Mambo 10 Ambayo ni Sumu Katika Mapenzi




Mambo 10 Ambayo ni Sumu Katika Mapenzi | UDAKU SPECIAL BLOG
KATIKA harakati zako za kutafuta mpenzi, unaweza kukutana na mwanamke ambaye kwa sababu moja au nyingine anakwondolea uwezo wako wa kufikiri, kutumia mantiki na pia kutumia akili yako ya kuzaliwa. Si lazima awe amekufanyia kitu, lakini inaweza kuwa ni ulevi wako tu unaosababisha ufanye mambo yasiyo ya kawaida. Pengine ndiyo maana baadhi ya wasanii huzungumzia suala la “kudata” kutokana na mapenzi.

Ni jambo jema kudhani kuwa wewe na mpenzi wako mnapendana kwa dhati na kwamba kila mmoja amefika kwa mwenzake, lakini kama mojawapo ya mambo haya kumi yaliyoelezwa hapa chini litajitokeza, basi fahamu kuwa yamkini umependa kuliko kawaida, yaani ni kama umenyweshwa sumu ya penzi. Kumbuka kupenda ni kuzuri, lakini kupenda kupindukia kunaweza kukutumbukia nyongo, kwani katika kila jambo kinahitajika kiasi.

1. WIVU WA KUPINDUKIA
Ni jambo jema kwa mwanamume kumtakia heri mpenzi wake na kufanya kila awezalo kuhakikisha kuwa hapati madhara, lakini iwapo utakuwa mtu wa wasiwasi na mashaka pale unapomwona mpenzi wako akizungumza na mwanamume mwingine, au anapotoka na marafiki zake wa kike, au anapovaa nguo inayomfanya atamanishe, basi fahamu kuwa tayari umekunywa sumu ya mapenzi.

Katika uhusiano wa kimapenzi, kuaminiana ni jambo muhimu sana. Kama kweli unataka mpenzi wako akupende kwa dhati, mwoneshe kuwa unamwamini na unaheshimu maamuzi yake, ikiwa ni pamoja na maamuzi ya kutoka na marafiki zake wa kike na kuwa na marafiki wa kawaida wa kiume. Ondoa hofu na acha kabisa kumpeleleza, maana wapo wanaume ambao hutumia muda wao mwingi kuwapeleleza wapenzi wao ikiwa ni pamoja na kuwategeshea kamera na rekoda za simu.

2. KUTOMWACHIA NAFASI MPENZI
Kama huishi na mpenzi wako ni jambo la kawaida kuwa na hamu ya kumwona mara kwa mara, lakini kumbuka kuwa mpenzi wako naye ana maisha yake na anahitaji nafasi ya kuwa peke yake kwa ajili ya mambo yake binafsi.

Hisia za kutaka kuwa na mpenzi wako muda wote zinaweza kudhaniwa kuwa ni za mapenzi ya dhati, lakini kwa hakika hiyo si ishara njema ya mapenzi ya kudumu. Hebu jiulize kama unaweza kuendeleza hali hiyo maisha yako yote. Ni wazi kuwa utachoka. Kwa hiyo, mpe mpenzi wako fursa ya kupumua. Namna hii mpenzi wako atajenga hamu ya kutaka kukutana nawe lakini ukiwa naye muda wote hamu hiyo itaisha.

3. KUMWAMULIA MPENZI MAMBO YAKE
Unaweza kujikuta ukisukumwa kumwambia mpenzi wako awe anavaa nini wakati gani, akutane na nani na kwa wakati gani au ale nini. Ukiona hivyo, fahamu kuwa hayo si mapenzi, bali umepitiliza na pengine mwisho wa uhusiano wenu unanukia.

Hata ukiachilia mbali suala zima la usawa wa jinsia, hakuna mwanamke ambaye angependa apangiwe kila kitu kuhusiana na maisha yake. Kama ilivyodokezwa hapo juu, kila mtu ana maisha yake na kilichowaunganisha ni mapenzi tu. Kama utataka kumpangia kila kitu ni wazi kuwa utaishia kuishi peke yako.

4. KUMUULIZA MPENZI MASWALI
Iwapo utajikuta ukimuuliza mpenzi wako maswali mengi yanayoonesha wasiwasi wako kuhusiana na mwenendo wake, fahamu kuwa kuna tatizo na tatizo hilo lisipopatiwa ufumbuzi utakuwa mwanzo wa mwisho wa uhusiano wenu.

Mwanamke angependa umuulize maswali ya kawaida kuhusiana na jinsi siku yake ilivyokuwa na kama marafiki zake hawajambo au la, lakini kila jambo lina mpaka wake. Mwanamke hatarajii kuwa kila mnapokutana atakuwa kama ameingia kwenye chumba cha mtihani au usaili wa kazi.

5. KUTOAMINI ANACHOKWELEZA MPENZI
Wakati mwingine watu hushindwa kuwaamini wenzao, lakini kwa sababu ambazo ni za msingi, lakini kuna wakati ambapo mtu hushindwa kumwamini mwenzake bila sababu yoyote ya msingi, au kwa sababu zisizo sahihi, kisingizio kikiwa ni mapenzi.

Kuna tatizo la kisaikolojia la kujishuku au kuwashuku wenzako. Hili ni jambo ambalo linaweza kukuharibia mustakabali wako katika mapenzi, maana husababisha kujengeka kwa mazingira ya kutokuaminiana. Ili uweze kwenda sanjari na mpenzi wako, amini kila anachokweleza hadi pale utakapokuwa na sababu za msingi za kutokumwamini. Na hata unapokuwa umelithibitisha jambo, endelea kuwa katika uhalisia wako.

