Tarehe (Tarehe 26/05/2018) ndiyo siku ambayo nilipaswa kufunga ndoa na mpenzi wangu wa muda mrefu. Mimi na Alex (Sio jina lake halisi) tulikutana wakati tuko chuo, yeye akiwa mwaka wa tatu mimi nikiwa mwaka wa pili. Ingawa tulikua tunakutana kabla lakini hatukuwahi kuongea mpaka siku moja Rafiki yangu mmoja alikua anaumwa nayeye alikuja hospitalini kumsalimia rafiki yake.
Kama wanachuo tulisalimiana na mazungumzo yakaanzia hapo, baada ya hapo tulikua marafiki mpaka kuwa wapenzi, alipomaliza chuo yeye alipata kazi mwanza hivyo akaniacha Dar, lakini tuliendelea kuwasiliana mpaka nikamaliza chuo. Kusema kweli alikua ananijali, nilikua nampenda nayeye ananipenda, katika kipindi chote cha miaka minne ambayo tulikua na mahusiano naye hatukuwahi kuwa na migogoro mikubwa.
Baada ya mimi kumaliza chuo nilikua tayari kuolewa lakini Alex alikua bado, aliniambia kuna mambo anakamilisha hivyo nilimuelewa, hata mimi nilitaka kupata kazi kwanza ili angalau niwe na kitu changu mwenyewe, sikutaka kuolewa na kuanza kuomba kila kitu. Mwaka jana mwanzoni ndipo nilipata kazi, haikua ya kudumu, nilipata kazi ya uhasibu katika kampuni moja ya ujenzi.
Wanahusika na kujenga Barabara, mimi nilikua kama mhasibu na nilianzia makao makuu hapa hapa Dar. Ilikua ni ya mkataba wa mwaka mmoja wanakuangalia kisha ndiyo wanakupa mkataba wa kudumu. Nilifanya kazi kwa miezi sita, mwezi wa saba Alex alikuja kwetu kujitambulisha, akanivalisha pete na kuanza mchakato wa harusi, kwakua nilikua na Kaka yangu ambaye alikua anaoa mwezi wa kumi na mbili tulikubaliana sisi tuoane mwezi wa tano mwaka huu.
Haikua na shida sana kwani tulikua tunapendana wote hatukua na haraka kihivyo. Mwezi wa tisa mwaka jana nilihamishwa kikazi, kampuni yetu ilipata mradi huko mkoani hivyo mimi nikapelekwa kama mhasibu. Haikua na shida sana kwani Alex alikua Mwanza hivyo hatukua karibu kihivyo, nilifikia huko na kuanza kazi, kampuni ilinitafutia nyumba na kunilipia hivyo kwa mara ya kwanza niliondoka nyumbani na kuanza kuishi maisha ya mwenyewe mwenyewe.
Nikiwa pale kuna Kaka mmoja ambaye alikua ni jirani yangu, wote tulikua tumepanga nyumba moja, yeye anafanya kazi Benki moja tu maarufu hivyo mara nyingi anakua bize lakini kila siku jioni akitoka kazini huwa tunaonana. Kwa muda kidogo tulianza kuzoeana, kwakua mimi siwi bize sana kazini basi jioni huwa napika na mara nyingi nilikua namkaribisha kuja kula.
Yeye pia alikua anajiongeza, alikua analeta nyama, ananunua Kuku na vitu vingine vingine kwaajili yangu mimi kupika. Kwa muda mfupi tu tulijikuta tunazoeana, bila kupanga tuliingia katika mapenzi. Mara ya kwanza niliona kama kitu cha mara moja, sikujali sana kama yeye ana mahusiano au la kwani nilikua na mchumba wangu na mimi nilimuambia. Pia alikua anamfahamu Alex kwani mara moja moja alikua anakuja na kila wakati akija basi aliheshimu.
