Kama wewe ni mwanaume ambaye umekuwa ukijijali mwenyewe kwa kujihudumia mahitaji mbalimbali kama vile kujinunulia pafyumu, boksa, nguo na vinginevyo halafu mwenza wako wala humjali, ujue wewe bado hujakamilika.
Unakuta mwanaume anaweza kununua nguo za zaidi ya laki moja, lakini hakumbuki kumnunulia mwenza wake japo sidiria au kufuli la shilingi elfu moja na mia tano.
Kwa mantiki hiyo, ni kama mapenzi umeyafanya yazoeleke, umemfanya mwenza wako kama ndugu yako wa damu. Unapoacha kumhudumia mwenza wako kwa kumnunulia nguo za ndani, unategemea nani amnunulie?
Usishangae mwenza wako akaingia kwenye mtego wa kuchepuka kwa mtu ambaye anamnunulia au kumpa zawadi hizo mara kwa mara na kumuona kama ni mwanaume ambaye anamjali.
Mwanaume aliyekamilika ni yule ambaye yupo tayari kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo kumjali, kumlinda na kumpenda mwenza wake.
Unawezaje kusimama mbele ya umati na kujiita mwanaume rijali wakati ni dhahiri huna vigezo kwa sababu huwezi hata kumnunulia mwenza wako nguo ya ndani?
Unaweza kukutana na mwanaume yuko na mwenza wake kwa takriban miaka mitatu, lakini hajawahi eti kumnunulia angalau sidiria mwanza wake. Hili ni tatizo ambalo wanawake wengi wamekuwa wakilalamika na kuwaona wanaume wao hawawajali.
Kama ulikuwa hujui kuhusu hilo, basi tambua kuwa kitendo cha wewe kutokumnunulia mwenza wako nguo za ndani ni kutoa fursa ya yeye kuchepuka na mwanaume ambaye ataonekana anamjali na kumpenda kwa kumnunulia vitu hivyo ambavyo wewe unavipuuza au kuviona vidogo vidogo.
Post a Comment