Agnes, msichana wa miaka 17 aliozwa miezi mitatu iliyopita kwa mwanamme ambaye hakua anamfahamu hata kidogo.
Anavyotusimulia Agnes, "Wazazi wangu walinikalisha na kuniarifu kuwa sikua jukumu lao tena. Walitaka nijitenge nao na kuanza maisha kivyangu.Mambo yalikwenda haraka kinyume na matarajio yangu wakati mwanamme huyo ambaye simfahamu alilipa mahari kwa wazazi wangu.”
“Sikua na usemi wowote kwenye jambo hilo,” Agnes alisema haya akiwa na simanzi tele na kububujikwa na machozi."Sikuchagua kuishi hivi na sina raha"
Agnes alikubali kuzungumza nasi mradi tusimtambulishe. Aidha BBC iliweza kuzungumza naye kwani mumewe hakuwepo.
Tulipopatana naye, alikuwa anatekeleza majukumu yake ya kila siku, kuosha vyombo, kufanya usafi kwa ujumla na hatimaye kujiandaa kutayarisha chajio.
Alionekana mwenye wasiwasi na masikitiko, na haikuwa vigumu kubainisha kuwa alionekana kukata tamaa- visigino vyake vilikuwa vimepasuka, na vipodozi vyake kufifia.
Kuozwa mapema na kwa lazima ni jambo la kawaida huko Zambia, lakini utamaduni huu si wa ki-Afrka tu, bali ni tatizo la kimataifa .
Inakadiriwa kuwa wasichana milioni 14 wanalazimishwa kuoleka kabla ya kufika miaka 18, kila mwaka. Kuamrishwa kuoleka wakiwa na umri mdogo hukatiza utoto wao ghafla.
Agnes anajaribu kwa udi na uvumba kuhepa mfumo huu mpya wa maisha, lakini ana hofu kuwa wazazi wake watamkana iwapo atakwepa ndoa yake.
Umasikini na tamaduni huchangia pakubwa mila hizi ambazo ni maarufu sana huko mashambani.
Wapinzani wa mila hizi wanadai kuwa wazazi huona mabinti zao kama jinsi ya kupata fedha na mali.
Chief Chamuka VI wa Zambia, na mavazi yake ya kiasili – vazi jekundu na kofia nyekundu ilyopambwa kwa manyoya- alihutubia wanakijiji kuhusu hatari na athari za kuoza watoto mapema, na kuwataka wasichana wachanga kuzingatia umuhimu wa masomo na kuenda shuleni.
Kama chifu, nimechukua msimamo kuwa hakuna mzazi atakayeamuru binti wa chini ya miaka 18 kuolewa. Yeyote akiukaye sheria hii ataadhibiwa vikali.” Chifu alisema.
Viongozi wa kitamaduni wanaopigia debe kuolewa kwa wasichana wachanga, hujawa na hamaki wanapoona wenzao wakibadilisha msimamo wao na kupinga kuozwa kwa mabinti wachanga.
Aghalabu, wanaopinga tamaduni hizi huchukuliwa kukiuka mila zilizotumika tangu jadi na vizazi vilivyopita, lakini chifu hakulegeza msimamo wake.
"Nahisi kuwa katika jamii kuna mila zilizo nzuri na zingine mbovu- jambo hili lazima likome,” chifu alisema.
'Athari za kudumu'
Wanaolazimishwa kuoleka mapema huhisi athari hizo kwenye maisha yao ya baadaye.
Beatrice Chikwekwe aliolewa akiwa 15, sasa ana umri wa miaka 32.
Nilijawa na hofu na kuchanganyikiwa siku yangu ya harusi, hata sikuwa na fahamu ya nilichokua nikifanya,” Beatrice alisema. “Nilipata mimba mwaka huo huo na nikapata matatizo nilipokuwa najifungua. Karibu nipoteze maisha yangu”
Bi Chikwekwe sasa anasoma mwaka wake wa mwisho katika chuo cha kilimo, baada ya kupoteza muda mwingi. Akilinganishwa na wengi ana bahati kubwa kwani ni nadra kupata hatima kama ya Beatrice- nafasi ya kwenda shule.
Kuolewa kwa watoto Zambia.'
Kuolewa kwa watoto Zambia.'
“Wasichana wanaooleka mapema hawapati elimu na nafasi za kujikuza kiuchumu hivyo basi hukosa uwezo wa kuinua jamii zao kutoka kwa umaskini,” kundi hili lilisema kwenye taarifa.
Graca Machel, mkewe hayati Nelson Mandela na mmojawapo wa wanaharakati waliarifu BBC kuwa Mila hubuniwa na binadamu na zilizo hatari na zenye athari mbaya lazima zibadilishwe. “Kama wazazi hatuna haki ya kulazimisha watoto wetu kuchukua uamuzi flani,” Graca alisema.
Tunapaswa kubadili mtazamo wa familia na jamii kwa wasichana na kuchukulia mtoto wa kike kama binadamu aliye na maazimio na matarajio, na aliye ana uwezo wa kufuzu kama awezavyo mtoto wa kiume.
Inakadiriwa kuwa wasichana wanopata mimba kabla ya kufikisha umri wa miaka 14 wana uwezekano mara tano Zaidi kufariki wanapojifungua.
Tukirejea Chibombo, shirika la ufadhili ‘Plan International Zambia’ linashirikiana na viongozi wa kitamaduni, serikali na vikundi vinginevyo ili kunusuru wasichana kama Agnes kutoka kwa ndoa za kulazimishwa.
Kwa mujibu wa msemaji wa shirka hilo, panapo ufukara watoto huwa kwenye hatari ya kunyanyaswa. Tunafanya juhudi kuelimisha jamii kuhusu haki za watoto na haki hizo zinazofaa kuheshimiwa.
Kwa sauti ya kutetemeka Agnes anahitimisha manung’uniko yake.
"Saa zingine ni vigumu kutofuata masharti ya wazazi wetu kwani ni ukosefu wa heshima, lakini hatuwezi kuruhusu watufanyie uamuzi ambao una athari mbaya kwetu,” alisema.
"Lilikuwa azimio langu nimalize shule na kuwa muuguzi lakini nadhani matarajio hayo hayatatimia kwani mume wangu hatoniruhusu niendeleze masomo yangu.”
Post a Comment