MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA UNAPOANZISHA BIASHARA YAKO
Wakati unapotaka kuanzisha biashara usijiulize maswali kama vile hivi ni biashara gani inayotoka zaidi nikiianzisha na mimi nitafanikiwa? La! Bali jiulize ni kitu gani ninachokipenda kufanya kitaleta mafanikio katika biashara yangu.
Kama unajua kupika chapati au chakula chochote vizuri kwanini usianzishe mgahawa?
Je kama we ni mwanasheria na unajiamini kwanini usianzishe Ofisi ya Kutoa huduma za msaada wa Kisheria?
Kama unajua kujirembua na ukapendeza vizuri kwanini usifungue saloon na duka la vipodozi?
Lakini pia kama wewe umesoma mambo ya uhasibu na mahesabu kwanini usite kuanzisha ofisi ya kutoa msaada wa kitaaluma wa mahesabu ya kifedha kwa maofisi mbali mbali.
Je kama sina elimu yoyote au fani nifanye nini? Jamani swali hili linasumbua sana lakini tunatakiwa kujua ya kwamba Mungu hakumnyima mwanadamu chochote kile, kila mtu aliopo hapa duniani ana kila sababu za uwepo wake ila suala gumu huwa linakuwa ni jinsi ya kutambua kipawa chako ambacho umepewa.
MBINU ZA KUTUMIA KUTAMBUA KIPAWA AU KIPAJI CHAKO
kipawa chako unaweza kugundua kwa kujiuliza binafsi ni kitu gani ambacho unakipenda kabisa kukifanya na moyo wako unafurahia, basi hicho kitakuwa ndio kipaji chako, kwa mfano unapenda kuvaa vizuri na kupendeza kwanini usifungue Duka la nguo au ufuaji wa nguo na kunyoosha?
Je kama unapenda kusafiri, basi kipaji chako kitakuwa ndio hicho fungua Office ya kutembeza watalii.
Ila pia wewe unaweza kuwa ni msomaji mzuri wa vitabu na unafurahia kufundisha sio mbaya ukianzisha maktaba icho ndo kipaji alichokupa Mungu.
Pia kama huwezi kabisa kutumia mbinu za hapo juu basi unaweza tumia njia rahisi ya kuwauliza marafiki zako, walezi au wazazi wanaweza kukusaidia kujua wewe ni nani na ni kipaji gani ulichonacho.
Ukikagua maswali na majibu yako utagundua shughuli unayoipenda, unayoiweza na una kipaji nayo na hiyo ndiyo inayokufaa.
ANZISHA BIASHARA HIVI
Tengeneza bajeti yako kwa kuorodhesha vitu vinavyohitajika na gharama zake ili kuweza kuanzisha biashara yako. Vitu hivyo ni:- Gharama za Kujenga au kupanga ofisi Gharama za Leseni ya biashara Makadirio ya kodi toka TRA Gharama ya vifaa vya ofisi yaani, thamani, makaratasi, mitambo, mashine, nk Manunuzi ya malighafi au bidhaa za kuanzia biashara Idadi ya wafanyakazi na gharama za mishahara yao. Gharama nyinginezo kama vile, umeme, maji, nk. Unatakiwa kujua ni mtaji kiasi gani unahitajika kuanzisha biashara yako. Mtaji huo utaujua baada ya kujumlisha gharama zilizoorodheshwa zote hapo juu.
TAFUTA MTAJI
Mtaji unaweza kupatikana kutoka kwenye vyanzo vifuatavyo:- Akiba au mshahara Msaada au mkopo kutoka kwa ndugu na jamaa. Kuingia ubia na mtu mwenye mtaji ila angalia mtu ambaye hata kuwa kikwazo kwako. Mkopo toka baadhi ya asasi kama vyama vya akiba na mikopo (SACCOS), NGO’s za kifedha isipokuwa Benki kwani hizi huwa hazitoi mikopo kwa mtu anayeanzisha biashara.
