujulikana ulishatoka kimapenzi na wapenzi wengi ambao ladha zao hata huikumbuki? Muda unapita mguso wao ndani yako umeshatoweka kwenye hisia zako, hakuna faida yoyote unayokuwa nayo isipokuwa kumbukumbu tu zenye ujinga ndani yake; “pale tayari nilishapita.”
Huo ndiyo utaahira wa ngo-no. Kinachobeba ubongo ni maneno hayo matatu; “pale tayari nimeshapita.” Si zaidi ya hapo. Unakuta mke wa mtu naye anatambua kuwa mwanaume mbele yake anataka ajiandikie kwenye ubongo wake; “pale tayari nilishapita.” Anakubali kuandikwa kwenye orodha ya waaliopitiwa.
Ng-ono achana nayo, inaajiri wafanyakazi na inafukuza watu kazi. Inatengeneza maelewano kati ya mwajiri na mwajiriwa, vilevile inawagombanisha. Ngo-no inadumisha amani ya nyumba, vilevile inavuruga.
Watu wanaitumia ng-ono kama kisasi. Mtu anaamua kutembea na mke wa mwenzake ili tu kumkomoa. Mwanamke anayetumika kama kisasi, anakuwa anafahamu uhusiano kati ya mume wake na huyo ambaye anafanya naye ngon-o. Usiseme mapenzi, maana mapenzi ni yenye kufuata utaratibu.
Mwanamke kwa visa tu vya kike, anasema mwenzake anaringa. Anaamua kutembea na mume wa mwenzake ili kumkomoa. Yanaendelea kuwepo, yatazidi kuwepo kwa sababu ngo-no ipo hai. Vile binadamu wapo na mapenzi yapo, ngo=no pia itaendelea kuwepo.
Utaahira wa mapenzi; mtu akijua umetembea na mwenzi wake yupo tayari kukutoa uhai. Anaona umefaidi sana matunda yake. Anajiona umemdhalilisha kupita mfano. Anajihisi kuonekana dhaifu si kawaida.
Jiulize; mtu katembea na mume au mkeo, baada ya kuwa ameshamaliza tendo, amepata nini? Ukimkagua maeneo yote ya mwili hakuna alama ambayo imeongezeka yenye kumtambulisha kuwa amewahi kutoka kimapenzi na mwenzi wako. Basi tu ujinga wa ngo-no na utaahira wake.
Baada ya ngo-no kila aliyeitenda hubaki vilevile. Sanasana kama umeingia njia yenye maradhi ndiyo hapo utayapata. Na ukishayapata maradhi huwezi kujisifu kutokana na mtu ambaye amekuambukiza, badala yake ni kilio tu.
Huwezi kukaa mahali na kusema: “Mimi ukimwi wangu ni mzuri maana nimeambukizwa na malkia.” Ukishaupata ni majuto kwa kwenda mbele hata kama umeupata kutoka kwa kiongozi mkubwa wa nchi yako au tajiri mkubwa.
Uendawazimu wa ng-ono; unakuwa na mtu ambaye huna uhuru wa kumtambulisha popote kuwa ni mwenzi wako. Mnakutana kwa kificho na kumalizana kwa kificho. Raha zenu mnafanyia gizani na inabaki siri ya wawili. Unajiumiza tu kifua kutunza yasiyo na maana.
Yupo ambaye atakwambia mapenzi ya wizi ni matamu. Wamekuwepo wanawake wenye kutamka kuwa waume za watu ni watamu. Vilevile wapo wanaume wenye kusifu kuwa wake za watu ni asali.
Wewe unaamini hayo? Kipi hasa cha kukupa hoja kwamba mke wa mtu ni asali au mume wa mtu ni mtamu? Ukifuatilia ndani kwa ndani unakuta wapo watu ambao ubongo wao umeshalemaa na mapenzi ya wizi.
Ukishalemazwa na mapenzi yasiyo na uhuru lazima useme mke wa mtu ni asali. Ukishaathirika na mapenzi yasiyo na uhakika wa kesho, utathubutu kusema hayo kuwa mume wa mtu ni mtamu.
