UTAJUAJE KAMA WEWE NI MTU WA KULALAMIKA LALAMIKA SI MTU WA KUONGEA NA UNABOA!

Mwanamke mzuri
Leo nilikua naongea na mteja wangu mmoja, akawa ananiuliza nini tofauti kati ya KUONGEA na KULALAMIKA. Mara nyingi ninapokua nawashauri wateja wangu huwa nawaambia kama unaongea na mpenzi wako hasa wanwake, kama unaongea na mume au mpenzi wako na unataka akusikilize ni lazima uache kulalamika na kuanza kuongea. Kwamba unapolalamika mwenza wako hukuzoea na hataacha kufanya kile kitu ambacho kila siku unakilalamikia.
Sasa najua watu wengi, hasa dada zangu inakua ngumu sana kwao kujua tofauti kati ya KUONGEA na KULALAMIKA. Wakati mwingine mtu anaweza kukuambia “Tatizo lako unapenda sana kulalamika!” Lakini kila ukifikiria unaona kama uko sawa, hujioni kama mlalamikaji hivyo unakuta hata hujui ufanye nini ili mahusiano yako yasimame bila kulalamika. Sasa kama una tabia hii basi kuna vitu viwili vikubwa ambavyo hutofautisha KUONGEA na KULALAMIKA.
(1) Kukumbushia Makosa Ya Zamani; Mtu anayelalamika ni mtu ambaye hasahau kitu kinapotokea, mume au mke anapofanya makosa badala ya kumhukumu kutokana na makosa ya wakati huo basi hukumbushia makosa ya zamani na kumhukumu nayo, kwake hakuna kitu kinapita. Kwa mfano mwenza wako kachelewa kurudi nyumbani, kwa mtu ambaye anaongea atasema hivi;
“Mbona leo umechelewa, nilijjaribu kukupigia simu yako haipatikani? Vipi huko kazini…ulikua wapi mpaka saa hizi?” Huyu ataongea, atasubiria jibu, hata kama mhusika ni kawaida yake kuchelewa lakini hatakumbushia kuchelewa kwake kwa jana. Lakini mtu anayelalamika atasema “Nimechoka na tabia yako, mambo gani haya kila siku kunijia usiku, juzi ulikuja hivi, tangu tuoane hujawahi, tangu sijui lini unakuja usiku!”
Hahukumu kuchelewa kwa siku ile, akasikiliza labda kweli mtu ni mchelewaji, lakini siku husika inawezekana hata alikua na tatizo la kweli, labda anaumwa, labda kulikua na mgonjwa, labda kasimamishwa kazi na mambo kama hayo. Wewe unabeba kuchelewa kwa miaka kumi iliyopita unakulete siku hiyo. Sasa kwakua mtu hatachelewa siku moja tu basi anasema kuwa kazi yako ni kulalamika.
Kama unaongea na mtu na unataka akusikilize kweli nilazima ujifunze kuacha kabisa kukumbushia makosa ya zamani hasa kama mhusika ulishamsamehe. Unapokumbushia makosa ya zamani haisaidii, inamfanya mhusika kukuzoea na badala ya kujiona mkosaji akaomba msamaha basi hukuona kama una kisirani kwani unakumbushia vitu ambavyo yeye ashavisahau na hawezi kuomba msamaha kila siku kwa kosa lilelile.
(2) Kuhukumu Kabla Ya Kusikiliza; Utajua unalalmika kama unamuona mwenza wako au mtu yeyote anafanya kitu flani, kabla ya kumsikiliza ili hata kama ni kukudanganya akudanganye ushaanza kumhukumu. Umemuona mpenzi wako anaongea na mwanaume au mwanamke, badala ya kuuliza unaanza nimekuona umesimama na Malaya wako, nishakuambia hiyo tabia yako, mfanyakazi mwenzako gani mnaangaliana namna ile.
Umekuta meseji “Mambo za tangu jana?”, unasikia “Mwanamke gani anakutumia meseji usiku huu!” Umemtumia meseji hajakujibu au unamuona online hachat na wewe unaanza. “Utakua ukichat na Malaya wako, usiku nimekutumia meseji hujajibu, kila nikiingia online unachat tu, kila saa simu yako iko bize ulikua unaongea na wanwake tu!” Humpi nafasi ya kujielezea ushahukumu, unakua na majibu yako kichwani na unaanza kulalamika.
Kama ingekua ni kuongea ungemuuliza mbona ulikua online hukujibu SMS zangu akakupa majibu kuwa labda alikua anachat kwenye group au alikua sijui anafanya nini! Lakini wewe unahukumu, unataja na Malaya wake na unaenda kuangalia na namba nyingine kuwa zipo Online unaamua kuwa alikua anachepuka. Amechelewa badala ya kusubiri aje akuambie kwanini kachelewa wewe anaingia tu ushaanza!
“Najua ulikua kwa wanwake zako, mtu gani unarudi saa nane, nimechoka kukufulia, atakua ni flani!” Simu inaita kapokelea nnje humuulizi kwanini ushaanza kuhukumu, “Najua ulikua unaongea na Malaya wako, najua hivi na vile!” Kama una tabia hizi, kama hivi ndivyo namna ambavyo mwenza wako akifanya kosa unaongea naye basi jua kuwa wewe huongei bali unalalamika.
Pia jua kuwa mwenza wako atakuzoea na hatakua akikuchukulia siriasi kwani hata wakati utakapokua ukilalamikia kitu cha kweli basi atakuona kama una kisirani. Nilazima ujifunze namna ya kuongea, kama unataka kuchukuliwa siriasi, kama unataka aache hiyo tabia inayokukera basi nilazima uache kulalamika na kuongea. Watu wanakuheshimu unapoongea zaidi kuliko unapolalamika.
Unaweza ukaona unaongelea kitu kila siku lakini wala habadiliki, kumbe ishu si kwamba hakusikii, hapana ishu nikuwa huongei bali unalalamika hivyo anakua anakuzoea na mbaya zaidi anachukulia kuwa kulalamika kwake si kwakua yeye anafanya makosa bali nikwakua wewe unakisirani. Hata akifanya kosa la kuonekana kwakua kashakuzoea ukiongea utasikia “Hiyo ndiyo kawaida yake!”


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post