WEKA MIPANGO YAKO YA FEDHA VIZURI
Kama unaondoka kwenye ajira na kuingia kwenye biashara, maana yake kipato cha ajira kimefutika moja kwa moja. Sasa usije ukafanya kosa kubwa sana la kuua biashara yako kwa kutegemea kipato cha biashara ndio uendeshe maisha yako, hasa mwanzoni. Utaua biashara yako, anza kuitegemea biashara yako ingalau inapotimiza mwaka mzima tena kwa mafanikio vinginevyo utakuwa unakimbia mbio za panya.
Usifanye kazi ya kuwa unapata Faida unaweka benki, hapana! Fedha zako watatumia wengine kuzifanyia biashara na hautaendelea wala kipato chako hakitakuwa, tumia faida unayoipata kwa kuwekeza na kukuza mtaji wako, acha kabisa biashara ya kuwa unapeleka faida benki.
FANYA BIASHARA YA KIPEKEE
Fikiri na kuwa mbunifu katika kubuni na kuibua biashara mpya, acha biashara za kukopy na kupaste itakugharimu hautadumu. Mfano kama mahali unapotaka kufanya biashara kuna maduka ya nguo na vitu vya makazini na majumbani au biashara nyingine maarufu. Ikiwa mahali pa biashara kuna mzunguko wa watu wengi na kuna mazingira ya kupata faida nzuri unaweza kufanya biashara kama wanazofanya wengine lakini bado una kila sababu ya kuongeza biashara nyingine kwa kubuni na kuibua biashara mpya tofauti na za wafanyabiashara wengine.
PATA MSHAURI WA BIASHARA
Unapokuwa katika wakati mgumu wa kutatua matatizo yako ya kibiashara au unapokuwa na utata katika kufanya maamuzi sahihi ya namna ya kuanza biashara ni vizuri utafute ushauri kutoka kwa watu ambao tayari wamefanikiwa katika biashara kama yako. Pia unaweza kutafuta watu wa kukufundisha jinsi ya kufanya biashara yaani “Business Mentors” ambao watakusaidia kupata ujuzi sahihi na kukupatia maarifa kuhusu biashara yako.
JIAMINI NA USIKATE TAMAA
Kuna wakati unapoanza biashara mambo huwa mabaya hivyo ni vema ujiamini na utafakari ni wapi umekosea au ni nini cha kufanya ili uboreshe biashara yako. Wakati mwingine unapoanzisha biashara inachukua muda watu kujua unauza nini hivyo swala la muda wa watu kujua biashara yako nalo ni jambo la kuzingatia.
Hakuna mafanikio ya haraka hivyo uvumilivu na ukakamavu wako ni muhimusana katika kukuza biashara yako. Kumbuka usikae na kusubiri sana watu waifahamu biashara yako, weka na bidii zako katika kuongeza na kupanua mtandao wa wateja wako.
FANYA BIASHARA UIPENDAYO
Inaaminika kuwa ikiwa mtu atafanya kazi aipendayo basi ataifanya kwa uhodari na utashi wake kuweza kupata mafanikio makubwa, swala hili ni muhimu katika kuamua ni biashara gani unapenda kuifanya. Maendeleo na mafanikio makubwa ya kazi yeyote ile huletwa kwa kufanya kazi unayoiridhia na kuipenda.
AJIRI WATU SAHIHI
Ajiri watu wenye uwezo na watakaokuwa na mchango mkubwa kwenye biashara yako.
Watu unaoajiri kwenye biashara yako wana mchango mkubwa sana wa kukuza au kuua biashara yako. Chagua watu ambao wataikuza biashara yako zaidi na hawa ndio uwaajiri.
Na hata baada ya kuwaajiri fanya nao kazi kwa karibu ili waweze kutoa mchango mkubwa kwenye biashara yako.
KUWA TAYARI KUBADILIKA
Wafanyabiashara wengi wanaoanza biashara na kuonekana ina mafanikio makubwa mwanzoni lakini wanashindwa kwenda na mafanikio yale huwa wanasahau sehemu hii muhimu sana. Kama hupo tayari kubadilika, ni vigumu kwa biashara yako kukua kwa kasi.