Mwanzo ilikua siri lakini baada ya muda wapangaji wengine walijua na maneno ya kaanza kusemwa. Nilianza kusikia maneno kutoka kwa majirani wakiniambia niwe makini kwani ameoa, mwanzoni sikujali ila niliamua kumuuliza. Aliniambia yeye hajaoa ila kuna mwanamke alikua naye kipindi flani wana mtoto mmoja lakini walishindwana na kuachana. Sijui kwanini lakini nilipata amani kidogo, kwa namna flani nilishaanza kumpenda.
Alikua yuko karibu sana na mimi, ananijali kwa kila kitu, tofauti na Alex yeye alikua ni mtu wa kunisifia, nikipendeza anajua, nikisuka anajua, mtu wa kunitoa out na alipenda utani utani sana. Kwakifupi nilikua najisikia raha zaidi ninapokua karibu naye kuliko nikiwa na mpenzi wangu. Kuna wakati nikawa sitamani tena kuwa na Alex ingawa kwa wakati huo sikua nafikiria kuvunja uchumba.
Alex alikua akitaka kuja natafuta sababu za kuwa bize ili asije jambo ambalo lilimkera kidogo na kumfanya kuwa na hasira, alianza kunihisi vibaya na mara nyingi usiku nilikua namuaga mapema kabisa nikimuambia nalala ili tu asije kunitafuta usiku na kunikosa. Hali hiyo ilimfanya Alex kulalamika kila siku, aliniambia nimebadilika simtafuti kwenye simu na mambo mengine mengi. Kule kulalamika kwake kulinifanya nizidi kumchukia na kumuona kichomi.
Siku moja mwaka huu mwezi wa pili mwanzoni kabisa nilipigiwa simu na mwanamke mmoja. Sijui alipata wapi namba yangu lakini aliniambia nimuache mume wake, nilishangaa lakini alinitumia picha za mtoto, picha zake za harusi yake huyu mwanaume mpya, akanitumia na cheti cha ndoa vyote kwenye Whatsapp, akaniambia yeye ni mke wake na kama ananidanganya kuwa hajaoa basi nijue tu kuwa yeye ni mume wa mtu na wana ndoa ya Kanisani.
Kusema kweli nilichanganyikiwa, pamoja na kwamba Fred (Si jina lake halisi) hakuwahi kuniambia kuwa anataka kunioa au hatukuzungumzia mahusiano siriasi lakini nilishaanza kumpenda. Nilipaniki sana, alipokuja nilimuonyesha ushahidi na kumuuliza kwanini alinidanganya aliniambia kuwa nikweli alioa na huyo mwanamke ni mke wake lakini wako katika mchakato wa kuachana, alioa akiwa mdogo sana hivyo hakufikiria na ulikua ni msukumo wa wazazi.
Alinihakikishia hampendi na kumpigia simu tena mbele yangu akimuambia aache kumsumbua yeye hataki tena mawasiliano nayeye kama ni mtoto basi atalea. Hapo nilipata amani kidogo, siku iliyofuata alinipeleka kwa marafiki zake na kuwatambulisha kama shemeji yao, alinipeleka mpaka kwa Mama yake mdogo na kunitambulisha. Hapo ndipo aliniambia kuwa ananipenda na anataka kunioa.
Kusema kweli nilikua njiapanda kwani Fred alikua na ndoa ya kanisani, aliniambia nisiwe na wasiwasi kwani ndoa inavunjika na ingawa hawezi kufunga tena ndoa nyingine ya kanisani lakini tunaweza kufunga ndoa ya serikali. Kumbuka wakati huo mimi na Alex hatukua vizuri sana, alishahisi namsaliti. Tayari nilishapata mkataba mwingine na nilitakiwa kurudi Dar lakini kwasababu ya Fred niliomba mpaka nikabakizwa mkoani.
Alex aliposikia alikasirika na kuniuliza kwanini nikamuambia huku kuna madili mengi. Aliniuliza nafanya nini nikamuambia nalima ndipo aliniambia kama kweli mimi ni mchumba wake nihamie Dar na kama simpendi basi nibaki. Nilijikuta nakasirika nikamuambia huwezi kunipangia maisha wakati hujanioa kama vipi kila mtu ashike njia yake. Nilimkatia mawasiliano, aliendelea kunitafuta kuuliza nini kimetokea lakini nilimblock, akawatumia na ndugu zangu lakini nalo lilishindikana.
