*Ujumbe kwa wewe ambaye Hujaoa Bado .*


Moja ya matatizo makubwa katika mahusiano ni watu kujiingiza katika mahusiano kabla ya wakati.
Mahusiano sio mabaya wala wale ambao wanahusiana sio wabaya ila watu wanahusiana vibaya na hakuna namna ambayo tunaweza tukahusiana vibaya alafu ikatuletea matokeo mazuri maishani.
Mhubiri anasema: “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.
Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.” (MHU.‬ ‭3:1, 11‬ ‭SUV‬‬). Katika maisha kila jambo lina majira yake na kila kusudi lina wakati wake.
Kujihusisha na mahusiano nje ya majira yake na kabla ya wakati wake ni hatari sana.
Moja ya makosa makubwa ambayo watu wanafanya ni kufikiri kwamba kwa sababu wamebalehe au kuvunja ungo basi hata nafsi yake na roho yake nayo imebalehe na kuvunja ungo.
Huwa miili inabalehe na kuvunja ungo muda mrefu kabla nafsi na roho hazija balehe na kuvunja ungo.
Kuwa tayari kimwili kwa ajili ya mahusiano haimaanishi kuwa kinafsi na kiroho upo tayari kwa ajili ya mahusiano.
Maandiko yanatuambia kuwa Mungu anakifanya kila kitu kuwa kizuri kwa wakati wake.
Kwa hiyo mahusiano yatakuwa mazuri kwa wakati wake.
Watu wanaanza kujihusisha na mahusiano mapema mno na kwa sababu ambazo sio sahihi.
Maandiko yanasema: “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” (RUM.‬ ‭12:2‬ ‭SUV‬‬). Katika swala zima la mahusiano lazima tuwe makini sana kutokufuatisha namna ya dunia hii.
Tunahitaji kugeuzwa namna tunavyofanya mahusiano kwa kufanywa upya nia zetu kwa Neno la Mungu.
Lazima tujue mapenzi ya Mungu hasa ni yapi kwa habari ya namna ya kuhusiana.
Watu wa dunia wana girlfriend na boyfriend na watu wa Kanisa nao vivyo hivyo.
Nani kakuambia kuwa ni mapenzi ya Mungu kuwa na girlfriend au boyfriend?
Hatuwezi kufanya kama wao alafu tutegemee matokeo tofauti na wao.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post