6. KUACHA HOBI, MARAFIKI
Mahusiano ya kimapenzi mara nyingi huhusisha kila mmoja kuacha baadhi ya mambo yake kwa ajili ya mwenzake. Hata hivyo, lengo ni kuweka tu uwiano wa mahitaji, si kuacha kila kitu ulichokuwa nacho kwa ajili ya mwenzako, ama kwa shinikizo, au kwa kulewa penzi.

Iwapo utabaini kuwa marafiki zako sasa wamekuwa ni marafiki zako wa zamani na hobi zako zimebaki tu katika kumbukumbu japo kwa hakika bado unahisi mapenzi katika hobi hizo, basi tambua kuwa huyo mrembo wako amekunywesha sumu ya penzi na sasa huwezi hata kuitumia vema mantiki yako.

Mbaya zaidi, iwapo utabaini kuwa marafiki zako wapya ni marafiki wa siku zote wa mpenzi wako na hobi zako ni zile za mpenzi wako, basi tambua kuwa huna tena nafsi yako, bali umejisalimisha mzima mzima kwa mpenzi wako. Lakini msemo mmoja wa hekima unatwambia usiweke mayai yako yote kwenye kikapu kimoja. Yamkini unaelewa.

7. KUKUBALI KUPELEKESHWA
Pengine unakumbuka kuwa kuna nyakati ambapo ulikuwa na uwezo wa kujikita katika jambo moja na kulifanya kwa umakini, huku ukiwa pia mwerevu, mjanja na unayejisimamia, lakini leo unayeyuka kirahisi tu kama barafu iliyowekwa juani! Hii ni hatari kwa mustakabali wa maisha yako.

Mbaya zaidi ni pale utakapoiacha kazi yako inayokulipa vizuri na kufanya kazi nyingine kwa ajili ya kumfurahisha mpenzi wako. Ukifika hali hii ujue wewe mwenyewe kuwa hapo hakuna mwanamume.

8. UTAYARI WA KUFA KWA AJILI YAKE
Umewahi kujisikia kuwa na utayari wa kufa kwa ajili ya mpenzi wako? Kama jibu ni “ndiyo”, basi fahamu kwa hakika kuwa hayo uliyo nayo si mapenzi bali ni upumbavu. Pengine huku ndiko kunywesha sumu ya mapenzi. Kwa hakika, hakuna mwanamke ambaye anastahili kumfanya mwanamume yeyote kufa kwa ajili yake.

Yamkini wanaume wanaolengwa katika makala haya si wavulana wanaosoma sekondari, waliobalehe majuzi, ambao wakipenda au kupendwa hujiona kama wako katika sayari yao. Mwanamume aliyepevuka hujiamini na hayaweki maisha yake yote mikononi mwa mwanamke, hata kama mwanamke huyo angekuwa ndiye mrembo wa dunia.

Iwapo, ama kwa ujinga au kwa kufahamu umewahi kumwambia mpenzi wako: “Ukiniacha nitajiua,” na ukawa unaamini hivyo kabisa, basi yamkini unahitaji kutafuta msaada wa ushauri nasaha, maana kwa hakika umepotoka.

9. MUDA WOTE UNAWASILIANA NAYE
Vijana wa siku hizi ni watumiaji wazuri sana wa simu, lakini iwapo utabaini kuwa asilimia kubwa ya muda wako unautumia ama kwa kuongea au kuwasiliana kwa ujumbe mfupi na mpenzi wako, basi fahamu kuwa kuna tatizo ambalo linahitaji ufumbuzi wa haraka.

Kumbuka kuwa mapenzi hayachukui nafasi ya kila kitu. Yamkini huyo mpenzi wako amekukuta unaishi na kuna mambo ya muhimu ya kufanya. Hebu achana na simu kwanza ufanye mambo ya muhimu kuhusiana na maisha yako. Kama mpenzi wako hakwelewi katika hili basi hakufai.

10. NDUGU ZAKE WANAKUFUATILIA
Iwapo utabaini kuwa marafiki, ndugu na jamaa za mpenzi wako wanamtonya mpenzi wako kuhusiana na kile wanachokiita mwenendo wako mbaya, usipuuze hali hii. Kuna uwezekano mkubwa kuwa watu hawa wanayo sababu ya kuwa na wasiwasi na mwenendo wako, kwa hiyo jichunguze na kuangalia jinsi unavyoenenda.

Hata hivyo, jambo hili si ishara njema ya mustakabali mwema wa uhusiano wenu. Iwapo mpenzi wako ataweka watu wake wakufuatilie, maana yake halisi ni kwamba hakuamini. Katika hali kama hii, haitarajiwi kuwa mustakabali wa uhusiano wenu utakuwa mzuri, kwani kutakuwa na uingilizi mwingi wa ndugu, jamaa na marafiki zake. Unaweza kukubali kuendelea kuishi katika hali hii kwa kisingizio cha mapenzi, lakini ukweli ni kwamba hayatakuwa mapenzi bali karaha.

KUWA MAKINI
Kama unavyoona, hizi ni baadhi tu ya dalili kuwa mapenzi yako kwa mwanamke sasa yanaelekea katika ulevi, mithili ya ule wa dawa za kulevya. Jambo moja la kukumbuka ni kwamba kweli mapenzi ni kitu kizuri, lakini pia mapenzi yanahitaji kuwa jambo linaloashiria mustakabali mwema kwa wahusika wawili. Yakiwapo mambo haya kumi hauwezi kuwapo mustakabali mwema katika mapenzi.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post