Anayependa uhuru, asiyetaka kunyata anapoyaendea mapenzi, asiyehitaji presha katika mzunguko wake wa kimaisha, hawezi kusema mke wa mtu mtamu au mume wa mtu sukari. Maana anajua uhondo wa kuwa na wake ambaye kuwa naye roho haimdundi au kuwa ana wasiwasi wa kujulikana au kufumwa.
Inahitaji ubongo uliofeli kuendekeza mapenzi ya wizi. Mapenzi ya kingo-nong-ono. Mapenzi yasiyo na heshima. Wewe ukijiona ni mtu wa heshima, kama unahusika na mapenzi ya wizi maana yake hujiheshimu. Wewe ni mwizi.
Ushetani wa ngo-no; mtu akizowea mapenzi ya wizi, ingia kwenye maisha yake ujifanye unambadilisha awe mke au mume. Mchana atakuzimia simu ili apate uhuru wa kukusaliti.
Aliyezoea mapenzi ya usaliti ana nyota ya popo; usiku mtalala wote kitandani lakini yeye usingizi haupandi ng'o! Wewe ukishapitiwa na usingizi, yeye atanyata kwenda kwa jirani kuchepuka, ikiwezekana hata kwa hausegirl au houseboy.
Ukishambaini anafanya hivyo usiumie sana eti kuna vitu humtimizii, hapana asikudanganye mtu. Unatakiwa kutambua kuwa mwezio ameshalemazwa na mapenzi ya wizi, kwa hiyo bila kukuchepuka akaibe kidogo hana amani.
Hapo sasa ni jukumu lako kumsahihisha asirudie tena au kumtimulia mbali kwenye maisha yako. Maana mwisho wa siku lazima ufanye uamuzi ambao utakupa furaha na siyo kukuumiza.
Ukitaka kujua kuwa mapenzi ya wizi ni tabia yake na ameshalemaa, wewe mwache halafu upate mpenzi mwingine kisha naye apate wake. Baadaye utajikuta ananyata kuja kukuiba wewe.
Utajiuliza: “Kama ulikuwa unanipenda si ungebaki na mimi tu na kuacha kuchepuka?” Siyo yeye ni tabia yake. N-gono na ushetani wake, ukishageuka wa kuiba unakuwa mwizi tu.
Kichaa cha ngo-no kikishampanda mtu, anaweza kugoma kumpa penzi mkewe hata abembelezwe vipi, halafu anatoka kwenda kujidai na changudoa, mapenzi ya wima, yasiyo na maandalizi wala uhuru.
Hicho kichaa cha ngo-no kikishamnasa mwanamke, mumewe anaweza kumpa kila kitu lakini akimpa kisogo tu, ananyata kwenda kwa muuza genge ambaye haendi naye mbali, palepale gengeni, juu ya viroba vya viazi na vitunguu shughuli inamalizika.
Nyumbani kwake kuna mazingira bora kabisa ya kufanyia tendo. Anaye wake tena ana uhuru naye wa kupitiliza. Chumba kizuri, kitanda murua na mwenzi wake humpa huduma bora yenye kumtosheleza. Ila ndiyo tena utaahira wa ng-ono unapochukua nafasi.
Mungu anawasaidia wengi wasiyajue mengi ya sirini ili waishi miaka mingi. Maana idadi ya wanaume wenye kujinyonga ingekuwa janga la dunia kama wangekuwa wanashuhudia jinsi wake zao wanavyofanywa gizani, vichakani au kwenye nyumba za kulala wageni na wanaume ambao hawalingani nao hadhi.
Wanawake wangeshuhudia jinsi ambavyo waume zao wanapelekeshwa na mashangingi wapenda fedha, halafu mwanaume huyohuyo akirudi nyumbani anavyokuwa mbabe, vifo vya wanawake vingekuwa vingi, ama kwa kujiua au kuuana na wanawake wenzao.
Ngon-o inavuruga kichwa; anamwacha mkewe nyumbani ambaye anamheshimu na kumjali, kisha anakwenda kwa mwanamke wa nje ambaye anachohitaji ni pesa tu. Siku akiwa hana fedha anakimbizwa kama mwizi.
Kichwa kikishavurugwa na ngon-o; mwanamke anaweza kushuhudia mume wake anamlilia machozi ili ampe mapenzi lakini akamnyima, kisha naye anatuma SMS za vilio, anaomba huduma hiyohiyo kwa mwanaume wake mhuni-mhuni mwenye wapenzi wengi.