Kama ambavyo tumekuwa tunaona, dunia ya sasa inabadilika kwa kasi sana. Biashara nazo zinabadilika kwa kasi kubwa. Kitu chenye faida leo kesho kinaweza kisiwe na faida kabisa. Biashara inayolipa leo kesho inaweza isiwepo kabisa. Jua mabadiliko yanakuja na jiandae kubadilika haraka.
TAMBUA WATEJA NDIO MAFANIKIO YAKO
Mtazamo wa wateja juu ya biashara yako ni kitu muhimu sana kwenye biashara yako, kinaweza kukuza au kuua biashara yako. Kama wateja wanaridhika watafurahi na kuwaambia wengine. Kama hawaridhishwi watalalamika na kuwaambia wengine pia.
Wekeza muda wako kuhakikisha wateja wanapata huduma bora na mahitaji yao yanatimizwa.
MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA KUJUA KABLA YA KUCHUKUA MKOPO
Unahitaji fedha kwa ajili ya nini?
Usichukue mkopo halafu ndio ukaanza kuupangia ufanyie kitu gani. Utajikuta fedha zinaisha na hujafanya jambo lolote kubwa. Jua kwanza hitaji lako la fedha kwenye biashara yako, unahitaji fedha kwa ajili ya nini? Kama ni kukuza, fedha hiyo utaiweka wapi? Huwezi kuchukua mkopo na kutumia fedha yote kwenye kila kitu. Jua matumizi ya mkopo unaochukua kabla hata hujauchukua.
Unahitaji fedha kiasi gani?
Ukishajua ni wapi unaweka fedha utakayopata kama mkopo, jua ni kiasi gani cha fedha unahitaji. Usiseme tu mkopo wowote nitakaopata utanifaa, jua hasa kiasi cha fedha unachohitaji ili kuweza kukamilisha lengo lako la biashara na ndoto zako.
Itakuchukua muda kiasi gani kulipa mkopo huo?
Watu wengi hufurahia kuchukua mkopo bila ya kufikiria muda ambao watatumia kurejesha mkopo huo. Kama utakuwa na kiwango kikubwa cha kurejesha, itakuchukua muda mfupi. Kama utakuwa na kiwango kidogo chakurejesha itakuchukua muda mrefu. Angalia biashara yako ilivyo na ujue ni muda kiasi gani utatumia kulipa mkopo huo.
Umekuwepo kwenye biashara kwa muda gani?
Muda ambao umekuwepo kwenye biashara ni muhimu sana katika maamuzi ya kuchukua mkopo. Kama biashara ndio changa au inaanza ni vyema kuepuka mikopo. Kama umeshaijua biashara vizuri hapa unaweza kuchukua mkopo na kuweka yale maeneo ambayo umeshajua kwa uhakika yanazalisha vizuri.
Hali yako ya kifedha kwenye biashara ikoje kwa sasa?
Je biashara inajiendesha kwa faida au kwa hasara. Kama biashara inajiendesha kwa hasara ni vyema ukajua kwanza chanzo cha hasara kabla hata hujaweka mkopo kwa sababu kama sasa unapata hasara, ukiweka fedha zaidi utapata hasara zaidi.
Ni dhamana kiasi gani unahitajika kuweka ili kupata mkopo?
Kuna mikopo ambayo inahitaji dhamana kubwa na kuna mingine inayohitaji dhamana ndogo. Ni vyema kuijua dhamana kabla hata hujachukua mkopo, usije kuchukua mkopo ambao utaiweka dhamana yako kwenye hatari kubwa ya kuipoteza.
Unahitaji fedha kwa haraka kiasi gani?
Uharaka wako wa kupata fedha za mkopo unaweza kukufanya ukapata mkopo ambao unakusumbua. Kuna taasisi ambazo zinaweza kukupatia mkopo wa haraka sana, lakini pia zikawa na riba kubwa. Na kuna taasisi ambazo itakuchukua muda mpaka upate mkopo ila zikawa na riba ndogo. Ni vyema kuchukua mkopo wakati ambao hauna haraka sana ili uweze kufanya maamuzi sahihi.
