Faida na Hasara za kuambizana ukweli katika mahusiano

Faida na Hasara za kuambizana ukweli katika mahusiano
Faida na Hasara za ukweli katika mahusiano

UKIZUNGUMZA na wanaume wengi kwa sasa, watakuambia wanawake siyo wa kuwaeleza kila kitu katika uhalisia wake. Wanatakiwa kudanganywa kidogo ili mambo yaende. Wanaitumia hiyo kama silaha wakidai kwamba wanawake ni watu ambao wakijua kila kitu wanasumbua. Wanaamini kwamba hata kama ni fedha, mwanaume akimuambia mpenzi wake ana jumla ya kiasi fulani cha fedha basi matumizi yatakayoibuliwa hapo yatakuwa si madogo. Yaani yataibuka matumizi ambayo hata haukuyategemea, yote hiyo ni kwa sababu tu amemuambia kiasi cha fedha alicho nacho.

Ili kuepusha ugomvi, malumbano yasiyokuwa na kichwa wala miguu, wanaume wengi huamua kuwadanganya wanawake. Hata kama ni kipato chao kwa maana ya mshahara au chanzo chochote cha fedha, hawawaambii ukweli wenzi wao.

Mathalan mwanaume ana mshahara wa shilingi laki tano, anamdanganya mwenza wake kuwa mshahara wake ni shilingi laki nne. Ile laki moja inabaki kama akiba yake. Anajua akimueleza ukweli litakuwa tatizo. Atataka kila shilingi aijue imetumikaje, hata kama mwanaume atakuwa na matumizi yake madogomadogo, yote atataka kuyajua.

Kwa kawaida mwanaume huwa hapendi kufuatiliwa hivyo. Anatamani wakati mwingine awe huru kufanya mambo yake ikiwemo hata kujiburudisha na marafiki zake na mambo mengine kama hayo. Ndiyo maana anaona kuepuka kugombana, bora amfiche.

Hivyo basi utaona, wanaume wakati mwingine hufurahia hiyo hali kwani inawafanya waishi vizuri na wenza wao bila kuwa na ugomvi. Kweli wanafanikiwa, mshahara ukiingia, mama anaweza kuupangia mahitaji yote mpaka unaisha lakini mwanaume anayo akiba yake na maisha yanaenda vizuri.

Hilo ni eneo moja ambalo yawezekana uongo ukawa na faida lakini kwa upande mwingine unaweza kuwa na hasara. Mwanamke anakuwa amefichwa kweli lakini siku zote dunia haina siri. Kama kweli ni mwenza wako na mmeshibana, ipo siku linaweza kutokea la kutokea na siri ikafichuka.

Inapofichuka huwa inakuwa ni aibu kubwa. Mwanamke ataumia kuujua ukweli. Uongo wa mwanaume ambao utakuwa umedumu kwa miaka mingi, utageuka kuwa pigo kubwa katika uhusiano. Mawazo yanakuwa mengi, atajiuliza kama amedanganywa katika hilo, mangapi atakuwa amedanganywa?

Uaminifu wake kwa mwanaume lazima utalegalega kama si kupungua. Kumbe basi ukiweka kwenye mizani kuambizana ukweli na uongo kwenye uhusiano utabaini ukweli una faida kuliko uongo. Ni vizuri mke na mume wakaambiana ukweli.

Kikubwa kinachotakiwa kuzingatia hapo ni namna ya wapendanao kukubaliana na ule ukweli na mipaka yake. Mwanamke anapaswa kutambua kwamba kuna matumizi ambayo si vibaya akampa uhuru kidogo mwanaume wake ili kumfanya naye awe huru.

Mambo ya msingi ya kumshauri kwa maana ya maendeleo kweli ni jukumu lake lakini iwepo tu busara ya kibinadamu katika kukumbushana. Siyo kwa sababu unajua kuna shilingi laki tano basi unaitaka yote, mwanaume awe anakuomba hadi nauli kila siku, haileti picha nzuri.

Tengenezeni mfumo rafiki wa kuelezana kila kitu ukweli kwani itawasaidia. Uongo mara nyingi huwa na madhara. Unaweza kujiona mjanja lakini mwisho wa siku utakuja kuumbuka. Ni ukweli pekee utakaokuweka huru katika uhusiano wenu.

Upo mahali fulani, hauna sababu ya kumficha mwenzako. Mueleze niko sehemu fulani. Hauna fedha, ajue kweli hauna fedha, utachelewa nyumbani basi useme ukweli sababu za kukufanya uchelewe. Zikiwepo fedha basi kwa pamoja mzitumie vizuri. Elekezaneni mambo ya msingi huku pia mkifurahia maisha.

Msijibane mpaka tone la mwisho. Mkipata kumi, tano mnaweza kutumia na tano nyingine mkaweka akiba ya kufanya mambo ya maendeleo. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Mnaweza kunifuata kwenye kurasa zangu za mitandao ya kijamii, Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post