Mke wa mtu anajua kabisa kuwa huyo anayempenda ni kicheche, ana wanawake wengi. Ukiwa naye inabidi usubiri mapenzi ya mgawo, maana mpaka azunguke wanawake wake wote ndiyo akurudie tayari imekatika miezi sita. Basi mke wa mtu kilio, anamlilia kicheche.
Eti analia ananyimwa haki yake ya penzi la kuchepuka kwa miezi sita. Halafu akishamaliza kumlilia kicheche wake, anakutana na mume wake naye anaomba huduma lakini anamyima. Swali; kama ulikuwa hujisikii kumpa mapenzi mumeo ulikubali kuolewa naye kwa nini?
Wagonjwa wa kichaa cha ng-ono kama wangekuwa wanapelekwa hospitali, inawezekana mitaani pangekuwa peupe, maana ni wengi mno. Asikwambie mtu, kichaa cha ngo-no kikimkamata mtu, anakuwa na akili za hovyo kuliko wagonjwa waliolazwa Mirembe, Dodoma.
Jitahidi ukae sana na Mungu kichaa cha ngo-no kisikupande kichwani. Pambana sana kujistahi kichaa cha ngo-no kisikupelekeshe, maana kikikuvaa hata uwe mtu mwenye heshima na nguvu kiasi gani, kitakudondosha tu dhambini. Chenyewe hakitumii nguvu, msuli mdogo mwenyewe unaelekea.
Utashangaa tu unavua suti na kubaki mtupu mbele ya ‘kabinti kadogo’. Utaanza naye safari kama vile unalingana naye. Ni sawa na mama kung’ang’ana na vijana wadogo, shida si wao ni kile kichaa.
Kuna yule bosi flani. Aliyekuwa akizungumza watu kimya, kumbe naye aliwahi kupandwa na kichaa cha ngo-no nyumbani kwake, akaenda kumkalia uchi housegirl wake, haikuishia hapo akalala naye. Mambo yakawa hadharani baada ya binti kupata mimba kisha akazaa. Housegirl akadai matunzo ya mtoto. Bosi wa**** aibu tupu!
Usimuone yeye ndiye mgonjwa kihivyo wa kichaa cha ngo=no, hapana! Kichaa cha ngo-no kilimdaka mtu wa Mungu Daud, akamtamani Bathsheba ambaye alikuwa mke wa askari wake anayeitwa Uriah. Daud akafanya ng-ono na Bathsheba kisha akaamuru Uriah auawe. Tiba ya kichaa cha ngo-no ni nusura tu ya Mungu.
Kuna watu hufunga safari pamoja mpaka hotelini. Tena wanaweza kuingia ndani wakiwa wameshikana mikono, kukumbatia na hata kupigana mabusu. Ajabu ni kuwa wakishamaliza haja zao, kile kichaa chao cha ngo-no kinawapotea kwa muda. Wanaona aibu kutoka pamoja, wanaambiana “anza wewe kutoka.” Kichaa cha ngo-no hukata mshipa wa aibu.
Mwanaume kwenda kutembea na ndugu wa mkewe au hata mama mkwe wake, hicho kama siyo kichaa cha ngo-no ni nini? Mwanamke kutoka na shemeji zake au baba mkwe wake, hicho ni kiwango cha juu kabisa cha maradhi ya kichaa cha ngo-no.
Kwa kawaida kichaa cha ngon-o hufanya kazi yake iliyodhamiria. Kikikupanda kisha kikakutuma uwe unatongoza na kutembea na marafiki wa mkeo, hata ukiwa unaumwa upo kitandani hujigeuzi, wakija kukuona kwa heshima ya urafiki wao na mkeo, wewe utatumia kila hila mpaka uombe namba ya simu.
Kichaa cha ngo-no kikimtuma mke wa mtu kuwamaliza marafiki wa mume wake, atakuwa kimbelembele kuwajali marafiki zake utafikiri mtu kweli. Ukarimu mwingi, kumbe ule ukarimu wake tafsiri yake ni ngo-no. Ukishakijua kichaa cha ngo-no hakikusumbui.