JE WEWE NI MJASIRIAMARI AU MFANYA BIASHARA TUTAMBUE TOFAUTI HAPA
Je umeshawahi kushangaa na kujiuliza hivi kuna tofauti gani kati ya Mjasiriamali na Mfanyabiashara ikiwa wote wanaajiri watu, wanatatua matatizo mbalimbali kwa wateja wao, pia wote wanachangia katika ukuaji wa uchumi katika nchi husika au tofauti, je ni nini tofauti sasa?
Tofauti za hawa watu ni kama ifuatavyo
WAZO LA UANZISHAJI
Mfanyabiashara huwa anaanza kwa kuchunguza kitu kinacho zungumzwa Zaidi katika biashara au kuchukuwa wazo kutoka kwa jirani au rafiki kuhusu kitu gani akikifanya au akiwekeza kitamletea faida kubwa.
Mjasiriamari ni mbunifu na mtu asiyehitaji wazo lake kufa, hivyo yuko tayari kuwekeza pesa, mawazo na mda ili kufanikisha wazo lake au jambo analofikilia kulifanya.
FIKRA ZAO KIFEDHA
Mfanyabiashara ni mtu ambae anakuwa na hofu sana juu ya fedha zake kupotea hasa kunapotekea na changamoto mbalimbali kama bei kupungua na suala la uchumi kiujumla.
Mjasiriamari kwake hii ipo tofauti kwasababu huyu ni mtu ambaye anafikilia ni jinsi gani wazo lake litapokelewa na litasaidia vipi jamii, na yupo tayari kurudi
mwanzo kabisa alipoazia, na baadhi ya wajasiriamari huwa hawafikirii kabisa kuhusu pesa.
JINSI WANAVYO JALI MUDA
Mfanyabiashara hujali Zaidi mda na kufanya kazi zake kwa haraka Zaidi kama mpango kazi wake unavyosema.
Mjasiriamari yeye hufanya kazi kama msanii au mwanasayansi maabara, anawezafanya kazi taaratibu lakini lengo lake ni kuhakikisha anafanya kitu bora na tofauti.
MTIZAMO WAO KWA DUNIA
Mfanyabiashara huiona dunia kama fursa ya kufanya maisha yake yaende au kufanya watu wanaoishi kupata huduma mbalimbali kutoka kwake.
Mjasiriamari anaitambua dunia kama wajibu wa yeye kuitendea jambo na sio fursa ya yeye kufanya maendeleo ya maisha yake.
KUHUSU MAFANIKIO
Mfanyabiashari anatambua mafanikio yeye pamoja na wafanyakazi wake pia wawekezaji wenye hisa kwake, wateja pamoja na jamii inayomzunguka.
Mjasiriamari yeye hufanya jambo na kuacha historia ndio ieleze juu ya mafanikio yake.
KUPENDA HALI HATARISHI
Mfanyabiashara anaogopa sana kufanya maamuzi ambayo ni hatarishi na yanaweza kuepelekea kupata hasara kubwa, yuko makini sana kwenye faida na hasara na kujaribu kwa kila hali kuepuka hasara.
Mjasiriamali anapenda kufanya maamuzi hatarishi ambayo yanaweza kumpelekea kufanikiwa au kushindwa, anajua maamuzi ya aina hii ndio yanayowezesha biashara kukua kwa kiwango kikubwa sana. Ni katika maamuzi ya aina hii ambapo wajasiriamali wengi wameweza kupata faida kubwa sana na kukuza biashara zao.
MALENGO MAKUBWA
Mfanyabiashara malengo yake makubwa ni kupata faida, kufikia lengo au kupitiliza lengo alilopanga kifedha.
Mjasiriamali ni mtu anayefikiria jinsi ya kuibadilisha dunia na kuelewa matatizo ili aweze kutatua ni mvumilivu na uweza kufanya kila mbinu aweze kutimiza ndoto zake.