Tukaachana na harusi ikaahirishwa, maandalizi yalishafanyika kwani ilibaki miezi miwili tu. Kwa hasira kwa upande wao hawakuahirisha chochote, Alex alitafuta mwanamke mwingine na alioa tarehe ileile ambayo tulipanga sisi. Ndani ya miezi miwili tu aliweza kupata mwanamke mwingine, mimi kwangu kuachana naye ilikua ni kama faraja kwani niliona nitapata uhuru wa kuwa na Fred wakati nikisubiri yeye kuachanana mke wake.
Baada ya kuachana na Alex nguvu zote nilielekezea kwa Fred, sikutaka kukaa muda mrefu kabla ya kuoana naye. Nilihamia kwake na tukaanza kuishi rasmi kama mke na mume, alinivalisha pete ya uchumba ingawa bado alikua hajaachana na mke wake. Mwezi huu mwanzoni Mama yake Fred alikua anaumwa, hivyo alilazimika kwenda Tabora, alichukua likizo kwani alikua na hali mbaya sana na yeye kwao ndiyo mtoto mkubwa.
Alikaa huko kwa wiki moja tu na kwa bahati mbaya Mama yake alifariki, kama mchumba wake niliamua kwenda, alitaka nisiende kwakua hatujarasimisha mambo lakini mwenyewe nilitaka tu kwenda nilitaka wanijue. Nilifunga safari na kwenda kwao ambapo niliongozana na Mama mdogo wake yule ambaye alinitambulisha kwake. Kule nilipokelewa vizuri tu kitu ambacho kilinipa moyo kuwa napendwa.
Nilikutana na mke wake, sikushangaa sana kwani kwakua wana mtoto nilijua kaenda kumpeleka mtoto ili amzike Bibi yake. Kilichonishangaza ni namna nilivyokua natambulishwa, kwa ndugu zake wengine wote nilikua natambulishwa kama rafiki wa Mama yake mdogo, mkewe alikua ananifahamu hivyo katika mazishi na siku zote tatu nilizokua pale Fred alijieweka mbali na mimi kabisa, sikutaka kumuuliza kwani alikua na uchungu wa kufiwa na Mama yake.
Alikaa kule kwa wiki tatu kisha akarudi, chakushangaza aliporudi hakurudia pale, alitafuta chumba kingine na kuhamia huko. Kumbe alirudi na mke wake na mwanae, pale kwangu bado alikua anakuja lakini haikua kama zamani, alikua akilala kule na mkewe. Nilipomuuliza aliniambia kuna mambo anamalizia, nilishangaa kwani haikuingia akilini ni kwanini amlete mkewe pale. Yeye alizidi kuniambia kuwa haya mambo hayahitaji haraka atamuacha taratibu.
Niliamua kuchunguza zaidi nikagundua kuwa kumbe hakua akiishi na mkewe kwakua mke alikua kijijini akimuuguza Mama yake ambaye alikua mgonjwa kwa muda mrefu. Baada ya Mama yake kufariki hakukua na mtu tena kwao hivyo alilazimika kumchukua mkewe na mwanae ili kuishi nao. Niliumia sana mbaya zaidi hataki hata kuniacha na kila nikimuuliza ananiambia atamuacha mke wake taratibu.
Ananiambia mke wake ni mjamzito hivyo hawezi kumuacha kwa haraka itaathiri mtoto nivumilie. Anaonekana hata kama hajali, anajifanya hajui kua nilimuacha mchumba wangu kwaajili yake, leo (Tarehe 26/05/2018) ndiyo ilikua niolewe lakini nikamuacha mchumba wangu. Alex kafunga ndoa na mwanamke mwingine mimi nabaki na maumivu sijui hata hatuma yangu, ndugu hawataki kunisikia kwani nimewaaibisha walishaandaa kila kitu, kweli YAMENIKUTA!
Post a Comment