Usiombe ukutane na mwanamke ambaye anaumwa kichaa cha ng-ono, anaweza kuzungukwa na wanaume 10 halafu wote hawajuani, kila mmoja anadhani yeye peke yake ndiye anakula. Anakuwa na mumewe ambaye anajulikana kisha marafiki tisa wa mumewe. Hao marafiki kila mmoja anaamini yeye ndiye anakula kwa siri nje ya mwenye mali. Kumbe wote pale wanakula.
Mwanamke anawapanga, stori za mezani kisha kwenye simu zinaendelea SMS: “Natamani baada ya kutoka hapa tukalale wote, sema tu jamaa hapa anabana.” Hiyo SMS anaituma kwa wanaume wote tisa kasoro mume wake, halafu kila mmoja anaamini katumiwa peke yake, kisha anajibu kwa madaha ya kuamini anapendwa: “Usijali baby, next time, you know I love you kuliko mume wako.”
SMS hiyo ikajibiwa na wanaume wote tisa, mwanamke huyo roho kwatu kwa kujiona yeye ndiye mwanamke wa shoka anayeweza kuwaendesha wanaume 10 kwa wakati mmoja bila kujuana. Anawachanganya tu kama karanga za Saida Kalori. Ile hali ya mwanamke huyo kujiona mjanja kwa ukahaba anaofanya ndiyo matokeo ya kichaa cha ngo-no kukomaa.
Kichaa cha ngo-no kinatesa vichwa jamani; unakuta mtu anajiona mjanja kuiba mke wa mwenzake. Akiwa na mke wa mtu anayemwiba, anaambiwa: “Wewe ndiye unayenipatia, mume wangu hata hanifikishi ndiyo maana nakuganda wewe.”
Kwa maneno hayo naye anaamini, anajiona kidume cha mbegu mwenye viwango vyote vya chumbani, wakati naye mke wake anaibwa na wengine, na mkewe pia anamwaga sifa kwa mchepuko wake: “Najuta hata kuolewa na yule jamaa, yaani kitandani hajiwezi kabisa.” Unasifiwa huku, unapondwa kule, hiyo ndito wajuzi wa mambo husema ngoma droo.
Kama watu wangekuwa wanasikia maneno ya kupondwa na waume au wake zao pindi wanapotoka nje ya ndoa na kukolea mapenzi ya pembeni, idadi ya watu wenye kuugua kiharusi ingekuwa kubwa kutokana na mshtuko wa moyo kutpkana na maneno yenye uchungu dhidi yao ambayo hawakuwa wakiyatarajia.
Kichaa cha ngon-o kikimkaa mwanaume anakuwa na nguvu kuliko fuso. Unakuta ana wanawake 20, wote hao wa nini? Basi tu ule ukichaa unamwambia akiwa nao wengi ndiyo ataonekana kidume.
Yupo ambaye kila anayekutana naye anataka awe mpenzi wake. Anapenda kutongoza wanawake kuliko kazi yenye kumpa riziki. Mwanamke mwenye kichaa cha ngo-no utamjua tu jinsi ambavyo anavyojirahisisha kwa wanaume. Ukiwasiliana naye tu ukichelewa kumtongoza anakutongoza yeye hata kama ni mke wa mtu.
Ukikutana na mwenye kichaa cha ngo-no muulize; haya ukishaonja ladha zote, makabila yote ya Tanzania, mataifa yote Afrika, rangi zote za duniani utakuwa umepata nini? Hatakuwa na jibu linalonyooka ila kwa ukichaa wake hudhani huo ndiyo ushujaa.
Katika ukichaa wa ngon-o, huu sasa tuuite uhayawani; mwanaume na mwanamke wanakutana kwenye mlango wa gesti au hoteli baada ya kila mmoja kumalizana na aliyemfanya afike pale. Baada ya kukutana wanatongozana kisha wanarudi tena ndani. Hapo kila mmoja anajua kuwa mwenzake ametoka kutumika lakini kichaa cha ngo-no huufubaza ule mshipa wa kinyaa.
Ukitaka kuwajua watu na ukichaa wao wa ngon-o, zungumza na wahudumu wa hoteli na gesti, vifua vyao vina mengi sana. Mwanamke (mke wa mtu) katokea Songwe amekwenda Dodoma kikazi. Mwanaume (mume wa mtu) ametokea Manyara amefika Dodoma kikazi. Mwanamke wa Songwe na mwanaume wa Manyara wanajikuta wamefikia hoteli moja.
