NIZUNGUMZE NA WANAUME


Mwanaume, mgeukie mke wako.
Wanaume wengi wamekuwa wakiwageuzia kisogo wake zao wakati wa ujauzito, badala ya kuwa karibu nao, wanakuwa mbali nao, na wengine huthubutu kutafuta mpango wa kando, tena hasa siku za mwanzoni wanapojifungua.
Ukweli ni kwamba, mwanamke anapokuwa mjamzito ndicho kipindi ambacho anamuhitaji sana mume wake, ndicho kipindi ambacho anahitaji sana kupendwa, kujaliwa, na kuangaliwa kwa ukaribu na mume wake.
Kwa upande wa wanaume, hiki ndicho kipindi cha kumgeukia mke wako kwa kuwa karibu naye; unamsaidia kupika, kufua, kusafisha chumba chenu cha kulala, kwenda naye kliniki, na hata kumtoa out kwa ajili ya chakula na mazungumzo au matembezi. Jambo hili litampa mkeo afya lakini pia mtoto tumboni mwa mama yake.
Eneo jingine ambalo wanaume wengi ni wadhaifu ni katika kipindi wake zao wanapokuwa wakiumwa. Utakuta mwanaume akiondoka nyumbani akiwa amemwacha mke wake mgonjwa kitandani, harudi mpaka jioni, na akirudi anakuwa bize na mambo mengine, hana muda wa kuwa karibu na mke wake. Jambo hili huwaumiza sana wanawake.
Kipindi mke wako anaumwa, ndicho kipindi cha kumgeukia mke wako hasaa na kumwonyesha kuwa unajali.
Mpikie chakula, mwekee maji bafuni ya kuoga, mnyoshee nguo za kuvaa, mwandikie chai na chakula mezani, alafu unakaa naye kumlisha na umsaidie kwa kila anachohitaji.
Unapokuwa mbali naye kwa ajili ya majukumu ya kazi, hakikisha kila wakati unampigia simu ili kumjulia hali yake; na unaporudi nyumbani njoo na kitu akipendacho mikononi mwako, kisha fika na kumlaza mapajani mwako au kifuani mwako na kumkabidhi zawadi hiyo, kisha mpe pole.
Unaweza kumletea hata kadi ya kumtakia kupona haraka ikiwa imeambatana na ua. Kifupi ni kwamba, fanya kila kitu chema kinachoonyesha kuwa umemgeukia, upo karibu naye, na upo kwa ajili yake. Hii itaimarisha ndoa yako na kumwongezea mke wako shauku yake juu yako.
Mwanaume mgeukie mke wako; jidhabihu kwa ajili yake, jitoe kwa furaha na moyo wa kupenda maana wewe ni wake na upo kwa ajili yake.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post