BIASHARA ZENYE FURSA NA ZINAZOLIPA
BIASHARA YA MTANDAO
Hii ni biashara ambayo unaweza kuifanya kwa muda mchache kwa siku au kwa wiki na ukaanza kujitengenezea kipato hata kama kwa sasa bado umeajiriwa. Kupitia biashara hii wewe unakuwa msambazaji wa huduma au bidhaa kwa njia ya kuwaambia wengine uzuri wa bidhaa au huduma zile na wanaponunua wewe unapata kamisheni. Kuna faida nyingine nyingi kupitia biashara hii kama kuweza kutengeneza timu kubwa na ikakuongezea kipato kikubwa.
MIGAHAWA NA FAST FOOD
Angalau kila binadamu anatakiwa kula chakula ili aweze kuishi, Wafanyabiashara wengi wanaofanya biashara hii kiufasaha wanaweza kukua zaidi na kuwa na biashara kubwa sana.
TIBA ASILI NA ZA KITAMADUNI
Kama ilivyo kwa nchi nyingi Afrika tiba asili zimekuwa zikiaminika kuwa bora zaidi. Hata nchi za wenzetu walioendelea kama China hupenda dawa za asili kwani hazina kemikali. Siyo kila mtu anaweza kufanya biashara hizi. Huhitaji uzoefu na lazima upate idhini ya serikali kama tiba ni salama.
VIFAA VYA UJENZI
Watu wanajenga kila siku. Vifaa vya ujenzi hununuliwa na kuisha kabisa madukani. Viwanda haviishii kutengeza bidhaa.Nani hapendi ujenzi?
FAMASIA NA MADAWA
Biashara hii utahitaji elimu na uzoefu lakini faida utaipata. Magonjwa hayaishi. Hivyo watu wanaofanya biashara hii ya kuuza madawa na vifaa vya famasia wamekuwa wakipata mapato mazuri na faida kwasababu ni biashara yenye uhakika wa kuuzika.
BIASHARA YA VIFAA VYA UMEME
Biashara ya vifaa vinavyotumia umeme inalipa duniani kote kwa kiasi kikubwa sana. Fikiri vifaa kama friji, computer. Mjasiriamali mwenye malengo haswa ataipenda zaidi biashara hii.
VIPODOZI
Wanawake wengi hupenda kutumia vipodozi. Jumla ya idadi ya wanawake ni kubwa sana ukilinganisha na idadi ya wanaume, Lakini Wanaume pia hununua vipodozi ivo hii ni fursa nzuri ya Kujiajili pia kutoa huduma kwa walengwa na utapata faida ya kutosha.
SALOON NA UREMBO
Hair dressing na kunyoa ni kama mambo ya lazima kwa mtu yeyote mwenye kuhitaji kuwa mtanashati. Biashara hii inaendelea kuwanufaisha wengi kama ukitoa huduma nzuri na za kipekee.
UBUNIFU WA TATIZO NA UTENGENEZAJI WA PROGRAMU
Inategemea ni tatizo gani unaloweza kuliona katika mazingira uliopo au dunia kwa ujumla, kwa mfano program za kifedha zinazoweza kumsaidia mteja kuelewa mwenendo wa pesa katika biashara zake au programu za kusaidia kupata mawasiliano kwa urahisi n.k hii pia ni fursa inayoweza kumsaidia mtu yeyote au kikundi cha wenye uwezo huu kupata pesa za kutosha kuendeleza biashara zao.
BIASHARA YA MAZAO NA UFUGAJI
Hizi ni kazi ambazo zinadharaulika sana lakini, ndio zinafanya wafanyabiashara wakubwa wanapata mafanikio usifuge au kulima kilimo cha chakula tu bali andaa kilimo ambacho kitakupatia mavuno makubwa na utapata faida kubwa tu, pia utaweza kuanzisha miradi tofauti na utafanikiwa
EDUSPORTSTZ inakutakia maandalizi mema ya siku. inakuomba kulike facebook page yetu au kufollow kupitia blog eneo la follow by email ili kutumiwa habari kwa wakati.
Post a Comment