MBINU ZA KUMWOMBA MSAMAHA MPENZI WAKO



Marafiki zangu kukosea katika maisha ya binadamu ni kawaida. Ni sehemu ya maisha yake. Tena inaaminika kwamba, kukosea ni kujifunza, maana kosa utakalofanya leo ni funzo la kesho. Hii ipo pia hata katika uhusiano na wapenzi wetu, mara kadha wa kadha tumejikwaa na kuwakosea.

Hakuna cha ajabu. Ni kawaida kabisa, lakini jambo la msingi hapo ni kwa namna gani tunajifunza kupitia makosa. Ni kwa jinsi gani tunamaliza tofauti hizo. Maana unaweza kuwa hodari wa kukosea au ukawa bingwa wa kusamehe, lakini wimbo huo ukaendelea kubaki hivyo hivyo kila siku.
Lakini pia, wapo ambao kwa bahati mbaya, bila matarajio yao, wanajikuta wakiwa wamewaudhi wapenzi wao. Ni bahati mbaya na yawezekana kabisa wanaumia sana mioyoni mwao, lakini wakashindwa jinsi ya kumaliza ‘bifu’ hilo katika penzi lake.
Siku zote mkosewa hukosa raha, hupoteza hamu ya kukutana na mpenzi wake lakini kubwa zaidi, hujishusha/hukushusha thamani ya mapenzi yake kwako. Lakini mkosewa huyo huyo, akioneshwa kwamba makosa yaliyofanyika hayakuwa ya makusudi na kutumia njia bora za kufikisha hisia zako kwake, hujisikia amani na hali yake kurejea kawaida.
Rafiki zangu, yawezekana ukawa upo katika kipindi cha matatizo na mpenzi wako na hujui jinsi ya kuweka mambo sawa. Wakati mwingine huna tatizo, lakini kwasababu upo kwenye uhusiano basi si ajabu mambo kwenda mrama siku moja.
Hapa chini, nimekuandalia mambo matano muhimu ya kuzingatia unapokuwa umekwenda kinyume kidogo kwa mpenzi wako. Weka ubongo wako wazi, kuruhusu somo hili kichwani mwako, ambalo litakuwa hazina yako na mwongozo katika uhusiano wako.

KOSA LINA UKUBWA GANI?

Hapa tayari umeshagundua kwamba umemkosea mpenzi wako na ni kweli kwamba unaumizwa sana na kosa lako, lakini kwasababu hujamwambia chochote, naye hana raha na wewe. Hana amani ya moyo.
Hapa unashauriwa kutulia na kutafakari ukubwa wa tatizo. Kufahamu ukubwa wa tatizo kutakupa muongozo mzuri sana wa jinsi ya kutatua tatizo hilo. Angalia ulimfanyia nini na kwa kiwango gani?
Mathalani unaweza kuwa ulimuudhi kwasababu alikupigia simu zaidi ya mara kumi bila kupokea, akakasirika. Hili ni kosa dogo.
Lakini yawezekana alikuta sms ya mapenzi kwenye simu yako au alikufumania; haya ni makosa makubwa. Tafakari na ujue ukubwa wa kosa lako.

ONESHA UNAVYOJUTA

Hii ni kwa ajili yako wewe mwenyewe. Rafiki zangu, kutakuwa hakuna maana yoyote kuomba msamaha wa kinafiki au kuomba msamaha ili kumaliza mambo, kama msamaha wako haujatoka moyoni.
Ukiwa peke yako, jiaminishe kwamba umekosea na kwa hakika unahitaji kusamehewa. Jutia ndani ya moyo wako, kwa dhati kabisa ukiwa na ahadi kwamba hutarudia tena. Hili ni zoezi la Kisaikolojia, ambalo litakusaidia baadaye wakati ukikutana na mpenzi wako kwa ajili ya kuomba msamaha.


KUWA MKWELI

Omba kukutana naye. Yawezekana hata mawasiliano si mazuri sana, lakini hapa jitahidi kumuomba mkutane, ikishindikana, tumia mtu wa karibu sana na yeye. Omba kutoka naye kwa ajili ya kuzungumza.
Mweleze ukweli wa kosa lako, onesha jinsi linavyokutesa na kukusumbua. Usijaribu kuongea uongo wowote katika suala hili. Kuwa mkweli. Jutia kwa moyo, aone majuto yako usoni mwako.

Mwambie jinsi unavyoteseka na jinsi msivyo katika maelewano mazuri. Kauli yako ya ukweli, hisia zako wakati wa kuzungumza, ndivyo vitakavyokuweka katika mazingira mazuri ya kuweka mambo sawa.

MHAKIKISHIE HUTARUDIA

Bila shaka, kama utakuwa umefuata taratibu zote hizo kwa umakini, uwezekano wa kusamehewa ni mkubwa sana. Hili ndiyo matarajio yangu, naamini hata wewe pia, lakini ili msamaha huo ukamilike, mhakikishie mpenzi wako kuwa hutarudia tena.

Mwambie kwa kumaanisha, kwamba umegundua udhaifu wako na haupo tayari kumfanya tena asiwe na furaha tena. Hakuna uchawi ni maneno tu!

FANYA KITU MAALUM

Hapa unatakiwa kufanya kitu maalumu kwa ajili ya mpenzi, ukionesha kwamba umekubaliana na msamaha wake na mambo yameisha. Kitu utakachokifanya hapa utalinganisha na ukubwa wa kosa kama nilivyosema awali.

Mathalani unaweza kutoka naye na kwenda kulala naye hotelini, ukihakikisha unampa mahaba mazito kama shukrani kwake. Yapo mengi ambayo unaweza kuyafanya kulingana na uwezo wako kifedha. Fanya vyovyote ili kosa lile lisahaulike moja kwa moja!

Nimeeleweka? Ahsanteni sana marafiki zangu, hadi wiki ijayo tena kwa mada nyigine nzuri zaidi itakayokupa mwanga mpya katika maisha yako ya kimapenzi.


Previous Post Next Post