Mwanamke na mwanaume huyo wanakutana kwenye korido, wanasalimiana kisha wanatongozana. Baadaye chumba kimoja kinalala tupu, mwanamke wa Songwe na mwanaume wa Manyara wanalala chumba kimoja. Eti tayari wamezoeana, wameshaaminiana kiasi cha kuwa wapenzi walioshibana mpaka kulala usiku mzima pamoja.
Jiulize mke wa mtu anashindwa kujiheshimu nje ya nyumbani kwake japo kwa siku moja tu! Mume wa mtu hana uwezo wa kulinda heshima ya ndoa yake japo kwa saa za usiku mmoja. Usiwarushie mawe kama adhabu ya uzinifu ilivyotamkwa kwenye Torati ya Musa, tumia muda wako kuwasikitikia, maana vichwa vyao havina udhibiti, vinapelekeshwa na kichaa cha ngo-no.
Sister na utawa wake kwenda hospitali ya uchochoroni kutoa mimba ya padri. Tazama na tukio la mwanamke mgonjwa wa akili kubeba mimba ya bishoo wa Gongo la Mboto. Ni kwamba matukio ya aina hiyo yatakoma pale Mungu atakapofanya uponyaji wa jumla juu ya kichaa cha ng-ono.
Usiombe kukutana na mwanamke mwenye kichaa chake cha ngo-no. Anaweza kumaliza wapangaji wenzake wanaume wote ikiwemo waume za watu. Ni hivyo pia kwa mwanaume kutembea na wake wa wapangaji wenzake. Kichaa cha ngon-o kina nguvu yenye kumstaajabisha hata Shetani.
Mwanamke anawapanga wanaume mtaa mzima anaoishi na haoni aibu kukatiza. Mwanaume hajaacha mwanamke katika mtaa wake, wote kawamaliza. Wanawake nao wanajua kuwa mwanaume huyo ni kumbakumba. Ajabu ya ulimwengu ni kuwa wanapeana kwa zamu bila hofu. Aliyekwambia nani kuwa mwenye kichaa cha n-gono ana hofu?
Tiba ya kichaa cha ngo-no haitapatikana leo wala kesho. Nina uhakika tiba ya Ukimwi itapatikana lakini ugonjwa wa kichaa cha ngon-o utadumu kama maradhi endelevu; Fikiria bosi anatumia kila hila kutembea na mke wa mfanyakazi wake. Wakati huohuo mke wa bosi naye analiwa na mfanyakazi wa mumewe. Hii kwa lugha ya mazingira inaitwa “kuchoma misitu ni kifo cha mazingira.”
Ukiwatembelea wajuzi wa mipasho watakwambia, ukipenda kula vya wenzako na vyako pia vitaliwa. Kwa maneno ya kanga wanasema “boflo kiboko yake chai.” Bosi na ujanja wake wote wa kujiona kidume kwa wake za wenzake, kamjamaa kasiko na mbele wala nyuma huingia nyumbani kwake na ‘kujisevia’ huduma zote kutoka kwa mkewe. Kanavaa taulo lake kisha kanaondoka kamejazwa mfuko.
Yupo ambaye ameumia hasa mwenzi wake kuchukuliwa, kwa hiyo anajua maumivu ya kusalitiwa na kuibiwa mpenzi. Badala ya kutulia mpaka apate mwingine atakayemfaa kwa hali zote, eti naye anakwenda kuiba mpenzi wa mwingine. Kaibiwa huku, naye kaenda kuiba kule. Katika lugha ya misitu, hii inaitwa “kata mti panda mti.”
Vigogo wengi hawajui tu; kuna magari wanapishana nayo barabarani yanaendeshwa na vijana wadogo yamenunuliwa na wake zao. Laiti wangepata ufunuo basi ingezuka vita kuu ya tatu ya dunia. Utashangaa vita haina msuluhishi, maana kila mmoja anakuwa vitani na wake. Ali Kiba alikosea alipoimba “Mapenzi Yana Run Dunia”, alitakiwa kuimba “Kichaa cha Ng-ono Kina Run Dunia.”
Post a Comment